Tatizo la ajira kwa vijana laundiwa mkakati

Saturday November 28 2020
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Jukwaa la wadau wa kilimo wasio wa kiserikali (Ansaf) limeandaa mjadala utakaoshirikisha wadau wa kada tofauti kujadili tatizo la ajira kwa vijana.                     

Akizungumza na waandishi wa habari mkurugenzi mtendaji wa Ansaf, Audax Rukonge amesema lengo la kongamano hilo ni kuangalia jinsi sekta ya kilimo na viwanda vinavyoweza kuwapatia ajira vijana.

Kauli mbiu yetu inasema 'Kufungua fursa za ajira kwa vijana kupitia kilimo na uchumi wa viwanda’.

"Kila mwaka kuna zaidi ya wanafunzi 700,000 wanahitimu masomo katika ngazi mbalimbali na hao ndiyo wanatafuta ajira.”

"Tukifungua milango ya ajira katika sekta ya kilimo tutawawezesha kuwa wakulima na ujasiriamali," amesema Rukonge.

Amesema katika mjadala huo watajikita katika mbinu za kugundua fursa kupitia kilimo, mifugo na uvuvi.

Advertisement

"Tunaangalia mnyororo mzima tangu mazao  yakiwa mbegu hadi mkulima anapovuna.

Kwenye mifugo, Tanzania ina mifugo mingi, lakini wanahitaji kunenepeshwa.”

"Vijana wanaweza kujiajiri kama wazalishaji wa mbegu bora za mifugo. Kuna fursa ya chakula cha mifugo, vijana wanaweza kujiajiri," amesema.

Kuhusu changamoto zinazomkabili kijana amesema watajadili jinsi mila na desturi, sheria na sera zinavyowakwaza vijana kupata ajira.

"Sera zetu zinawezeshaje vijana kupata mikopo, kumiliki ardhi na kupata biashara. Taasisi wezeshi zinachangiaje kuwawezesha vijana kupata ajira," amehoji.

Akizungumzia manufaa ya kongamano hilo, Rukonge amesema kwa wameendesha mijadala kama hiyo kwa miaka 13 iliyopita na imeleta mafanikio ikiwa pamoja na kuanzishwa kwa mfuko wa mazingira kwa wakulima.

"Mwaka jana mgeni rasmi  alikuwa George Simbachawene aliyekuwa Waziri wa nchi ofisi ya makamu wa rais,  tuliunda kikundi kazi cha kuchangia mazingira, tumeendelea na waziri Mussa Zungu, sasa mfuko unachangiwa kwa wingi,” amesema.

Amesema mijadala hiyo imewezesha kutengwa kwa akaunti maalum ya mikopo kwa vijana na wanawake katika halmashauri ili kutekeleza agizo la serikali la kutenga asilimia 10 ya mapato ya halmashauri.

Alisema kongamano hilo litakalofanyikia jijini Dodoma Desemba 3 na 4, 2020  litahusisha wadau wakiwemo vijana waliojiajiri katika kilimo.

Advertisement