TBS: Ukaguzi magari kutoka nje utafanyika nchini

Muktasari:

Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema kuanzia Machi Mosi mwaka huu utaratibu wote wa kukagua magari kutoka nje ya nchi utakuwa ukifanyika baada ya gari husika kuwasili hapa nchini.

Dar es Salaam. Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limesema kuanzia Machi Mosi mwaka huu utaratibu wote wa kukagua magari kutoka nje ya nchi utakuwa ukifanyika baada ya gari husika kuwasili hapa nchini.

Kwa sasa TBS inakagua magari kutoka nje kupitia mawakala watatu nchini Japan na mwingine Dubai, Falme za Kiarabu, ambao mikataba yao itakoma hivi karibuni.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana na Mkuu wa itengo cha uhusiano wa TBS, Rhoida Andusamile ilieleza kuwa magari yote yatakayosafirishwa kuanzia Machi Mosi yatakaguliwa katika Bandari ya Dar es Salaam.

“Vyeti vyote vya ukaguzi vitakavyotolewa na mawakala hao kwa magari yatakayosafirishwa kuanzia Machi Mosi mwaka huu havitambulika na TBS,” alisema Andusamile katika taarifa hiyo.

Mbali na hilo, Andusamile amesema magari yatakayopimwa bandari na kutokidhi matakwa ya viwango yatahitaji kufanyiwa matengenezo nje ya bandari kisha kupelekwa kupimwa kwenye ghala la UDA lililopo mkabala na bandarini Dar.

“Shirika litandelea kuhakikisha kuwa magari yote yaliyotumika na kuingizwa nchini yanakidhi matakwa ya kiwango cha magari yaliyotumika,” alisema Andusamile.

Andusamile alisema taasisi hiyo imepata eneo la UDA karibu na bandari ya Dar es Salaam, ambalo alifafanua ni kubwa na linatosha kufanya shughuli hivyo kwa urahisi na haraka.

“Hakutakuwa na malipo ya ziada wakati wa uchunguzi, tutatumia viwango vilevile walivyokuwa wanatumia mawakala wetu na tutajitahidi kufanya haraka ndani ya muda,” alisema.

Alisema awali TBS ilikuwa inatumia mawakala hao kwa mkataba wa miaka mitatumitatu lakini sasa ukiwa unaelekea ukingoni wameona shughuli hiyo wawe wanaifanya wenyewe kwa kuwa wanao uwezo wa kufanya hivyo.

“Sasa fedha zilizokuwa zikilipwa kwa ajili ya kazi hiyo zitabaki ndani na gereji zetu za ndani zitapata kipato pindi gari litakapoonekana linahitaji kufanyiwa matengenezo,” alisema Andusamile.

Ngoja tuone

Mmoja wa wauzaji wa magari hapa nchini, Hashim Said alisema uamuzi huo wa TBS huenda ukaongeza au kupunguza bei ya magari lakini wanasubiri kuona viwango vya gharama za ukaguzi huo vitakavyotangazwa na TBS.

“Japan tulikuwa tunatozwa Dola 300 kama laki 7 hivi za Tanzania sasa sijajua hao wataweka shilingi ngapi, wakiongeza wataongeza bei ya magari ambayo tayari imeongezwa na kodi lakini wakipunguza itakuwa ni ahueni,” alisema Said.

Wakati wakala huyo akidai kuwa wanalipa kiasi hicho cha Dola 300 (Sh 692,000), msemaji wa TBS, Andusamile alitaja kuwa kiwango cha malipo hayo ni Dola 150 (Sh 346,000) ambacho ndio kilikuwa kinatakiwa kutozwa na wakala hao.

Said, alidai wasiwasi mwingine ni pale ambapo mamlaka za Japan zitataka ukaguzi huo kufanyika huko na hivyo ukaguzi kufanyika mara mbili.