TCU yatangaza dirisha la udahili masomo elimu ya juu

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa.

Muktasari:

  • Wakati Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) likitangaza matokeo ya kidato cha sita, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la awali la udahili wa wanafunzi kwa mwaka wa masomo 2023/24 hadi Agosti 4, 2023.

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imekufungua dirisha la udahili wa wanafunzi wa elimu ya juu kwa awamu ya kwanza wa mwaka wa masomo 2023/24 zikiwa zimepita siku mbili tangu Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) kutangaza matokeo ya kidato cha sita.

Shughuli hiyo ya udahili itafanyika kuanzia leo Jumamosi Julai 15 hadi Agosti 4, 2023.

Kupitia dirisha hilo wanafunzi, wataweza kuomba nafasi za masomo katika vyuo mbalimbali vya elimu ya juu wanavyotaka kusoma.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 15, 2023 jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema maombi hayo yanatakiwa kutumwa moja kwa moja kwenye vyuo ambavyo muombaji amevichagua na kuchagua programu za masomo anazozipenda huku akisisitiza maelekezo mahsusi ya jinsi ya kutuma maombi yanatolewa na vyuo husika.

"Vigezo na sifa katika programu mbalimbali za masomo vinapatikana katika tovuti za vyuo husika na katika vitabu vya mwongozo wa maombi ya udahili vinavyopatikana kwenye tovuti ya TCU,” amesema.

Profesa Kihampa amewataka waombaji kusoma mwongozo wa udahili uliotolewa na TCU kwa makini na kuelewa kabla ya kuanza kutuma maombi ya udahili, kuingia katika tovuti za vyuo ili kujua taratibu za kutuma maombi pamoja na kuwasiliana na vyuo moja kwa moja na kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kujiridhisha kabla ya kutuma maombi.

Vilevile, amewataka waombaji wenye vyeti vilivyotolewa na mabaraza ya mitihani nje ya nchi wawasilishe vyeti vyao Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwa vyeti vya Elimu ya Sekondari au Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Nactvet) kwa vyeti vya stashahada ili kupata ithibati ya ulinganifu wa sifa zao kabla ya kutuma maombi ya udahili.

Pia, Profesa Kihampa ametumia fursa hiyo kutangaza rasmi kuanza kwa maonyesho ya taasisi za elimu ya juu kuanzia rasmi Julai 17 hadi 22 katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

Maonyesho hayo yatazinduliwa Jumanne Julai 18, 2023 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda.

“Takribani taasisi 80 za elimu ya juu zinatarajiwa kushiriki na kuonyesha huduma mbalimbali wanazozitoa ikiwemo kufanya udahili kwa wanafunzi,” amesema Profesa Kihampa.