Tembo yaua watu wawili Tanga
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Edward Bukombe
Muktasari:
- Ni mwanamke na mwanaume wilayani Korogwe
Korogwe: Watu wawili akiwemo mwanaume mmoja na mwanamke wamekufa baada ya kushambuliwa na Tembo huko katika vijiji viwili tofauti vya Halmashauri ya wilaya ya Korogwe, mkoani Tanga.
Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Edward Bukombe alisema tukio hilo lilitokea jana Agusti 19, 2018 saa moja asubuhi katika kata za Kalalani na Kizara kwenye vijiji vilivyopo mpakani mwa hifadhi ya mbuga ya Mkomazi.
Kamanda Bukombe aliwataja majina ya watu hao waliokufa kuwa ni Jumaa Kanju (24) mkazi wa Bombo Majimoto, kata ya Kizara na Habiba Ramadhani (70) mkazi wa Mtoni Bombo Kalalani. Alisema kuwa watu walishambuliwa Agosti 19.
Alisema kikundi cha Tembo kiliwashambulia kwa kuwakanyaga kanyaga marehemu hao na kusababisha majeraha sehemu za kichwani, tumboni na miguuni.
Aliongeza kusema kuwa miili ya marehemu imezikwa jana baada ya polisi kufika eneo la tukio na kujiridhisha juu ya kile kilichotokea na kutoa ruksa kwa ndugu wa marehemu kufanya maziko.
Diwani wa Mashewa, Seif Hillary alisema tukio kama hilo halijawahi kutokea bali tembo hao wanaosadikiwa kutoka hifadhi ya Mkomazi wamekuwa na tabia kuharibu mazao kwenye mashamba ya wananchi wa vijiji hivyo.
Hillary alisema baada ya tukio hilo waliwataarifu askari wa Tanapa ambao walifika mapema kwenye eneo hilo wakifanya taratibu za kuwarejesha Tembo hao walikotoka.
Pamoja na hayo tayari wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari juu ya wanyama hao huku diwani huyo akisema iko haja kwa wanyama hao kuwekewa udhibiti wasiweze kudhuru wananchi.
Mkuu wa askari wa Hifadhi ya Taifa Mkomazi, Laurent Kawau alisema baada ya kupata taarifa kutoka kwa viongozi wa Kata ya Mashewa waliweza kutuma askari na magari katika eneo la tukio
Kawau alisema mpaka sasa wamefanikiwa kuwanasaga Tembo hao kurudi katika hifadhi hiyo ya Mkomazi na wengine wameelekea katika msitu wa Mashewa uliopo mbali na makazi ya wanakijiji.
“Tulituma askari na magari kutoka Hifadhi ya Mkomazi, Tanapa pamoja na magari matatu yapo katika eneo la tukio “
Alisema tembo hawa kwa sasa wanatoka kutokana na utulivu ulipo (wawindaji haramu hawapo) hivyo wanafuata njia zao za zamani kwani tembo hata kama alipita miaka 50 iliyopita lazima kizazi chake pia kipite njia hiyo.
Pia aliwataka wananchi wa maeneo hayo uchukua tahadhari kwa kuacha kutembea usiku sana na asubuhi pamoja na kuacha kupiga kelele wawapo barabarani kwani tembo hao wakisikia kelele huzifuata sauti zilipo.