TLS yakwaa kisiki mahakamani kuzuia kesi ya kupinga mkutano wake
Muktasari:
- TLS iliweka pingamizi dhidi ya shauri lililofunguliwa na mwanachama wake, akiiomba mahakama isilisikilize kwa madai kuwa limepitwa na wakati, lakini Mahakama imetupilia mbali pingamizi hilo na imeamuru kuendelea na usikilizwaji wa shauri hilo.
Dar es Salaam. Jitihada za Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) kuzuia usikilizwaji wa shauri la kupinga mkutano wake mkuu wa dharura, lililofunguliwa na mwanachama wake Baltazary Bosco Mahai, zimegonga ukuta baada ya Mahakama Kuu Masjala Kuu Dodoma kutupilia mbali pingamizi lake.
Badala yake mahakama hiyo imeamua utaendelea na usikilizwaji wa shauri hilo.
Wakili Mahai amelieleza Mwananchi leo Jumapili, Juni 16, 2024 kuwa shauri hilo limepangwa kusikilizwa Juni 26, 2024.
Katika shauri hilo la mapitio ya Mahakama namba 7969 la mwaka 2024 Mahai anadai kuwa uamuzi wa Baraza la Uongozi na taarifa ya kuitisha mkutano huo vimegubikwa na kasoro kwa kuwa taratibu hazikuzingatiwa.
Hivyo aliiomba Mahakama itoe amri ya kutengua uamuzi wa Baraza la Uongozi la TLS na taarifa yake ya Desemba Mosi, 2023 ya kuitisha mkutano huo wa dharura kwa madai ni batili kutokana na kutofuata taratibu za kisheria.
Pia aliiomba mahakama iiamuru TLS kuitisha mkutano huo mkuu wa dharura kwa kuzingatia taratibu.
TLS iliweka pingamizi dhidi ya shauri hilo ikiiomba mahakama hiyo ilitupilie mbali bila kuisikiliza ikidai kuwa limeshapitwa na wakati.
Mahakama baada ya kusikiliza hoja za pande zote katika uamuzi wake uliotolewa na Jaji Abdi Kagomba, Juni 13, 2024, imetupilia mbali pingamizi hilo baada ya kukubaliana na hoja za Wakili Mahai na za Serikali.
Kwanza Jaji Kagomba amekubaliana na Wakili wa TLS kuwa amri ya kuilazimisha TLS kuitisha mkutano huo kwa kuzingatia sheria haitakuwa na maana wakati tayari taarifa ya mkutano mkuu wa mwaka wa kawaida imeshatolewa.
Hata hivyo, Jaji Kagomba pia amekubaliana na hoja za Wakili wa Serikali, Webiro na mdai, Wakili Mahai.
Amesema kwa mujibu wa hati ya maombi miongoni mwa hoja zinazohitaji kuamuriwa ni pamoja na nani anapaswa kutoa taarifa kuitisha mkutano, muda wa taarifa na muda wa wanachama kupewa nyaraka za mkutano wakati wa kuitisha mkutano mkuu wa dharura wa TLS.
Amesema ni jambo lisilobishaniwa kuwa hoja hizo zimeibuliwa katika shauri ambalo bado liko mahakamani kwa uamuzi na kwa sababu hiyo ni mtazamo wake kwamba shauri hilo bado halijapitwa na wakati.
"Kwa hiyo pingamizi la awali linatupiliwa mbali. Shauri la maombi ya mapitio ya mahakama litaendelea kusikilizwa katika ustahilifu wake," amesema Jaji Kagomba huku akiiamuru TLS kumlipa wakili Mahai gharama za usikilizwaji wa pingamizi hilo.
Wakili Mahai alifungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Kuu Dar es Salaam, kabla ya Masjala hiyo kuhamishiwa Dodoma baada ya kupata ridhaa ili kupinga mkutano mkuu wa dharura wa TLS.
Mkutano huo uliopangwa kufanyika Desemba 16, 2023, ukiwa na agenda kuu mbili, yaani muundo na mamlaka ya Kamati ya Kitaifa ya Mawakili na Kamati ya Mawakili ya Mikoa ambapo matokeo ya marekebisho ya Sheria ya TLS yaliyopitishwa Novemba mwaka 2023.
Hata hivyo, Desemba 15, siku moja kabla Mahai alifungua shauri la maombi dhidi ya TLS na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba ridhaa ya kufungua shauri la mapitio ya mahakama kupinga mkutano huo.
Pia alifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda la mkutano, chini ya hati ya dharura ili kusubiri usikilizwaji wa shauri la maombi ya ridhaa ya kufungua shauri la mapitio ya Mahakama kupinga mkutano huo.
Siku hiyohiyo, Desemba 15 Mahakama ilisikilizwa upande mmoja shauri hilo la maombi ya zuio la muda na ikatoa amri ya zuio la mkutano huo, kusubiri usikilizwaji wa shauri la maombi ya ridhaa ya kufungua shauri la mapitio ya mahakama.
Hata hivyo, baada ya Mahai kupata ridhaa na kufungua shauri rasmi la kupinga kutano huo, TLS iliibua pingamizi la kisheria.
Siku ya usikilizwaji wa pingamizi hilo, Wakili wa TLS, Josephine Mzava aliieleza Mahakama shauri hilo limeshapitwa na wakati kwa kuwa linakusudia kupinga mkutano Mkuu wa dharura uliokuwa imepangwa kufanyika Desemba 16, 2023.
Alidai kwa sasa hitaji la kuitisha mkutano mkuu wa dharura halipo kwa kuwa tayari tarehe ya mkutano mkuu wa kawaida imeshatangazwa, Agosti 31, 2024. Hivyo aliiomba Mahakama hiyo ilitupilie mbali shauri hilo bila kulisikiliza.
Wakili wa Serikali, Edwin Webiro kwa niaba ya AG, alipinga hoja ya pingamizi la TLS akidai shauri hilo halina lengo la kuzuia kufanyika kwa mkutano mkuu wa dharura wa Desemba 16, 2023.
Badala yake alidai linaomba amri ya Mahakama kutengua uamuzi na taarifa ya TLS ya Desemba Mosi, 2023 kuitisha mkutano huo wa dharura kwa kuwa ni batili kwa kutofuata sheria.
Alidai shauri lililoko mahakamani linahitaji kuamuriwa iwapo TLS inafungwa na sheria kutoa taarifa ya siku 21 kwa wanachama wake inapotaka kuitisha mkutano mkuu wa dharura.
Wakili Webiro aliongeza kuwa pia shauri hilo linahitaji kuamuriwa kuhusu takwa la kuwapatia wanachama nyaraka za mkutano ndani ya siku 14 na kama taarifa ya kuitisha mkutano wowote wa TLS inatolewa na sekretarieti au rais.
Hivyo aliiomba Mahakama hiyo iitupilie mbali pingamizi hilo na ipange tarehe ya usikilizwaji wa shauri hilo.
Kwa upande wake Mahai aliunga mkono hoja zilizotolewa na Wakili Webiro naye akaiomba Mahakama iitupilie mbali pingamizi hilo na TLS imlipe gharama za usikilizwaji wake.