Tatizo la ugonjwa usiojulikana Chunya lachukua sura mpya, daktari asimamishwa

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila 

Muktasari:

  • Sakata la kuibuka kwa ugonjwa wa ajabu katika kata ya Ifumbo wilaya ya Chunya mkoani hapa kwa wananchi kutapika damu na kupoteza maisha limeingia sura mpya huku baadhi ya wananchi wakitilia shaka matumizi ya maji yasiyo  salama kutokana na baadhi ya vijiji kuwa na changamoto hiyo. 

Dar es Salaam. Viongozi wa Serikali wametua wilayani Chunya kushughulikia sakata la taarifa za kuwepo ugonjwa usiojulikana katika Kata ya Ifumbo huku Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Doroth Gwajima akiagiza kusimamishwa kazi kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Dk Felista Kisandu.

Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila akiambatana na kamati ya ulinzi na usalama alikwenda huko Chunya jana na kutangaza ataunda kamati ya kuchunguza tatizo hilo.

Sakata hilo liliibuka juzi kwenye kikao cha Baraza la Madiwani wa Wilaya ya Chunya baada ya Diwani wa Kata ya Ifumbo, Weston Mpyila kueleza kuwepo kwa ugonjwa huo.

Iliripotiwa kuwa kulikuwa na vifo vya watu 15 na wengine 50 kuugua jambo lililozua sintofahamu.

Wizara ya Afya ilitoa tamko juzi likieleza kuwa Dk Gwajima ametuma timu ya wataalamu na kuagiza apewe taarifa ifikapo jana mchana.

Jana jioni Dk, Gwajima alitoa tamko la wizara yake akiagiza kusimamishwa kazi kwa Dk Kisandu kupisha uchunguzi kufuatia sakata la kusambaa kwa taarifa ya mlipuko wa ugonjwa usiofahamika katika kata ya Ifumbo.

Dk Gwajima amesema Dk Kisandu amepewa adhabu hiyo kwa kukiuka mwongozo wa utoaji wa taarifa za milipuko kama ilivyoelezwa kwenye ya Sheria ya Afya kwa Umma (Public Health Act) ya mwaka 2009 kuwa msemaji wa mwisho ni Waziri wa Afya baada ya kujiridhisha na si vinginevyo.

Waziri Dk Gwajima aliwakumbusha na kuwasisitiza wataalamu wote wenye dhamana ya afya kufanya kazi kwa kufuata miongozo yote kwa mujibu wa dhamana ya majukumu waliyoaminiwa.

“Kutokana na kadhia hii ambayo imeleta taharuki isiyo ya lazima naiagiza mamlaka ya ajira ya Dk Felista Kisandu ambaye ni Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya ichukue hatua za kumsimamisha kazi ili kupisha uchunguzi chini ya Baraza la Madaktari na taarifa nipate ndani ya siku 10,” alisema Dk Gwajima.

Alisema katika Kata ya Ifumbo, Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya hakuna mlipuko wa ugonjwa wowote uliothibitishwa wala hakuna janga lolote la kiafya kama ilivyoripotiwa na vyombo vya habari.

“Kuhusu madai ya kuwepo kwa wagonjwa wanaougua kutapika damu timu imebaini kuwa kwenye rekodi za afya za Zahanati ya Ifumbo ni wagonjwa watatu pekee ndiyo waliwahi kuripotiwa ambapo wa kwanza ilikuwa Septemba 7, 2020 ambaye alifariki akiwa anapata matibabu ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo.

“Mgonjwa mwingine alifika kwenye zahanati hiyo Desemba 28, 2020 na kupata matibabu kisha akapewa rufaa kwenda hospitali ya halmashauri ambapo alitibiwa na kupona. Mgonjwa wa tatu aliripotiwa Februari 6, 2021 na kupata matibabu kwenye zahanati hiyo kisha akapewa rufaa kwenda Hospitali ya Halmashauri na hata sasa bado amelazwa,” aliongeza.

Dk Gwajima alisema, timu ya wataalamu imefanya mahojiano na wananchi na kubaini hakuna vifo 15 kwa mara moja vya wagonjwa wanaodaiwa kuwa na dalili za kutapika damu kama ilivyoripotiwa na m Diwani wa Ifumbo na takwimu hizo hazijawahi kuripotiwa popote.

“Imethibitika kuwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Chunya, Dk Felista Kisandu naye hana hizo takwimu kwani naye amekiri kusikia tu kutoka kwa wananchi na diwani.

“Kwa mazingira haya Dk Kisandu hakuchukua hatua za kujiridhisha na taarifa hizo kwa utaratibu wa miongozo ya kitaalamu badala yake akaungana na Mheshimiwa Diwani kwenye ajenda hiyo pasipo ushahidi wa kitaalamu na matokeo yake kuleta taharuki kwenye jamii bila sababu,” aliongeza Dk Gwajima.

Pia katika ziara yake, Chalamila alizungumza na wananchi ambao walimuomba kuboreshewa miundombinu ya barabara, kituo cha afya ili wanapougua waweze kupata huduma mapema na kuokoa maisha yao.

Chalamila pia ametuma timu ya wataalamu kwenda kuchunguza sababu za kuibuka kwa ugonjwa huo na kuagiza wagonjwa waliopo wachukuliwe sampuli zao ili zikapimwe na kujua chanzo chake.

Naye Diwani Weston Mpyila alisema watu wa huko wanatilia shaka maji yanayotumiwa na wananchi huenda yakawa chanzo cha ugonjwa huo kwa kuwa wilaya hiyo ina changamoto ya maji safi na salama.

Imeandikwa na Hawa Mathias, Mery Mwaisenye na Harriet Makwetta.