Dk Chao: Biashara inahitaji kanuni ili isianguke

Muktasari:
- Wajasiriamali kutofuata kanuni za kuwezesha biashara kumetajwa kusababisha biashara nyingi kushindwa kufanya vizuri kwa muda mrefu sokoni.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Sayansi ya Masoko nchini Dk Emmanuel Chao, amesema biashara yoyote inapaswa ilindwe na kuongozwa na kanuni ili isianguke.
Amesema asilimia 80 hadi 90 biashara za wafanyabiashara wadogo kwa wa kati hazifiki mwaka wa tano sokoni kwa kuwa kanuni za kibiashara hazizingatiwi na biashara haianguki ikiwa sokoni bali inaanguka ikiwa bado haijaingia sokoni.
Amesema mipango ndio inayomfanya mfanyabiashara kuishi sokoni akitolea mfano, mtu aliyepanga safari ya kwenda mkoani Moshi lazima aweke mipango ya ununuzi mafuta hivyo mafuta hayo yatakapomfikisha ndipo mipango yake ilipokuwa imeelekezwa hata endapo mafuta yakiishia njiani.
Dk Chao ambaye ni Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Mzumbe ametoa sababu hiyo leo Alhamisi, Aprili 27, 2023 katika kongamano la wafanyabiashara wachanga, wadogo na kati lillilofanyika katika ukumbi wa Super Dome uliopo Masaki na limeandaliwa na Mwananchi Communications Limited (MCL) na kukutanisha wadau waliojadili nini kifanyike kuwawezesha biashara zao ziwe na ufanisi.
Amesema moja ya kanuni bora ya biashara ni kupanga namna ya kuendesha soko ambapo kimsingi wateja wengi huwa wananunua mtazamo wa bidhaa.
"Lazima tuelewe Sayansi ya soko inaanzia kabla ya biashara kuanza hivyo unapoingia kwenye soko utambue wateja wananunua hisia na mtazamo uliofungashwa kwenye bidhaa. Mtazamo huo huwa unaishi kwa muda mrefu kwa mteja" amesema Chao.
Amesema wafanyabiashara lazima wakubali kujifunza namna ya kupanga mipango kabla ya kuingia sokoni. Ambapo watazalisha bidhaa bora na zenye uaminifu.
Amesema suala la mtazamo wa wateja kwenye bidhaa ni jambo la kuzingatiwa akitolea mfano chapa ya bidhaa zenye uaminifu kutoka nchi mbalimbali duniani.
Amesema mteja akiona chapa ya bidhaa imetoka nchi fulani anaweza kuwa na imani nayo kama nchi inazalisha bidhaa bora na wateja wengine hawanunui bidhaa kutoka nchi ambayo haijawekeza kwenye mipango mizuri na uzalishaji wa bidhaa bora.
Kongamano hilo la (MSMEs) limedhaminiwa na Ashton, benki ya CRDB, Kampuni ya Usafirishaji DHL, Benki ya Stanbic, Benki ya NMB, Clouds media na Ukumbi wa Mikutano wa Dome.