TCAA yafanya mabadiliko ya sheria kuendana mahitaji

Muktasari:

 Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imetoa elimu ya kanuni za masuala ya usafiri wa anga kwa wadau mbalimbali

Dar es Salaam. Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema imefanya mabadiliko ya sheria mbalimbali ndani ya sekta ya anga ili kuendana na nguvu ya soko.

Sheria iliyofanyiwa mabadiliko ni ya usafiri wa anga kifungu cha 80, inavyozungumzia utoaji wa leseni na usajili wa viwanja vidogo vya ndege, utendaji kazi wa helikopta,udhibiti wa vihatarishi na utendaji kazi wa ndege kwa jumla pamoja na uwezeshaji wa usafiri wa anga.

Maboresho hayo yametajwa kuwa ni mahususi kwa abiria na wasafirishaji wa mizigo kabla na baada ya safari.

Marekebisho ya sheria hizo zimetangazwa leo Jumatatu, Machi 25, 2024 Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari wakati wa mkutano wa kupokea maoni ya wadau wa sekta ya anga kuhusu Soko la Pamoja la Afrika pamoja na mabadiliko ya sheria mbalimbali za sekta ya anga.

Johari amesema mabadiliko hayo yamelenga kuondoa changamoto zilizobainika wakati wa usafirishaji wa abiria na mizigo.

“Kuna maboresho mengi yanayolenga kukabiliana na changamoto ambazo zimeonekana katika usafiri wa anga wa watu na usafirishaji wa mizigo,

Baadhi ya masuala mapya ni kama vile usitishwaji wa safari, kuchelewa kwa ndege na wasafiri wenye mahitaji maalum,” amesema.

Kulingana na kanuni zitakazosimamia uwezeshaji wa usafiri wa anga za mwaka 2024, abiria watakaosubiri kuunganisha ndege kwenda mataifa mengine endapo safari itakatishwa au ndege kuchelewa, wataruhusiwa kuondoka ndani ya uwanja kwa ajili ya kutafuta malazi.

Pia, mamlaka husika itaanda mpangilio utakaowafanya abiria kubaki ndani ya uwanja wa ndege kwa saa 24.

Kwa kesi ya namna hiyo, kanuni hizo zimeelekeza kuwa, abiria atagharamiwa kifungua kinywa, chakula na mahitaji mengine kwa muda atakaoongeza kusubiri usafiri,

Vilevile usafiri wa abiria kutoka eneo la uwanja wa ndege hadi anakokwenda kupata malazi kwa mujibu wa kanuni hizo, zitagharamiwa na mtoa huduma husika.

Pia, mtoa huduma huyo atahakikisha hakuna abiria anayelalamika kwa huduma zao huku wakihitajika kuweka uangalizi wa karibu kwa abiria wenye watoto.

Johari amesema sekta ya anga inatumia sheria na ni lazima zifanyiwe mabadiliko mara kwa mara.

“Tunasimamia sekta hii kwa kutumia sheria na sheria hizi lazima tuzibadili mara kwa mara, kama tunavyojua  soko  la anga halifungamani na upande wowote lazima uliheshimu na unyumbulike nalo, sheria zinafungamana na upande  sasa ni lazima  tuziandike ili ziendane na soko hivyo tunazibadili  ili soko lisitukatae,’’ amesema.

Amesema ili kuendana na matakwa ya soko la anga ni lazima kama nchi kujipanga kuwa na  kanuni na sheria zenye kuhakikisha Tanzania inakua kwenye sekta ya anga na inazingatia usalama wa abiria.

Mdau wa Usafirishaji wa Anga Juma Fimbo akizungumzia mabadiliko ya sheria za sekta ya anga, amesema ni muhimu kwani usalama na umadhubuti wa nchi ni vitu vinavyopaswa kupewa kipaumbele.

“Kanuni lazima zibadilike ili kuchochea mabadiliko katika sekta ya anga kiuchumi na kiusalama,” amesema.