TMA yatabiri El Nino hadi Aprili, mafuriko yaendelea kutesa Morogoro
Muktasari:
- Mara kadhaa tangu mwishoni mwa mwaka jana, TMA imekuwa ikitoa angalizo la hali mbaya ya hewa hadi juzi ilipotangaza uwepo wa hali hiyo kwa siku tano kuanzia jana kwenye mikoa ya Morogoro, Lindi, Iringa, Mtwara, Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma.
Dar/Moro. Wakati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), ikibainisha kuwepo viashiria vya El Nino hadi Aprili mwaka huu, wakulima wameshauriwa kupanda mazao ya muda mfupi yanayohimili wingi wa mvua katika kipindi hiki.
Hata hivyo, maeneo mengi nchini yameendelea kupata mvua ambazo TMA imeeleza ni za nje ya msimu wa vuli, zilizotarajiwa kuanza Oktoba hadi Desemba mwaka jana, huku maeneo yanayopata mvua za masika zikitarajiwa kuanza Machi hadi Mei.
Wakati utabiri wa TMA ukieleza hayo, leo Jumanne Januari 30, 2024 mjini Morogoro, askari wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji, jana walilazimika kuwavusha kwa kamba wananchi wanaotumia Barabara ya Mazimbu iliyopo Kata ya Kihonda na Lukobe baada ya barabara hiyo kujaa maji eneo la 'Kwa bwanajelaMara kadhaa tangu mwishoni mwa mwaka jana,
TMA imekuwa ikitoa angalizo la hali mbaya ya hewa hadi juzi ilipotangaza uwepo wa hali hiyo kwa siku tano kuanzia jana kwenye mikoa ya Morogoro, Lindi, Iringa, Mtwara, Mbeya, Songwe, Njombe na Ruvuma.
Baadhi ya mikoa ikiwamo Dar es Salaam, Morogoro na Pwani imeendelea kupata mvua kubwa zinazoathiri miundombinu na kwenye baadhi ya mikoa kusababisha vifo na mafuriko.
Mvua za kipindi hiki zinatajwa kuchangia kuwapo kwa unyevyunyevu kutoka magharibi ya misitu ya Congo na unaelezwa kusababisha uwepo wa viashiria vya El Nino itakayoendelea hadi Aprili.Meneja wa Utabiri wa TMA, Dk Mafuru Kantamla amesema viashiria vya El Nino bado vipo ingawa nguvu yake sio kubwa kama ilivyokuwa awali.
“Mwanzo ilionyesha El Nino itakwenda hadi Desemba 2023 au Januari 2024, lakini bado ipo hadi Aprili,” amesema Dk Kantamla alipokuwa akifafanua juu ya wingi wa mvua katika maeneo mbalimbali nchini,
Amefafanua kuwa hali hiyo huwa inasababishwa na migandamizo midogo ya hewa iliyoko Mashariki mwa Kisiwa cha Madagascar.
“Hii migandamizo imekuwa na mchango mkubwa kwenye kuvuta upepo wenye unyevunyevu kutoka Magharibi ya misitu ya Congo kuja maeneo mengi ya nchi.
“Kuwepo kwa migandamizo hii kwa takribani wiki tatu na kuimarika kwa ukanda mvua kumesababisha uwepo wa hizi mvua.“Ingawa inaonyesha Februari Mosi na 2 hii migandamizo itakwenda Kusini mwa ncha ya Bara la Afrika, hivyo hata hizi mvua zitaanza kupungua,” amesema.
Mvua hizo zimeendelea kuleta madhara mkoani Morogoro, ikiwamo ile iliyonyesha jana na kusababisha wananchi kushindwa kwenda kwenye shughuli zao wakiwamo wanafunzi kutokwenda shule.
Huo ni mwendelezo wa ile ya Januari 5, mwaka huu iliyosababisha mafuriko mkoani humo na baadhi ya barabarakukatika na kushindwa kupitika.
Mmoja wa wananchi aliyelazimika kuvushwa kwa kamba, Shani Ally amesema pamoja na eneo hilo kuwa korofi nyakati za mvua, lakini za mwaka huu hali ni mbaya zaidi.Diwani wa Lukobe, Selestine Mbilinyi amesema mvua hizo zimeleta madhara makubwa kuliko za miaka ya nyuma.
"Watu wamepoteza maisha, makazi, mali na hata miundombinu nayo imeharibika kwa kiasi kikubwa,” amesema na kuwataka wananchi kuwa wavumilivu huku akiwasisitiza kuchukua tahadhari, ili kuepuka madhara yanayoweza kutokea.
Maeneo mengine yaliyoathirika na mvua hiyo katika Manispaa ya Morogoro ni pamoja na Mkundi, Lugala, Kasanga, Bigwa, Mafisa na Mwembesongo.Mkoani Njombe, wakulima wamesema mazao kama nyanya zinaoza kutokana na mvua nyingi kupita kiasi na maeneo mengine mashamba yamejaa maji na baadhi mazao yamesombwa na maji.
Hata hivyo, Dk Kantamla amesema maeneo ambayo mvua inanyesha kwa wingi, unyevunyevu wa udongo nao ni mwingi na ukipitiliza unaweza kuathiri mazao ambayo hayaendani na maji mengi.“Ni vema wakulima wachukue ushauri kutoka kwa maofisa ugani hasa katika kipindi hiki,” amesema.
Mwananchi Digitali imezungumza na Ofisa ugani wa eneo la Lupembe Mkoani Njombe, Ibrahim Mhessi ambaye amesema kwa eneo lao, wamewashauri wakulima kupanda mihogo, parachichi na aina mbalimbali za mbogamboga.
“Kuna uwezekano wa kutokuwa na mavuno mazuri ya mahindi, ili kujihami na hali hii tumewashauri wakulima katika kipindi hiki wapande mbegu za muda mfupi yaani za siku 75,” amesema.
Ametaja mazao mengine waliyoshauri yapandwe ni pamoja na muhogo ambao hustahimili pia maji mengi.Mhessi amesema kwa mazao ya muda mrefu, kwa ajili ya biashara, wakulima wameshauriwa kupanda parachichi na miti ya aina zote, lakini pia kuhifadhi chakula.
Mkulima, Everenansio Msambwa amesema changamoto ya kilimo kwa nyakati hizi ni nyingi ikiwamo ya mazao mengi kusombwa na maji na mengine maji yanapojaa yanashindwa kustahimili na hatimaye hudumaa.“
Kuna mashamba rutuba yake nyingi inasombwa na maji hasa yaliyoko kwenye maeneo ya miinuko, hii inaathiri sana mimea kwa sababu inakosa virutubisho,” amesema Msambwa.
Mkulima huyo amesema tayari maofisa ugani wamewashauri wakulima kuweka makinga maji mengi kwenye mashamba yao hasa yaliyopo kwenye miinuko ili kuzuia rutuba isisombwe na maji.