Tetemeko la ardhi lazua taharuki Dodoma, Singida

Muktasari:

  • Tetemeko hilo limetokea mara tatu kwa nyakati tofauti na kuzua taharuki kwa wananchi wa mikoa ya Singida na Dodoma.

Dar es Salaam. Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 4.3 na 4.9 limeikumba mikoa ya Singida na Dodoma leo Februari 17,2023 Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imethibitisha.

 Katika taarifa ambayo imetolewa na GST, imesema haijapokea taarifa za madhara yoyote kufuatia tetemeko hilo ambalo limezua taharuki kubwa kwa wakazi wa mikoa hiyo na maeneo ya jirani.

"Ikumbukwe kwamba mikoa ya Singida na Dodoma imepitiwa na Ukanda wa Bonde la Ufa la Afrika Mashariki mkondo wa Mashariki. Maeneo ya ukanda wa Bonde la Ufa kwa kawaida ni maeneo tete ya mabadiliko ya kijiolojia ambayo hukumbwa na matetemeko ya ardhi na milipuko ya volkano," imesema taarifa hiyo.

Pia, Februari 9 mwaka tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kipimo cha 4.7 lilitokea visiwani Pemba na kusikika katika baadhi ya miji nchi ya Tanzania na Kenya.

Vilevile ni wiki mbili zimepita tangu limetokea tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.8 nchini Uturuki, Sria ambapo maelfu ya watu wamepoteza maisha na kujeruhiwa na majengo na miundombinu kadhaa kuharibiwa.