Tehama kutumika ukusanywaji takwimu sekta ya afya
Muktasari:
- Ili kuhakikisha takwimu zinakuwa sahihi na zinapatikana kwa urahisi, Wizara ya Afya imeanza kutumia mifumo ya kielektroniki itakayowezesha kupatikana kwa takwimu sahihi.
Morogoro. Wizara ya Afya imewataka Waratibu wa Mfumo wa Takwimu na Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya nchini (HMIS), kuhakikisha ukusanyaji wa takwimu kielektroniki unafika kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zote nchini.
Agizo lime limetolewa leo Alhamisi, Novemba 16, 2023 mkoani Morogoro na Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk John Jingu wakati akifungua mkutano wa mwaka wa waratibu hao akiwaeleza kuwa takwimu ni nyenzo muhimu.
Dk amesema kila mratibu katika eneo lake ahakikishe anakuwa sahihi kwenye takwimu na zipatikane kwa wakati na hivyo kuwezesha uamuzi kufanyika kwa haraka kwa usahihi.
“Takwimu ni moja ya nyenzo muhimu ya kazi na hii inasaidia kujipima na kujitathimini kama wizara na nchi ili kwenye utendaji kazi tuwe sahihi, hatuhitaji kufanya kwa kubahatisha pale tunapopanga bajeti zetu,” amesema.
Amesema takwimu zinasaidia kufikia malengo ya nchi ikiwemo kupambana na magonjwa, kuonyesha utoshelevu au upungufu wa dawa na kuona namna bora ya kutafuta suluhisho.
Pia Katibu Mkuu huyo amesema umefika wakati kwa Wizara ya Afya kuwa na mifumo michache ya kielektroniki ambayo ni rahisi kusomana na kuacha mifumo mingi inayoongeza gharama na haisomani
Dk Jingu amesema takwimu zinazokusanywa nje ya mfumo wa DHIS2, zinatakiwa kupatikana katika mfumo huo ili kuiwezesha sekta ya afya kupata viashiria vya kitaifa.
Kwa mujibu wa Dk Jingu, takwimu zinazokusanywa nje ya mfumo wa wa DHIS2 ni pamoja na GoT-HoMIS, Emr, VIMS-BID, na CTC.
Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Tumaini Nagu amesema upatikanaji wa sahihi wa takwimu utawezesha uwepo na upatikanaji wa dawa kwa kipimo sahihi kulingana na uhitaji wa maeneo husika.
Profesa Nagu amesema sekta ya afya inaendelea kuwekeza katika upatikanaji wa huduma ya afya kwa jamii, huku elimu ya kinga na utambuzi wa magonjwa kwa mapema ukiendelea kutolewa kwa jamii.
“Takwimu sahihi na zinazotolewa kwa wakati ni nguzo ya mafanikio ya juhudi hizi,” amesema Profesa Nagu.
Ameeleza kuwa Wizara ya afya ina jukumu la kuhakikisha linatoa huduma bora za tiba na huduma za kinga nchini kote na kwamba huduma hizo haziwezi kuwa bora kama hakutakuwa na takwimu sahihi.
Amewataka wataalamu wa afya ambao ni waidhinishaji wa dawa kutumia takwimu zao kwa usahihi, ili kuondokana na tatizo la kuwa na dawa zilizoisha muda wa matumizi.
“Kuna wakati tulikuwa tunafanya tathimini ya dawa za malaria na kiwango cha wagonjwa kilichoonekana kuwa na malaria ni takribani watu 6 milioni lakini dawa zilizotumika za malaria zilikuwa mara mbili ya 12 milioni na data zote zilitokana na mifumo tofauti,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Afya, Claud Kumalija amesema malengo ya kikao ni kufanya tathmini ya hali ya sasa ya takwimu za afya na kuazimia, kujadili bunifu mpya zitakazolenga kuwezesha mifumo ya takwimu za afya kusomana kupitia mfumo wa DHIS2.
“Pia tunalenga kuwezesha takwimu kuwafikia wahitaji kwa njia rahisi ya simu za mikononi ili ziweze kutumika katika mipango na maamuzi katika sekta ya afya nchini..