Tanzania yafikia kiwango cha WHO kutokomeza ukoma
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu
Muktasari:
- Dalili za ugonjwa wa ukoma ni pamoja na mabaka yenye rangi ya shaba mwilini ambayo hayaumi wala hayawashi, bali hupoteza hisia unapoyagusa na yanaweza kujitokeza mahala popote mwilini.
Dar es Salaam. Baada ya miaka mingi ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukoma, Tanzania imeandika historia baada ya kufikia kiwango cha awali cha Shirika la Afya Duniani (WHO) cha kutokomeza ugonjwa huo.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, idadi ya wagonjwa wapya imepungua kutoka 2,297 mwaka 2015 hadi wagonjwa 1,309 mwaka 2023, sawa na punguzo la asilimia 57.
Tamko hilo limetolewa leo Jumapili, Januari 28, 2024 na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu wakati dunia ikiadhimisha siku ya ukoma leo, huku Tanzania ikishuhudia kupungua kwa kiwango cha wagonjwa hao.
“Kwa tafsiri hii, mwaka 2023, nchi yetu ilikuwa na wagonjwa watatu kwa kila watu 100,000, hivyo Tanzania imefika kiwango cha awali cha WHO cha kutokomeza ukoma, yaani chini ya mgonjwa mmoja kati ya watu 10,000 tangu mwaka 2006,” amesema.
Profesa Nagu amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna halmashauri 19 katika mikoa ya Morogoro, Lindi, Dar es Salaam, Mtwara, Kigoma, Tanga, Dodoma, Geita, na Pwani hazijafikia viwango vya utokomezaji.
Akizungumza jana Januari 27, 2024 jijini Dodoma, mratibu wa mpango wa Taifa wa kuthibiti kifua kikuu na ukoma, Dk Deus Kamara amesema kuna juhudi mbalimbali zinafanywa na Serikali kuwatibu wenye dalili na wagonjwa wa ukoma, lengo kuutokomeza kabisa ugonjwa huo.
“Tuna kampeni maalumu ya kutoa hamasa kwa jamii pamoja na kuwafuata wagonjwa hao majumbani na kama itatokea tunawapata, tunatoa tiba kinga kwa watu alioshirikiana nao ili kuwakinga wasipate ugonjwa huo,” alisema Dk Kamara na kuongeza;
“Pamoja na hamasa inayotolewa, bado kuna mikoa yenye maambukizi ya ukoma kwa wastani wa wagonjwa 50 hadi 200 kwa mwaka na hivyo tumeiagiza mikoa hiyo kuhakikisha inaweka juhudi za kudhibiti ugonjwa huu.”
Profesa Nagu amesema nchi ina wajibu wa kuendelea na mapambano ili kutokomeza ukoma katika mikoa hiyo huku akitoa rai kuhusu ugonjwa huo ambao ni miongoni mwa magonjwa yasiyopewa kipaumbele nchini.
“Kila mwanajamii ana wajibu wa kutambua dalili za ukoma na kuhakikisha wote wenye dalili wanafika katika kituo chochote cha kutolea huduma za afya kwa uchunguzi na matibabu,” amesema.
Profesa Nagu amewaagiza waganga wakuu wa mikoa na halmashauri, kushirikiana na vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa ugonjwa wa ukoma katika kaya zote zenye wagonjwa wapya wa ukoma na kutoa tiba.
“Kila Halmashauri nchini ihakikishe inafanya juhudi kuibua wagonjwa, inafuatilia mwenendo wa ugonjwa na kuwa na takwimu sahihi kulingana na maeneo, vijiji au mitaa wanakopatikana,” amesema.
Profesa Nagu amesema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kutoa hamasa kwa jamii juu ya wajibu wa kuendelea kupambana na kuutokomeza kabisa ugonjwa wa ukoma ifikapo mwaka 2030.
Ametaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni pamoja na mabaka yenye rangi ya shaba mwilini ambayo hayaumi wala hayawashi, bali hupoteza hisia unapoyagusa na yanaweza kujitokeza mahala popote mwilini.
Amesema ugonjwa huo unaweza kusababisha ulemavu wa kudumu ikiwa ni pamoja na vidonda sugu mikononi na miguuni, kukakamaa viungo, kuharibu sura ya mtu, kukatika viungo na upofu.
“Ukoma si ugonjwa wa kulogwa, kurithi, wala laana, ni ugonjwa wa kuambukizwa, unatibika na kupona. Hivyo naisihi jamii kuachana na dhana hizo potofu na aina zote za unyanyapaa,” amesisitiza Profesa Nagu.
Maadhimisho ya mwaka huu yamebeba kaulimbiu “Thamini utu; Tokomeza unyanyapaa dhidi ya waathirika wa ukoma” inayochagiza umuhimu wa kila Mtanzania kushiriki katika kutokomeza ugonjwa huo.