Tarura yapewa fedha kiduchu, Kamati ya Bunge yatoa angalizo

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dennis Londo akizungumza wakati akitoa maoni ya kamati kuhusiana na makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) leo Jumanne Aprili 16, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Kamati ya Bunge yasema hali hiyo hairidhishi, Tarura itashindwa kutekeleza miradi kwa ufanisi.

Dodoma. Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, imesema licha ya Serikali kutenga zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura), fedha zilizopelekwa zimefikia asilimia 45.7.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne Aprili 16, 2024 na mwenyekiti wa kamati hiyo, Dennis Londo wakati akitoa maoni ya kamati kuhusu makadirio na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), iliyosomwa na Waziri, Mohamed Mchengerwa.

“Katika kipindi cha mwaka 2023/2024 Serikali ilitenga zaidi ya Sh1 trilioni kwa ajili ya Tarura. Hata hivyo, upelekaji wa fedha hizo ulifikia asilimia 45.7. Upokeaji huu hauridhishi na hautaiwezesha Tarura kutekeleza miradi yake kwa ufanisi,” amesema.

Amesema katika kipindi cha kuanzia mwishoni mwa mwaka 2023 hadi sasa, nchi imekumbwa na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya barabara katika maeneo mbalimbali kutokana na kunyesha kwa mvua kubwa za el nino.

“Hali hii imesababisha barabara nyingi hasa za vijijini kutokupitika kabisa kutokana na uharibifu huo na hivyo kusababisha huduma mbalimbali za usafiri kwa wananchi kuwa ngumu,” amesema.

Londo amesema kutokana na hali hiyo, Tamisemi imeweka mkakati wa kuzirejesha barabara hizo katika hali yake ya kawaida kwa kuitumia Tarura.

“Azma ya Tamisemi kusimamia miradi ya ujenzi wa barabara na miundombinu inayoendana na barabara hizo inaweza kufanikiwa kwa kuongeza fedha kwa Tarura,” amesema.

Kamati inashauri Serikali izingatie ushauri iliyoutoa katika Bunge la Bajeti lililopita.

“Kamati inaishauri Serikali kupeleka fedha Tarura kikamilifu na kwa wakati; na kutoa bajeti ya dharura kwa kuzingatia ombi maalumu lililotolewa na kamati kwa ajili ya kusaidia urejeshaji wa miundombinu hiyo,” amesema.


Upandaji miti

Londo amesema ushauri wa kamati ni kuwa Serikali ianzishe programu maalumu katika shule za msingi na sekondari kwa kila mwanafunzi anayeanza shule kupanda na kuutunza mti wakati wa maisha yake yote awapo shuleni.

Amesema halmashauri zielekezwe kuweka sheria ndogo kwa ajili ya kusimamia wajibu wa wananchi kupanda miti na kuitunza kwenye maeneo ya makazi yao.

“Kwa kuwa kuratibu na kusimamia mkakati wa kuongeza ukusanyaji wa mapato ni sehemu ya lengo la Tamisemi, uboreshaji wa mazingira ni sehemu muhimu katika kuziwezesha halmashauri kujiongezea kipato kutokana na mazingira kuweza kuwa kama chazo cha mapato kwa ajili ya biashara ya kaboni (hewa ukaa),” amesema.

Kamati imeishauri Tamisemi ijenge uwezo wa kitengo kinachosimamia biashara ya kaboni, ili kutoa ushauri wa kitaalamu kwa halmashauri nchini.

“Serikali za vijiji, kata na halmashauri zipime maeneo na kumilikishwa maeneo hayo kama hatua ya kuweza kuhifadhi na kuitunza misitu wenyewe ili kuwanufaisha katika biashara ya kaboni,” amesema.

Waziri Mchengerwa akisoma hotuba alitoa maelekezo kwa viongozi wa mikoa na wilaya kuratibu usimamizi wa masuala ya uhifadhi na utunzaji wa misitu, wanyamapori, nyuki, vyanzo vya maji, athari za mabadiliko ya tabianchi.

“Pia, fursa za mabadiliko hayo kupitia biashara ya kaboni na udhibiti wa uzalishaji taka katika mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa,” amesema.

Kamati ya Bunge pia imeeleza matumizi ya fedha yasiyo sahihi yanayofanywa na halmashauri katika utekelezaji wa bajeti.

Londo amesema uchambuzi wa taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya Tamisemi kwa mwaka 2023/2024 kwa ngazi ya halmashauri umebaini zipo taasisi zinazoandaa makongamano, warsha na semina na kuwaalika wataalamu wa halmashauri, huku zikiwaelekeza wakurugenzi wa halmasahuri kugharimia.

“Hali hii imekuwa ikizifanya halmashauri kutumia fedha ambazo awali hazikuwa kwenye bajeti yao, hivyo kufanya shughuli nyingine za kibajeti katika halmasahuri kutokutekelezwa,” amesema.

Kamati imeishauri Tamisemi kuelekeza mialiko yoyote itakayoenda kwa wakurugenzi iambatane na taarifa ya walioandaa matukio hayo kuonyesha kuwajibika kwao kibajeti.