Tatizo la uhaba wa fedha za kigeni laibuka bungeni

Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Ezra John Chiwelesa akizungumza wakati wakati akizungumza bungeni leo Jumanne Juni 7, 2023 jijini Dodoma. Picha na Edwin Mjwahuzi.

Muktasari:

  • Sakata la uhaba wa fedha za kigeni kwenye benki limetinga bungeni baada ya Mbunge wa Biharamuro Magharibi (CCM), Ezra Chiwelesa kuhoji

Dodoma. Mbunge wa Biharamulo Magharibi (CCM), Ezra John Chiwelesa amesema wafanyabiashara ndogondogo na wa kati wamekuwa wakipata shida ya fedha za kigeni huku benki zikiweka viwango vya fedha zinazotoa kwa siku.Akiuliza swali leo Juni 7, 2023 bungeni, Chiwelesa amesema katika Benki ya CRDB huwezi kupata zaidi ya dola za marekani 1,000 huku NMB na NBC hauwezi kutoa Dola za Marekani 500.

“Kama mtu anataka kutuma fedha nyingi nje ya nchi, inabidi kutumia muda mwingi kuzunguka katika mabenki kukusanya fedha. Nini mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa tunawapeleka wafanyabiashara kwenye ndoto zao waweze kufanya biashara zao vizuri bila kukwama,”alisema.

Akijibu Chande amesema tayari Serikali imechukua hatua kadhaa ili kuepukana na hilo na kumuomba mbunge kuwa na subira changamoto hiyo itatatuliwa.

Katika swali la msingi mbunge huyo alihoji nini kauli ya Serikali juu ya ucheleweshaji wa fedha zinazotumwa nje ya nchi kutokana na benki nyingi kuwa na uhaba wa fedha za kigeni.

Akijibu Chande amesema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania imechukua hatua kadhaa katika kupunguza athari kwenye soko la ndani la fedha za kigeni ili kusaidia shughuli za biashara na miamala kuendelea kufanyika.

Amezitaja hatua hizo ni pamoja na kuanzia Machi 2023, BoT imeongeza kiasi cha fedha za kigeni kinachouzwa katika soko la jumla la fedha za kigeni kutoka Dola za Marekani milioni 1 hadi Dola za Marekani milioni 2 kila siku.

“Kuongeza kiwango kinachoruhusiwa kuuzwa kwa muamala mmoja kwa njia ya rejareja kwenye soko la fedha za kigeni baina ya mabenki kutoka dola za Marekani 250,000 hadi Dola 500,000,”amesema.

Amesema katika kuhakikisha ukwasi wa shilingi ya Tanzania unabakia katika viwango vinavyoendana na mahitaji halisi ya kiuchumi, kwa kutumia nyenzo mbalimbali za sera ya fedha.

“Benki za biashara nchini zimeendelea kutunza amana ya kutosha katika akaunti kwenye benki nje ya nchi ili kufanikisha miamala ya ulipaji wa bidhaa na huduma mbalimbali zinazoagizwa na kuuzwa nje ya nchi.

Amezielekeza benki zote nchini, kuhakikisha kuwa zina akiba ya kutosha ya fedha za kigeni kabla ya kupokea fedha kutoka kwa mteja anayetarajia kuzituma nje ya nchi ili kuepuka ucheleweshaji.