TGDC kuanza kuzalisha umeme wa Jotoardhi kuukabili mgawo

Muktasari:

  • Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) imeanza utekelezaji wa miradi mitano ya kipaumbele ya rasilimali jotoardhi ambayo itapatikana katika mikoa zaidi ya 16 nchini.

Arusha. Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) imeanza utekelezaji wa miradi mitano ya kipaumbele ya rasilimali jotoardhi ambayo itapatikana katika mikoa zaidi ya 16 nchini.

 Kampuni   hiyo ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) ambapo inatekeleza nishati ya jotoardhi inayochimbwa urefu wa kilometa tatu kwenda chini na ina uwezo wa kuzalisha megawati 5,000 nchini.

Hayo yamesemwa leo Jumatano, Novemba 23, 2022 jijini Arusha na Kaimu Meneja Mkuu wa TGDC, Mhandisi Shakiru Idrissa Kajugus wakati akizungumza katika ziara ya Bodi ya wakurugenzi ya kampuni hiyo ilipotembelea eneo la mradi lililipo Ziwa Natron, wilayani Ngorongoro, Mkoa wa Arusha.

Amesema nishati hiyo ya jotoardhi inapatikana kwa wingi katika maeneo ya bonde la Ufa ambapo kwa upande wa  Ziwa Natron wapo katika hatua za utafiti kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo ambao utazalisha megawati 60 na unatarajiwa kukamilika mwaka 2025.

"Mradi huu wa Ziwa Natron kwa kuanzia tutazalisha megawati 10 baada ya hapo tunaendelea na upanuzi zaidi na unatarajiwa kugharimu zaidi ya  Sh 1 bilioni  na kukamilika kwa mradi huo kutaleta manufaa makubwa sana kwa wananchi kwani ni nishati endelevu ya kisasa isiyotegemea mabadiliko ya tabia ya nchi," amesema Mhandisi Kajugus. 

Amesema Tanzania kwa sasa tunatekeleza miradi mitano ya kipaumbele na  huo ni mmojawapo na  maeneo hayo yapo katika mkoa wa  Mbeya ambapo ipo  miradi miwili katika  wilaya ya   Rungwe katika maeneo ya  Ngozi  na Kiejo - Mbaka  huku mikoa mingine ikiwa  ni Songwe na Pwani na tayari  ipo katika hatua ya uhakiki kwa ajili ya kuchimba visima huku kwa mkoa wa Arusha wakiendelea  na tafiti za kisayansi ambazo zinatarajiwa kumalizika mwaka 2023.

Kwa upande wake, Mwenyekiti  wa bodi ya TGDC, Profesa Shubi Kaijage amesema ikiwa kama bodi mpya wamefikia hatua ya kutembelea  moja ya miradi ya kampuni hiyo kujionea  na kuweza kuangalia cha  kushauri  ili mradi huo uweze  kufanyiwa kazi kwa haraka na kwa weledi.

Amesema nishati hiyo inapatikana chini ya ardhi kwa kutumia joto lililopo  chini ya ardhi na kuwa itaweza kupunguza sana changamoto  ya mgao wa umeme uliopo hivi sasa unaosababishwa na ukame.Kwani nishati hii ni endelevi na haiathiriwi na mabadiliko ya tabia nchi. 

"Sisi kama bodi tunaendelea kuhakikisha tunasimamia kikamilifu mradi huu ili uweze kukamilika kwa wakati na tunaomba kampuni hii iendelee kutekeleza majukumu  yake kwa wakati ili tuendelee kupata vyanzo  zaidi vya umeme,” amesema