Tanzania yatajwa maambukizi ya TB duniani

Naibu Katibu Mkuu Wizara Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Maduhu Kazi akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kikao cha Baraza dogo la wafanyakazi wa Wizara ya mambo ya Ndani Nchi.  Picha na Lilian Lucas

Muktasari:

  • Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kukabiliana na ugonjwa wa kifua kikuu(TB) imeanza kutoa elimu ya kujikinga na kudhibiti ugonjwa huo kwa watendaji wake mahali pa kazi kutokana na huduma wanazotoa kwa makundi ya watu.

Morogoro. Kila mwaka, Tanzania inakadiriwa kuwa watu 130, 000 ambao wanasumbuliwa na ugonjwa Kifua Kikuu (TB), huku wakiwa hawajui, ama hawajaanza matibabu na hivyo kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi 30 zinazotoa mchango wa maambukizi ya ugonjwa huo duniani.

Mshauri wa mtandao wa wapambanaji wa TB kwenye sekta ya umma na binafsi nchini, unaoratibiwa na Wizara ya Afya, Oscar Mukasa amesema hayo Novemba 17,2023 mjini Morogoro wakati wa kikao cha Baraza dogo la wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani Nchi.

Mukasa amesema mgonjwa ambaye anaumwa na ameanza tiba walau kwa wiki mbili, haambukizi ila mtu anayeumwa na hajaanza tiba, huambukiza watu 15 mpaka 20 kwa mwezi, na kwamba hiyo ndio sababu kuzitaka sekta zote kukabiliana na ugonjwa huo.

Akitoa mada ya mpango wa ujumuishi wa sekta mbalimbali kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Kifua Kikuu, Mukasa amesema mpango huo unajaribu kuzileta sekta zote kwa pamoja kwa ajili ya mapambano ya TB.

“Mfano kwenye Wizara ya Elimu ndiko kuna wanafunzi wanakaa bweni, Wizara ya Mambo ya Ndani kama Magereza wafungwa kukaa pamoja, Uhamiaji wapo wakimbizi, hivyo Wizara ya Afya inakuwa inatoa utaalamu na uratibu kwa kushirikiana wizara husika kwa lengo la kupambana na TB,” amesema.

Aidha, amesema kumekuwa na mapokeo potofu kuwa mwenye TB lazima awe na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) jambo ambalo si sahihi, na kwamba wamekuwa wakitoa elimu ili kuondokana na mambo ya unyanyapaa mahali pa kazi, na namna ya utoaji huduma pindi wanapoona dalili.

“Kwa sababu TB ni ugonjwa unaoambukizwa kwa urahisi kwa njia ya hewa ndio maana watu wengi wanapata maambukizi kwa wingi na idadi kuwa kubwa, cha msingi wafanyakazi wanatakiwa kupata ufahamu wa hali ya juu kwenye maeneo yao ya kazi na hata wanapoishi,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu Wizara Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Maduhu Kazi akizungumza katika kikao hicho amewataka viongozi wa baraza hilo kufanyakazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu, huku akieleza kuwa pamoja na kuwepo kwa mafanikio, baadhi ya changamoto zilizopo wanatakiwa kukabiliana nazo kwa kuwashirikisha wafanyakazi waliopo chini yao.

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Kazi, amewataka kuendelea kusimamia uwepo wa amani, utulivu na usalama wa raia na mali zake nchini.

“Zingatieni maadili ya utumishi wa umma ili kuweza kuleta matokeo chanja ya utendaji kazi wenye tija kwa nchi yetu,”amesema.