Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Tazara inavyoweza kulinda barabara zisiharibike

Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya kusheherekea miaka 50 ya kuanzishwa kwa Shirika la Reli Tanzania na Zambia (Tazara), zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda ameyasema hayo kwenye uzinduzi wa wiki ya  kusheherekea miaka 50 ya kuanzishwa kwa shirika hilo.

Dar es Salaam. Shirika la Reli Tanzania na Zambia (Tazara), limeelezwa ni muhimu kuzilinda barabara kwa kubeba mizigo inayobebwa na malori yanayokwenda Congo, Zambia na Malawi.

Hayo yamesema leo Jumanne Juni 30 na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sixtus Mapunda, kwenye uzinduzi wa wiki ya kusherehekea miaka 50 ya kuanzishwa kwa shirika hilo, zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Mapunda amesema kwa sasa asilimia 50 ya mizigo inayokuja bandarini ndio inatoka nje ya Tanzania na asilimia 50 inayobaki inatumika ndani ya nchi.

"Katika hiyo asilimia 50 inayotumika nchini, asilimia 10 ni mizigo inayotumika nje ya mkoa wa Dar es Salaam huku 90 ikibaki Dar es Salaam.

Pia, asilimia 90 ya mizigo inatumika Dar es Salaam, asilimia 67 hubaki Temeke...ikimaanisha ufanisi wa bandari kwa mizigo inayokwenda nje, asilimia 65 hadi 70 inapita njia ambayo Tazara inaweza ikatoa huduma," amefafanua Mapunda.

Kutokana na hilo amesema Tazara ni muhimu kwenye kulinda barabara zisiharibike kutokana na malori.

Pia amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali wa kuwekeza kwenye bandari kunasababisha ongezeko la mizigo mara mbili ifikapo mwaka 2030.

"Hivyo maboresho ya Tazara kwa sasa hivi ni maamuzi ya busara na ya msingi yatakayoenda kufanya bandari yetu ya Dar es Salaam kutoa huduma katika kiwango cha hali ya juu," amesema Mapunda.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema ana imani miaka 50 ya Tazara ni ya kimapinduzi na inaamini itaileta Tazara mpya.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tazara, Bruno Chinga’ndu amesema Serikali za Tanzania na Zambia zimeanza kutekeleza mpango mkubwa wa kuifufua reli hiyo ambao utaibadilisha na kuwa njia ya kisasa, yenye ufanisi na  ushindani katika sekta ya usafirishaji na huduma za ugavi.

“Tumeingia katika makubaliano ya ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP) na mkandarasi mwenye uwezo mkubwa wa kimataifa, CECC, ambaye amejenga reli katika nchi mbalimbali za Afrika ikiwemo Ethiopia na Nigeria,” amesema Chinga’ndu

Mkurugenzi Mkuu wa Tazara, Bruno Chinga’ndu, akizungumza kwenye uzinduzi wa wiki ya  kusheherekea miaka 50 ya kuanzishwa kwa Shirika la Reli Tanzania na Zambia (Tazara), zilizofanyika jijini Dar es Salaam.

Amesema kupitia uwekezaji wa kimkakati katika miundombinu, mabehewa na injini za reli, pamoja na mifumo ya uendeshaji, Tazara itaweka msingi wa kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo, kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi wa shughuli zake.

“Tunaweka msingi wa kuongeza uwezo wa usafirishaji wa mizigo, kuboresha huduma kwa wateja na kuongeza ufanisi wa uendeshaji,” amesema.

Awali, Meneja Mkuu wa Tazara Dar es Salaam, Fuwad Abdallah akielezea historia ya reli hiyo, amesema ni mradi uliyoandikwa katika historia ya Afrika kama ishara ya uungwana na ukombozi.

Abdallah amesema Julai 14, 1976, reli hiyo ndio ilianza rasmi kufanya kazi, ikiwa ni zawadi kutoka serikali ya watu wa China kwa mkopo usiokua na riba.

"Makubaliano ya ujenzi wa reli hiyo yalifanyika Septemba 5, 1967 jijini Beijing Jamhuri ya Watu wa China na ujenzi ulianza Oktoba 1970 na ulikamilika Juni 1975 na kukabidhiwa rasmi Julai 1976.

Hata hivyo amesema ujenzi huo ulikuwa na changamoto kubwa hasa maeneo kati ya Mlimba na Makambako lililojumuisha mahandaki 18 na madaraja 46.

Amesema Tazara ilikuwa chombo cha ukombozi na kueleza kuwa baada ya Ian Smith kuitangaza UDI Rhodesia 1965, Zambia ilikosa ushoroba unaoiunga na bandari. na hivyo Tazara  ikawa "Reli ya Uhuru" iliyoiwezesha Zambia kudumisha uhuru wake na kuisaidia harakati za ukombozi  Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia na Angola.

Wakati kiuchumi Abdallah amesema Tazara imekuwa shoroba la biashara, ikifanya Dar es Salaam kuwa kituo kikuu cha usafirishaji wa madini ambapo miji kama Mbeya, Mlimba, Kisaki, Ifakara na Makambako imekua kwa haraka.