TAWA yatoa elimu kuhusu wanyamapori waharibifu

Mkuu wa dawati la Ujirani Mwema wa Mamlaka ya Usimamizi wa wanyamapori Tanzania (TAWA), Twaha Twaibu akitoa elimu katika moja ya vijiji katika Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro. Lilian Lucas.
Muktasari:
- Elimu ya Ujirani Mwema kuhusu wanyamapori wakali na waharibifu yatolewa kwa umma na jamii yatakiw kuzingatia maelekezo ya wataalamu.
Morogoro. Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imeishauri jamii kuacha tabia ya kujenga makazi karibu na maeneo ya hifadhi za mbuga za wanyamapori ili kuepuka hatari zinazoweza kutokea kutokana na wanyama wakali na waharibifu kama tembo, nyati, mamba na kiboko.
Kauli hiyo imetolewa na Mhifadhi Mkuu anaesimamia Dawati la Ujirani Mwema kutoka TAWA PC, Twaha Twaibu wakati akizungumza na Mwananchi Digital juu athari za kufanya shughuli za kibinadamu karibu na hifadhi za wanyamapori.
"Wananchi wengi wanaopata madhara ya wanyamapori ni wale wanaoishi karibu kabisa na hifadhi sasa kama jamii inatakiwa kuepuka kujenga nyumba, ama kulima mashamba kwa karibu, hii itasaidia sana majanga kupungua," amesema Twaibu
Mhifadhi Twaibu ameitaka jamii kuzingatia maelekezo yanayotolewa na wataalamu wa wanyamapori kwa ajili ya kuepukana na madhara yatokanayo na Wanyamapori hao.
Aidha ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa haraka pindi wanyamapori hao wanapoingia katika makazi ama mashamba na kuacha tabia ya kupiga nao picha kwani kitendo hicho kinahatarisha maisha yao.
Katika hatua nyingine Mkuu huyo wa dawati la ujirani mwema wa TAWA, Twaibu ametumia fursa hiyo Kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi wa TAWA kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa kinara katika masuala ya uhifadhi, na utalii.
Kwa upande weke Afisa wanyamapori wa TAWA, Joseph Mnyai amesema kuwa kunafaida nyingi zinazopatikana kupitia uwindaji wa kitalii pamoja na utalii wa picha ikiwemo fedha zinazopatikana kwenda kuchangia shughuli za kimaendeleo kwa wananchi wanaishi kando na Mapori ya Akiba, Mapori Tengefu na maeneo ya Ardhioevu.