GST yataja mikoa iliyo hatarini kwa tetemeko

Dar es Salaam. Mikoa 11 inayopitiwa na ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki imetakiwa kuhakikisha inazingatia viwango halisi vya ujenzi vinavyojumuisha ushauri wa kitaalamu wa jiolojia ya eneo husika, na kuepuka ujenzi wa nyumba katika miinuko yenye mawe na mipasuko ya miamba.

Ushauri huo umetolewa na Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), katika mahojiano na gazeti hili, ikiwa umepita mwezi mmoja tangu yalipotokea matetemeko katika nchi za Uturuki na Syria, yaliyosababisha vifo zaidi ya watu 41,000 na watu zaidi ya milioni 1.5 kukosa makazi.

“Sisi hatuna mamlaka ya kukagua majengo yamejengwa vipi, kuna mamlaka nyingine,” anasema mwanajiolojia kutoka GST, Gabriel Mbogomi.

Kwa mujibu wa GST, mikoa hiyo ni Dodoma, Katavi, Singida, Rukwa, Songwe, Mbeya, Ruvuma, Manyara, Arusha, Kigoma na Kagera.

Hata hivyo, Mbogomi anafafanua kuwa haimaanishi mikoa hiyo inayokumbwa na matetemeko ya mara kwa mara, ndiyo inaathirika zaidi kuliko mikoa mingine. “Inawezekana kabisa tetemeko likatokea mkoa mwingine likaleta madhara kuliko lingetokea mikoa hiyo,” alisema. Mbali na Uturuki, hivi karibuni hapa nchini kulitokea matetemeko ya ardhi katika maeneo ya wilaya ya Manyoni kwenye mpaka kati ya Mkoa wa Singida na Dodoma yakiwa na ukubwa wa 4.3 na 4.9 katika kipimo cha richa. Kwa mujibu wa Sensa ya Majengo ya Mwaka 2022, kuna zaidi ya majengo 13.9 milioni, yakiwamo magorofa 61,258 Tanzania bara.

“Ni hatari sana, ndio maana Serikali iko kwenye utekelezaji wa mpango wa urasimishaji makazi holela, kama alikosea kujenga bila kuzingatia tahadhari za kitalaamu basi ataamua mwenyewe baada ya kumuelimisha,” alisema Dk Mukuki Hante, Mkurugenzi wa uendelezaji vijiji na miji wa Tamisemi.

Kwa upande wa Profesa Abel Kinyondo kutoka Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alisema hakukuwa na sababu ya kuwa na kiwango kikubwa cha madhara kwa wananchi kila yanapotokea matetemeko nchini, kutokana na mifumo ya ufuatiliaji iliyopo Serikali chini idara za mipango miji. “Tungekuwa na utawala bora, hao wapanga miji wangewajibika kwa kusababisha hali ya ujenzi usiozingatia taratibu na ushauri wa kitaalamu, kwa sababu tunajua tupo kwenye mkondo wa bonde la ufa na tunajua matetemeko yanaweza kutokea wakati wowote, tunapaswa kuchukua tahadhari za kitaalamu mapema. “Kwenye mataifa ya Ulaya yenye changamoto za kutokea matetetemeko tayari wameshachukua hatua, ikiwamo kujenga nyumba za mbao,” alisema Profesa Kinyondo.

Akilizungumzia suala hilo, Awadhi Salim, Mkurugenzi Msaidizi wa Nyumba na Uendelezaji miliki kutoka Idara ya Maendeleo ya Makazi, alisema kuna baadhi ya wananchi hufanya ujenzi holela bila kuzingatia ushauri wa wataalamu. “Kisheria, kila nyumba inayojengwa inatakiwa kuombewa kibali. Kwenye maombi yako utaambatanisha na mchoro wa aina ya jengo na mahali unapotaka kujenga,” alisema Salim.

Akifafanua kuhusu Mkoa wa Dodoma, Dk Hante alisema pamoja na kuwa miongoni mwa mikoa iliyo hatarini kukumbwa na matetemeko, utafiti wa kujihakikishia uwezo wa ardhi ya mji huo kabla ya Serikali kuhamia ulibaini hali sio mbaya. “Tuligundua mtu anaweza kujenga hata jengo la gorofa 25, changamoto ya pale ni mfumo wa kutoa ‘control number’ za utoaji wa hati za viwanja, haufanyi kazi vizuri, kwa hiyo inasababisha watu kujenga bila kufuata taratibu, lakini wengine wanakimbia tu kulipia,” alisema.

Naye Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye alisema tayari ofisi yake ilishaanza kutoa maelekezo kwa kila anayeomba kibali cha ujenzi, kupatiwa ushauri juu ya mchoro wa jengo analotaka kujenga kwa kuzingatia mazingira na maelekezo ya jiolojia.