Tanzania yapiga hatua udhibiti usalama wa anga

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) Daniel Malanga akiwasilisha majukumu ya mamlaka mbele ya Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza La Wawakilshi Zanzibar lilipotembelea Makao Makuu ya TCAA kujionea na kujifunza shughuli za usimamizi wa sekta ya usafiri wa anga nchini.

Muktasari:

  • Wakati ambao Tanzania inajipanga kujiunga katika soko la pamoja la Usafiri wa anga, viwango vyake vya udhibiti usalama vimeongezeka.

Dar es Salaam. Tanzania imepiga hatua katika uwezo wake wa udhibiti wa usalama katika usafiri wa anga kutoka asilimia 37 miaka 10 iliyopita hadi asilimia 67.3 sasa.

 Viwango hivyo kwa mujibu wa miongozo ya shirika la kimataifa la usafiri wa anga vinazidi kukua wakati ambao Tanzania imeonyesha utayari wa kujiunga na soko la pamoja la ndege Afrika, huku ikieleza soko hilo lina faida kwa mashirika ya ndege nchini.

Hayo yamesemwa leo Jumanne, Aprili 16, 2024 wakati wajumbe wa Baraza la wawakilishi Zanzibar walipotembelea Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) wakiongozana na watendaji wa Mamalaka ya Viwanja vya Ndege Zanzibar (ZAA) kwa ajili ya kujifunza na kuongeza uwezo wa kusimamia anga kwa njia za kisasa zenye usalama zaidi.

Akizungumza katika kikao hicho, Kaimu Mkurugenzi wa TCAA, Daniel Malanga amesema lengo la nchi ni kuhakikisha inakuwa na uwezo wa kudhibiti usalama wa anga lake kwa asilimia 100.

“Kinachofanyika sasa ili kufika huko ni kuendelea kupata wataalamu hasa marubani tuwe nao wa kutosha, pia kuendelea kutoa mafunzo kwa marubani na wahandisi wa ndege. Mpaka sasa marubani wanane wanaendelea kusoma maeneo mbalimbali na wahandisi pia,” amesema Malanga.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha usalama katika usafiri wa anga unakuwa si tatizo kwa upande wa Tanzania, ili kuweka uhuru wa watu kulitumia.

Malanga amesema hata sasa wakati Taifa linapotimiza miaka 60 ya Muungano, mmlaka hiyo itaendelea kusimamia sekta hiyo muhimu kwa kufuata misingi na miongozo yote stahiki ya kitaifa na kimataifa, ili Taifa liendelee kuvutia wawekezaji wengi zaidi katika sekta hiyo adhimu.

Kufuatia hilo, wajumbe wa Baraza la Wawakilshi Zanzibar wamesema usalama wa anga unatakiwa kupewa kipaumbele na kutazamwa kwa upana wake hasa katika kuimarisha huduma za uongozaji ndege, ili kuiwezesha anga kuwa salama na kuleta tija.

Pia, wamaitaka TCAA kuhakikisha wakati wote wanakuwa mstari wa mbele katika kupokea teknolojia mpya za sekta ya anga, ili kuhakikisha Taifa haliachwi nyuma na mageuzi yanayotokea kwa kasi duniani.


Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Yahaya Rashid Abdallah amesema kama nchi inapaswa kujipongeza juu ya sifa mbalimbali inayozipata hasa katika kudhibiti usalama wa usafiri wa anga na hilo limekuwa likithibitishwa kupitia tuzo mbalimbali ambazo nchi imekuwa ikipewa.

“Kazi yetu ni kuendeleza sifa tunazozipata, ili tuendelee kuaminika kama nchi hasa linapokuja suala na matumizi ya viwanja vyetu vya ndege,” amesema Yahaya.