TRA yawatala wafanyabiashara kutunza kumbukumbu za kodi

Tuesday August 31 2021
TRA pc
By Florah Temba
By Janeth Joseph

Moshi. Mamlaka ya mapato nchini (TRA) Mkoa wa Kilimanjaro, imewataka wafanyabiashara mkoani humo, kuwa wazalendo na kuhakikisha wanajenga utamaduni wa kutunza kumbukumbu ili kulipa kodi sahihi na kwa hiari.


Rai hiyo imetolewa mjini Moshi na Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Massawa Masatu wakati akizungumza kwenye kikao cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na wafanyabiashara, kilichokuwa na lengo la kusikiliza kero na kutoa ufafanuzi wa maboresho ya sheria za kodi kama zilivyopitishwa na bunge.


Amesema ili wafanyabiashara waweze kuwa na taarifa sahihi ni lazima watunze kumbukumbu za biashara zao na kuhakikisha wanakuwa wawazi na wanafuata sheria.


"Serikali inahimiza sana watu kulipa kodi kwa hiari, niwaombe wafanyabiashara wa mkoa huu kuzingatia hili ndio maana sisi kama watumishi tuko kwa ajili ya kuwahudumia na kusikiliza kero zinazowakabili kwenye biashara zenu na kuwatafutia ufumbuzi," amesema Masatu.


Akitoa ufafanuzi wa sheria zilizofanyiwa maboresho, Lazaro Mafie kutoka TRA makao makuu, amewataka wenye nyumba ambao wana Luku zaidi ya moja kwenye nyumba moja kuandika barua TRA na kuainisha namba ya mita hiyo atahitaji ikatwe kodi hiyo.


Mmoja wa wafanyabiashara waliohudhuria kikao hicho, Hadija Said amesema ipo haja ya serikali kuangalia namna ya kupunguza mlundikano wa kodi kwani mara nyingi wamekuwa wakifanyabiashara bila kuona faida za biashara zao.

Advertisement
Advertisement