THRDC: Watanzania wengi vijijini hawamudu gharama huduma ya kisheria
Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa.
Muktasari:
- Watanzania wengi hasa waishio vijijini wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama za huduma ya sheria, Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umeishauri Serikali kuangalia kuangalia namna ya kuwawezesha wasaidizi wa kisheria.
Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umeishauri Serikali kuangalia namna ya kuwawezesha wasaidizi wa kisheria Ili waweze kuwasaidia watu wasiokuwa na uwezo wa kifedha.
Kutokana na kukosa rasilimali fedha watu wengi hasa wa vijijini wamekuwa wakipoteza haki zao kwa kukosa msaada wa kisheria.
Akizungumza leo Jumatatu Agosti 8, 2023 wakati mafunzo ya msaada wa kisheria uliohusisha mikoa mitatu, Mratibu THRDC, Onesmo Olengurumwa amesema changamoto ni nyingi hasa vijijini kutokana na wasaidizi wa kisheria kukosa fedha.
"Taasisi zinazotoa msaada wakisheria ni chache, bado kunauhotaji mkubwa wa Watetezi licha ya kutokuwa na rasilimali fedha,"amesema Olengurumwa.
Amesema lengo la THRDC ni kuanzisha taasisi nyingi ili kuwa na wawakilishi katika kila kata na ikiwezekana kwenye kila kijiji.
"Taasisi zinazotoa msaada wa kisheria hazizidi 200 lakini watetezi hawazidi hawazidi 5,000 hii ni idadi ndogo sana Watanzania wengi wanakosa haki na kudhulimiwa kwa kukosa msaada wa kisheria," amesema.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam Shule ya Sheria, Dk Veronica Buchumi amesema mafunzo hayo ya siku mbili yatasaidia kuboresha huduma za sheria kwa watetezi wakisheria.
Amesema maeneo mengi bado kuna changamoto kutokana na kutofautiana mila, desturi na itikadi za dini.
"Mafunzo haya yatasaidia kuboresha huduma ambazo Watanzania wanazitaka kwenye masuala ya haki kwa kuwa kuna watu wasiokuwa na uwezo," amesema Dk Buchumi.
Buchumi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Msaada wa Kisheria Watanzania wengi hawana uwezo wa kumudu gharama za kupata huduma za kisheria kutokana na kushindwa kugharamia.