Tanzania yatoa msaada Sh2.3 bilioni tetemeko la ardhi Uturuki

Muktasari:

  • Tanzania imetoa msaada wa Sh2.3 bilioni kwa nchi ya Uturuki kutokana na madhara yaliyotokana na tetemeko la ardhi Februari mwaka huu na kuua takribani watu 56,000.

Dar es Saalam. Tanzania imetoa msaada wa Dola za Marekani 1,000,000 (Sh2.3 bilioni) kwa nchi ya Uturuki kutokana na madhara yaliyotokana na tetemeko la ardhi Februari mwaka huu na kuua takribani watu 56,000.

Taarifa iliyowekwa jana katika ukurasa wa Twitter wa Msemaji mkuu wa Serikali, Greson Msigwa jana Machi 23, 2023, imesema Tanzania imekabidhi msaada huo wa kibinadamu kwa Balozi wa Uturuki, Gen Yacoub Mohammed.

Tetemeko hilo la ardhi la kipimo cha 7.8 liliikumba jimbo la Kusini mwa Uturuki la Hatay na eneo la Aleppo Kaskazini mwa Syria huku watu 125,626 wakijeruhiwa  na zaidi ya watu milioni 24 nyumba zao zikiathirika.

Shirika la Utangazaji la Uingireza la BBC Swahili, liliripoti majengo takribani 200,089 yakiharibiwa.

Imeelezwa kwamba tetemeko hilo limesababisha hasara ya jumla ya takribani Dola109 bilioni za Marekani.

Shirika la Kukabiliana na Majanga la AFAD liliripoti kuwa maelfu ya watu walihudumiwa na kupatiwa msaada wa dharura wakati wa uokoaji.

Kituo cha Kunasa Majanga Ulaya cha Seismoloji (EMSC) kilisema tetemeko hilo lilipiga kwa kina kidogo cha kilomita 2 (maili 1.2).

Shirika hilo lilirekodi matetemeko mawili zaidi yenye ukubwa wa 5.2 karibu dakika 20 baada ya lile la kwanza kutokea.