Tawa wakabidhiwa magari tisa kusaidia shughuli za uhifadhi

Muktasari:
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) Meja Jenerali (Mstaafu) Hamisi Semfuko amekabidhi magari tisa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uhifadhi.
Dodoma. Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa) Meja Jenerali (Mstaafu) Hamisi Semfuko amekabidhi magari tisa kwa ajili ya shughuli mbalimbali za uhifadhi.
Magari hayo aina ya Toyota Land Cruiser 'Hard Top' matano na Suzuki Jimny, manne yamekabidhiwa kwa menejimenti ya Tawa iliyoongozwa na Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi, Sylivester Mushi, aliyemwakilisha Kamishna wa Uhifadhi, Mabula Misungwi Nyanda.
Magari ya Toyota Land Cruiser yatatumiwa kwa shughuli za doria na utawala huku Suzuki zikitarajiwa kutumika kwenye ufuatiliaji (Monitoring) wanyamapori jamii ya faru katika Mapori ya Akiba ya Maswa na Ikorongo na Grumeti.
Kwa mujibu wa kitengo cha mawasiliano Serikali cha Tawa makabidhiano hayo yalifanyika katika ofisi za makao makuu ya mamlaka hiyo Morogoro.
Akizungumza katika makabidhiano hayo Morogoro, Meja Jenerali mstaafu Semfuko ameitaka Menejimenti ya Tawa kuyatunza magari hayo ili yafanye kazi kwa ufanisi uliokusudiwa.
Aidha, sambamba na kukabidhi magari hayo, Mwenyekiti huyo pia amezindua ujenzi wa miundombinu ya utalii ikiwepo barabara yenye urefu wa kilometa 42, ujenzi wa geti la kuingilia watalii na nyumba za watumishi katika Pori la Akiba Wami-Mbiki.