TFC kusambaza mbolea kwa wakulima 150,000

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Samwel Mshote kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 Serikali imewatengea kiasi cha Sh40 bilioni kwa ajili ya kufanikisha mpango huo na kiasi kingine cha Sh70 bilioni kitatolewa na wadau wa maendeleo (wahisani).

Tabora. Kampuni ya Mbolea nchini (TFC) inatarajia kusambaza zaidi ya tani 75,000 za mbolea ya ruzuku iliyotolewa na Serikali kwa wakulima zaidi ya 150,000.

Hayo yameekezwa Oktoba 13 na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni hiyo, Samwel Mshote alipokuwa akingungumzia maonesho ya siku ya mbolea duniani yanayofanyika katika uwanja wa Chipukizi mjini Tabora.

Amesema kwa mwaka huu wa fedha 2023/2024 Serikali imewatengea kiasi cha Sh40 bilioni kwa ajili ya kufanikisha mpango huo na kiasi kingine cha Sh70 bilioni kitatolewa na wadau wa maendeleo (wahisani).

Amefafanua kuwa tani 25,000 za awali tayari zimenunuliwa na kuanza kusambazwa kwa wakulima na sasa wapo kwenye mchakato wa kununua tani zingine 50,000 ambazo zitasambazwa katika Mikoa yote.

 “Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuiwezesha kampuni ya mbolea kununua na kusambaza mbolea ya ruzuku kwa wakulima nchini,” amesema.

Mshote ameongeza kuwa baada ya kuanza tena shughuli zao mwaka jana 2022/2023; Serikali iliwapatia kiasi cha sh 6 bilioni ambapo walinunua na kusambaza tani 4,500 za mbolea hiyo na hadi sasa wameshahudumia zaidi ya wakulima 30,000 na kufikisha huduma hiyo katika Mikoa 17 ya Tanzania Bara na halmashauri 40.

Ameeleza mikakati yao kuwa ni kununua na kusambaza zaidi ya tani 150,000 kuanzia msimu huu na kufikia wakulima zaidi ya 500,000.

Aidha ameongeza kuwa tayari wamesajili mawakala wa ununuzi na usambazaji mbolea wapatao 300 na kwamba watatumia vyama vikuu vya ushirika na maghala ya Serikali kuuza mbolea hiyo.

Wakati huo huo ongezeko la tani 3 milioni za nafaka mbalimbali limepatikana kutokana matumizi ya mbolea ya ruzuku inayotolewa na Serikali kwa lengo la kuwapunguzia mzigo wakulima nchini.

Mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa mbolea nchini (TFRA), Dk Anthony Diallo akizungumza katika maadhimisho hayo amesema jumla ya tani 10 milioni za nafaka zimepatikana baada ya matumizi ya mbolea ya ruzuku ukilinganisha na tani 7 milioni zilizopatikana kabla ya matumizi ya mbolea ya ruzuku.

Amesema wanataka wakulima watumie mbolea kwa usahihi ili tija iongezeke na wakulima wanufaike na kilimo chao

Sanjari na hilo amesema kuwa watahakikisha wanadhibiti ubora wa mbolea na wakulima wanapata huduma bora katika kilimo chao ili kuongeza tija katika uzalishaji na kuwa na usalama wa chakula nchini.

"Natoa wito kwa wakulima kujitokeza katika maadhimisho haya ili kupata elimu ya aina sahihi ya matumizi ya mbolea," amesema.

Alisema wamejipanga kuhakikisha mkulima haifuati mbolea zaidi ya km 1 na kwa Mkoa wa Tabora kuna vituo 80 kutoka vituo 16 vilivyokuwepo awali.