Tanzania yatoa somo urasimishaji biashara

Naibu katibu Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Biashara na Viwanda Sempeno Nyari (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji Brela Geofrey Nyaisa (kushoto) wakiwa na wageni kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki, Sudan Kusini na Burundi katika ofisi za Brela zilizopo jijini Dar es Salaam.
Muktasari:
Tanzania imeonekana kufanya vizuri katika urasimishaji wa biashara ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan
Dar es Salaam. Kuimarishwa kwa mifumo ya kidijitali katika urasimishaji wa biashara kumetajwa kuwa sababu ya Tanzania kupokea wageni nchi za Burundi na Sudan Kusini kwa ajili ya kujifunza mazingira bora ya biashara.
Akizungumza leo Jumatatu Machi 25, 2024 Kaimu Katibu Mkuu wa Idara ya Maendelo ya Biashara na Viwanda, Sempeno Nyari alipowakaribisha wageni hao, amesema kumekuwa na mchakato wa kubadilisha na kurekebisha sheria zote zenye mkinzamo ili kuendelea kuhamasisha mazingira ya uendeshaji wa biashara.
"Katika moja ya mambo makubwa yaliyofanywa ni mfumo mmoja wa kuweza kusajili biashara na kuweza kupata leseni (ORS) ambao kila mwananchi au mfanyabiashara anaweza kuingia," amesema Nyari.
Amesema Tanzania imeonekana kufanya vizuri katika urasimishaji wa biashara, ikiwa ni kutekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuna kuwa na mifumo imara na Jumuiya ya Afrika Mashariki inazungumza lugha moja.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji, Wakala wa Usajili wa biashara na Leseni (Brela), Geofrey Nyaisa amesema licha ya kutumika kwa mifumo bado kuna changamoto ya kutosomana kwa mifumo katika taasisi.
Akitoa mfano wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), amesema endapo mifumo ingekuwa inasomana isingesumbua wafanyabiashara na kufanya mambo yao kwa haraka.
"Licha ya changamoto hiyo lakini wenzetu wameona tunajitahidi na wameamua kuja kujifunza kwetu masuala yote ya mifumo na kwa kuanzia tutawaonyesha tulikuwa wapi,tupo wapi na tunaelekea wapi," amesema Nyaisa.
Pia, amesema hakuna jambo lolote linalokosa changamoto hivyo hata kwenye eneo la mifumo haitegemewi kila kitu kitakwenda kikiwa kimenyooka lakini wanachojaribu kufanya ni kupunguza urasimu na matumizi mazima ya makaratasi.
Kwa upande wake, Charles Omusana, kutoka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki amesema Brela ina uzoefu wa uendeshaji wa kwenye mifumo tangu mwaka 2018, hivyo itawasidia nchi hizo katika kuimarisha mifumo ya sekta ya biashara.
"Tunaelewa kuwa sekta binafsi kwenye biashara ndizo zinazoleta maendeleo katika nchi, hivyo ili kuboresha sekta hiyo nchi ya Sudan Kusini na Burundi kufika hapa tunaamini kuwa watapata elimu iliyobora kuhusu mifumo,"amesema.
Msajili Mkuu wa Biashara wa Sudan Kusini, Amadol Anyuat amesema watakapojifunza itakuwa rahisi kuwaandaa na kuwashawishi wafanyabiashara wa Sudan na Tanzania kuweza kushirikiana kwenye uwekezaji.
Msajili Mkuu wa Maendeleo ya Biashara wa Burundi, Alida Mugisha amesema wameanza kutumia mfumo katika usajili wa biashara kuanzia mwaka 2022 na wamekuwa wanakutana na changamoto, hivyo wapo nchini kwa ajili ya kujifunza namna ya kukabiliana nazo.
"Wenzetu wameanza muda mrefu tofauti na sisi kwa hiyo tutakachojifunza hapa itatupa urahisi wa kukabiliana na changamoto zote na tunaimani tutafikia malengo kama Brela," amesema.