Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

TBA yapambana kutekeleza agizo la Waziri Mkuu

Jengo la Utumishi linalojengwa na Wakala wa Majengo nchini (TBA), lililopo mji wa Serikali Mtumba Dodoma likiwa limefikia asilimia 97, ikiwa ni kasi inayoendana na agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Muktasari:

  • Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umesema umefikia asilimia 97 ya ujenzi wa jengo la utumishi lililopo mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.

Dodoma. Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), imefikia asilimia 97 ya ujenzi wa jengo la Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora lililopo mji wa Serikali Mtumba nje kidogo ya Jiji la Dodoma.

Kasi ya ujenzi wa jengo hilo la Utumishi litakalogharimu zaidi ya Sh21.4 bilioni mpaka kukamilika kwake inaendana na agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa lililotaka majengo yote kukamilika Desemba mwaka 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari waliofika eneo hilo kuangalia maendeleo ya mradi, Mtendaji Mkuu wa TBA, Daud Kondoro amesema wanatarajia kukabidhi mradi huo ifikapo Novemba 30, mwaka huu 2023.

Amesema Serikali ilitoa Sh69 bilioni ambazo zimeelekezwa kwenye miradi ya ujenzi na ukarabati wa nyumba za watumishi na viongozi wa Serikali ambapo TBA inaratibu, kushauri, pamoja na kujenga miradi hiyo.

Hivyo, Kondoro amebainisha kwamba utekelezaji wa miradi kutokana na fedha hizo kwa sasa mbali na jengo la utumishi, majengo mengine pia wanayoyajenga na kuyasimamia yamefikia asilimia 70 hadi 80.

Kadhalika, amesema kasi ya ujenzi inaendana na ubora na uimara dhidi ya changamoto kama tetemeko ambalo linaweza kutokea katika eneo hilo.

Katika kutekeleza hilo amesema kwamba wamezingatia upimaji mzuri kiasi cha kwamba ikitokea tetemeko kusitokee madhara. Hivyo walichagua kujenga eneo lisilo na nyufa.

"Iliwahi kutokea tetemeko hapa timu yetu ilikuja kuangalia lakini hakukuwa na madhara yeyote. Niwapongeze timu nzima kwa kuzingatia ubora na uimara wa ujenzi kwa viwango vya juu," amesema.

Vilevile, ili kuendana na teknolojia amesema wamezingatia nyenzo za mawasiliano ya kisasa katika majengo pamoja na miundombinu ya walemavu ikiwemo lifti ili kila mmoja asipate kikwazo wakati majengo yakianza kutumika.


Kaimu Meneja wa TBA Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Wambura amesema wanasimamia zaidi ya miradi 30 ya taasisi mbalimbali za Serikali mkoani humo ambapo kwa Mtumba wana miradi 18.

Amesema moja ya faida katika utekelezaji wa miradi hiyo ni ununuzi wa vifaa vya ndani ya nchi pamoja na kutoa ajira kwa Watanzania.

Kauli hiyo inaungwa mkono na Mustapha Hassan ambaye ni fundi wa madirisha ya Aluminum anayefanya kazi katika jengo la utumushi kwa zaidi ya miezi saba sasa.

"Naishukuru TBA mkono unaenda kinywani, niko hapa muda mrefu nafanya kazi katika huu mradi," amesema Hassan.

Vilevile, Shamira Moshi, Aneth Amir pamoja na Merciana Charles wanafanya kazi ya utunzaji bustani ambapo wameishukuru Serikali na TBA kwa ujumla.