Tanzania yasikitishwa Denmark kufunga ubalozi

Tanzania yasikitishwa Denmark kufunga ubalozi

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imeeleza kusikitishwa na hatua ya Serikali ya Denmark kuamua kufunga shughuli za Ubalozi wake nchini Tanzania ifikapo mwaka 2024.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeeleza kusikitishwa na hatua ya Serikali ya Denmark kuamua kufunga shughuli za Ubalozi wake nchini Tanzania ifikapo mwaka 2024.

Denmark jana ilitangaza uamuzi huo ambao ulihusishwa na mkakati wao mpya wa masuala ya mambo ya nje. Mbali na Tanzania pia nchi hiyo itafunga ubalozi wake nchini Argentina, Ubalozi mdogo wa Chongqing nchini China na ujumbe wa biashara huko Barcelona (Uhispania).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula leo Jumamosi Agosti 28, 2021 amesema hatua hiyo ya Denmark inasikitisha ikizingatiwa kuwa hivi karibuni Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikifanya jitihada za kufufua na kuimarisha diplomasia na uhusiano wa nchi rafiki ikiwemo Denmark.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo imeeleza kulikuwa na jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini pamoja na kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria.

Aidha taarifa hiyo inaeleza  Balozi Mulamula jana  alifanya mazungumzo kwa njia ya mtandao na Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Denmark,  Flemming Mortensen ambapo walikubaliana kuendelea kushirikiana na Mortensen anatarajia kuzulu nchini siku zijazo.

“Pamoja na hatua iliyochukuliwa na Denmark, ni matarajio ya Tanzania kuwa Serikali ya Denmark itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono ajenda za Tanzania katika Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na majukwaa mengine ya kimataifa,” inaeleza taarifa hiyo.