TMDA yasema kuna hatari ya ugumba kuongezeka

Muktasari:

  • Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Magharibi, imesema ipo hatari ya kuwepo ongezeko la wagumba nchini kutokana na vijana wengi kutumia dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo hazijasajiliwa, huku wasichana wakitumia dawa za P2 bila kupata ushauri wa kitaalamu.

Geita. Asilimia 30 ya maduka ya dawa za binadamu Kanda ya Ziwa Magharibi yanadaiwa kuuza dawa za kuongeza nguvu za kiume ambazo hazijasajiliwa pamoja na dawa za kuharibu vichocheo (hormones) kwa wasichana ili mimba isitungwe maarufu P2, jambo linalotajwa kuhatarisha afya ya uzazi.

Meneja wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) kanda ya Ziwa Mangaribi Geita inayosimamia mikoa ya Geita, Shinyanga na Kagera, Dk Edgar Mahundi amesema ipo hatari ya kuwa na Taifa la vijana wanaoshindwa kuzaliana kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya dawa wanazotumia bila kupata ushauri wa mtaalamu wa afya.

“Umekua mtindo kwa baadhi ya vijana kutumia dawa bila kufuata masharti au utaalamu wa afya ili kuongeza nguvu za kiume.

“Tumezikamata kwenye maduka binafsi ya dawa zinaitwa VEGA 100 dawa hizi hazijasajiliwa lakini tulipofuatilia kiwanda kilichoandikwa hakipo duniani na kwa maana hiyo ni dawa bandia,” amesema.

Akifafanua kuhusu dawa hizo, Dk Mahundi amesema kuwa zinaweza zisiwe na kiambata kinachowezesha dawa ifanye au inaweza kuwekwa kemikali nyingine ambazo ni hatarishi zaidi kwa afya ya mhusika.

“Tumekuta hazijafungashwa kwenye vifungashio vinavyokubalika na zinauzwa na watu ambao hawana taaluma ya mambo ya dawa zinauzwa kiholela zinatumiwa na vijana wanadai zinawasaidia lakini ni hatari kwao,” amesema.

Akizungumzia dawa za P2 amesema dawa hizo zinauzwa kiholela na kwenye maduka bubu na zinatumika kuharibu vichocheo ili mimba isitungwe na ipo hatari kwa wasichana wanaotumia dawa hizo kukosa watoto miaka ijayo na kuongeza wagumba nchini.

Aidha, amesema zipo dawa zinazouzwa kwenye maduka binafsi za dawa zinauzwa zikiwa kwenye makopo na hazijasajiliwa na kwamba TMDA ilishatoa muongozo kuwa dawa zilizopo kwenye makopo hazipaswi kuuzwa kwenye maduka binafsi.

“Dawa za vifungashio vilivyoko kwenye makopo zinatakiwa kukutwa kwenye hospitali kubwa na zinatakiwa zisambazwe na MSD kwenye ukaguzi wetu tumezikuta madukani niwaombe wananchi wanapozikuta wasizinunue hizi tumezifuatilia hazijasajiliwa na ni dawa bandia,” amesema.

Ili kuondoka na changamoto za madhara ya kiafya kwa kutumia dawa bandia, ameishauri jamii kwenda kwenye vituo vya afya na kupata dawa sahihi au kuwasiliana na mtaalamu wa afya kabla ya kununua dawa kwenye maduka binafsi ya dawa.