Kozi hizi tano ‘usipime’ vyuo vikuu

Wakati idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa katika vyuo viku ikizidi kuongezeka kila mwaka, imebainika kuwa wanafunzi wengi wamekuwa wakikimbilia kusoma kozi za ualimu, biashara, sayansi ya jamii, tiba na sayansi za afya na sheria.

Kozi hizo mbali na kudahili idadi kubwa ya wanafunzi katika vyuo, pia wanafunzi wanaochagua kozi hizo wamekuwa wakiongezeka kila mwaka, huku wadau wakitaja fursa za ajira, urahisi wa masomo husika na motisha inayotolewa ikiwemo mikopo kuwa sababu.

Kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za elimu ya vyuo vikuu nchini ya mwaka 2022 iliyotolewa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kwa ajili ya kusomea fani ya ualimu katika vyuo mbalimbali nchini imeongezeka kwa asilimia 12 kati ya mwaka 2019 hadi 2022.

Wanafunzi waliosajiliwa mwaka 2022 walifikia 58,021 kutoka wanafunzi 51,489 waliodahiliwa mwaka 2020/2021.
Licha ya ualimu kuongoza kwa kupokea wanafunzi wengi lakini fani ya biashara na afya kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyotoka Mei mwaka huu, ndizo zinazoongoza kwa kushuhudia ongezeko kubwa la wanafunzi na katika kipindi cha miaka mitatu kwa asilimia 25 na asilimia 24.

Fani ya biashara ilifikisha wanafunzi 48,397 mwaka 2022 kutoka wanafunzi 38,462 mwaka 2020/2021, huku afya ikifikisha wanafunzi 30,589 kutoka 24,642 katika mtiririko wa awali.
Fani ya sayansi ya jamii ambayo mwaka 2021/2022 iliipiku fani ya afya katika udahili wa wanafunzi, nayo imeshuhudia ukuaji kwa asilimia 19.8 katika kipindi hicho.
 

Sababu kukimbilia ualimu

Akizungumia suala hilo, Muhanyi Nkoronko ambaye ni mtafiti wa masuala ya elimu alisema wanafunzi wengi wamekuwa wakikimbilia ualimu kutokana na kasumba iliyojengeka kuwa kozi hiyo ni rahisi.
Urahisi huo si katika kusoma pekee bali pia katika kupata nafasi ya kusoma kozi hiyo katika vyuo na hata ufaulu wa watu wanaochukuliwa si mkubwa sana ikilinganishwa na fani nyingine.

"Mtu anaona akisoma ualimu ni rahisi kuliko kusoma udaktari ambao pia ana vigezo, pia kuna upatikanaji wa ajira hivi karibuni Serikali imeanza kutoa ajira. Pia ajira kwa sekta binafsi soko limekuwa kubwa, hivyo kwa ajili ya kuajirika imefanya wengi wasome kozi ya ualimu kuliko fani nyingine," alisema Nkoronko.

Alisema licha ya ajira na urahisi katika kusoma pia alama za ufaulu ambazo zinamfanya mtu kusoma ualimu si kubwa sana ikilinganisha na fani nyingine zenye ushindani, hivyo badala ya kupambania nafasi chache katika kozi nyingine, wanaamua kubaki huko.

Katika upande wa kozi ya biashara alisema umechangiwa na mwamko wa watu kufanya vitu vya kijasiriamali hasa katika dunia ya sasa ambayo imekuwa ikihamasisha watu kujiajiri.
Pia alisema baadhi ya familia zimekuwa zikiwashauri watoto wao kusoma elimu ya biashara, ili wakitoka hapo waweze kusimamia shughuli za familia.

"Hii pia inaenda kulekule kwa kuangalia namna gani anaweza kufanya baada ya kumaliza chuo, anaweza kujiendelea katika ufanyaji biashara au anaweza kupata ajira katika kampuni nyingi zinazofanya uwekezaji kwa sasa,’’ alieleza.
 

Ajira kwa walimu

Tangu mwaka 2021 Serikali imeanza kutoa tena ajira kwa walimu ikiwa ni baada ya kusitishwa kwa miaka kadhaa.

Katika kupunguza pengo la walimu lililokuwapo, Juni 202, walimu 6,949 waliajiriwa ambapo kati yao 3,949 walikuwa wa shule za msingi na 3,000 wa sekondari.

Baadaye Juni mwaka uliofuatia walimu 9,800 waliajiriwa ambapo kati yao 5,000 walikuwa wa shule za msingi na 4800 ni wa sekondari.

Ajira za walimu zimeendelea kutolewa tena ambapo pia mwaka huu, walimu 13,130 wa shule za msingi na sekondari waliajiriwa.

Mbali na walimu pia katika miaka hiyo wahitimu wa kada ya afya hawakuachwa nyuma. Mwaka 2023 pekee nafasi 8,070 zilitolewa kwa watumishi wa ngazi ya zahanati, vituo vya afya na hopsitali.

Mwaka 2021, wataalamu wa afya 2,726 waliajiriwa huku mwaka 2022 wakiajiriwa watumishi 7612 wa kada ya afya.
 

Wasemavyo wachambuzi

Dk Luka Mkonongwa kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), alisema ajira kwa walimu haijawa motisha tena kwa sababu tangu mwaka 2015 hawakuajiriwa lakini waliendelea kuongezeka vyuoni.

"Kinachoendelea kwa sasa ni motisha iliyokuwapo kwa watu wanaosoma ualimu, ukisoma ualimu mkopo unapewa asilimia 100 ndiyo ilibaki kuwa motisha ya wanafunzi wengi kuingia ualimu," alisema.

Pia alisema wanafunzi waliendelea kuchagua fani hiyo kwani wanapohitimu wanakuwa na nafasi ya kufanya kazi maeneo tofauti badala ya shuleni pekee.

"Vyuoni tunaona wanagraduate (wanahitimu) wengi lakini si wote wanaingia katika sekta ya elimu. Ukienda jeshini, benki utawakuta kwa sababu mtaala ni mpana na unafundisha vitu tofauti tofaut," alisema.

"Hata akimaliza bado akiomba fani nyingine anaweza kumudu, kitu kikubwa ambacho wengi wanavutiwa nacho ni mkopo lakini kama mtu atapata ajira moja kwa moja hapana," aliongeza Dk Mkonongwa.

Japokuwa alisema kwa sasa ile kasi ya uajiri walimu imerudi huenda kuanzia hapo ndiyo inaweza kuelezewa kama motisha.

Katika upande wa biashara, alisema uwekezaji unaofanywa katika sekta binafsi umekuwa ukifanya watu wengi kusoma fani hiyo.

Pia baadhi wamekuwa wakitumia kile wanachokipata chuoni kama maarifa yatakayowawezesha wao kujiajiri na kufikia malengo yao katika biashara.
"Lakini huku pia mtu mmoja anaweza kujikuta amevuta wengi kusomea kozi hiyo kisa alisoma akafanikiwa, baadhi wamekuwa wanaangalia upepo kuangalia rafiki yangu yuko wapi," alisema Dk Mkonongwa.

Alisema hiyo bado ni changamoto ambayo vijana wanahitaji kupewa ushauri nasihi katika utambuzi wa fani kwa kuangalia kile wanachokichagua kinakuwa kimefanyiwa tathmini ya kutosha.

"Hii ni kati ya vitu ambavyo ni changamoto katika vyuo vyetu tunatakiwa kusisitiza zaidi kuhusu suala la uchaguzi wa fani, mtoto anapotaka kuingia fani fulani afanye uamuzi ambao tayari ana taarifa za kutosha na si kusema baba yake amesema nisome,"

Akizungumzia suala hilo, Kassana Salehe ambaye ni mwalimu mstaafu alisema zamani watoto walikuwa wakisoma kile ambacho mzazi anahitaji na mara zote ualimu ulikuwa kimbilio kwa sababu ya uhakika wa ajira.

"Miaka ya nyuma ulikuwa ukisoma chuo ukimaliza tu unaingia moja kwa moja katika ajira, tofauti na miaka michache iliyopita lakini pia wazazi walikuwa na mchango mkubwa katika kufanya watoto wasome kozi fulani kwa sababu ya ushawishi waliokuwa nao," alisema Kasana ambaye watoto wake watatu kati ya watano ni walimu.

Lakini si hilo tu, kwa upande wa wanafunzi wanaosoma ualimu walisema wamechagua kozi hiyo kutokana na mapenzi yao sambamba na urahisi wa upatikanaji wa mikopo.
"Ukisoma ualimu kuwa na asilimia kubwa ya kupata mkopo, familia zetu wengine ni duni haziwezi kumudu asilimia 100 ya gharama za chuo kulipa wenyewe hivyo tunawasaidia," alisema Martha Nyambalya ambaye ni mwanafunzi wa ualimu.

Alisema pia kuendelea kuanza kutolewa kwa ajira za walimu ni suala ambalo linawavuta kwa sasa na linawapa uhakika hapo baadaye kuwa wanaziinua familia zao kiuchumi.

"Familia zetu zinaamini ukifika chuo wewe unaweza kusaidia ndugu zako wa nyuma. Wakati naingia chuo mwaka 2021 ndiyo mwaka ambao mwanga wa ajira za ualimu ulianza kurejea, tunaomba hili liendelee hivi ili tuweze kujikwamua kwa kufanyia kazi kile ambacho tulisomea.
Baadhi ya wanafunzi waliosomea fani hizo walieleza kuwa walisukumwa na mapenzi ya fani husika.

"Udaktari ni kitu ambacho nimekua nacho tangu nikiwa mdogo, katika familia yetu hakuna anayefanya kazi hii lakini mimi nilisema nitaifanya na niliweka bidii tangu mwanzo ili kufikia malengo yangu," anasema Paschalia Hilary ambaye ni mhitimu wa udaktari.