TRA yaweka mkakati kurahisisha ulipaji kodi nchini

Naibu Kamishna wa idara ya kodi za ndani, Swalehe Byarugabe akizungumza na waandishi wa habari katika kikao hicho.
Muktasari:
- Mamlaka ya mapato nchini (TRA) imeweka mikakati katika ulipaji kodi kwa kwa kusikiliza malalamiko ya walipa kodi.
Arusha. Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) imeendelea kuweka mikakati na miundombinu ya ulipaji kodi kwa wateja wake ili kuwarahisisha wafanyabiashara wa Tanzania Bara na Visiwani.
Akizungumza leo Oktoba 20 mwaka huu, katika kikao cha wadau wa sekta ya utalii jijini Arusha, Naibu kamishna wa Idara ya Kodi za Ndani, Swalehe Byarugabe amesema mkakati wao ni kuwasikiliza wadau ili kuweka mikakati ya ukusanyaji wa kodi.
"Hapa tupo katika mwendelezo wa kukutana na makundi ya walipa kodi lango likiwa ni kusikiliza changamoto wanazokumbananazo zikiwemo za kibiashara pamoja na kikodi," amesema Byarugabe.
Naibu huyo amesema wamekuwa na taratibu za kusikiliza changamoto kwa makundi kwani kwa kufanya hivyo hali ya mapato nchini inazidi kuongezeka kwani hali hiyo ni matunda yatokanayo na ushirikiano baina ya TRA na wateja wake kutoka sekta mbalimbali.
Kwa upande wake Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar, Yusuph Mwenda amesema ushirikiano walionao ni moja ya kurahisisha ukusanyaji wa kodi kwa wateja wake ambapo sekta ya utalii kwa upande wa Zanzibar ndio unaoendesha uchumi kwa zaidi ya asilimia 40.
"Leo tumekutana jijini Arusha kuwasikiliza changamoto za wadau wa sekta ya utalii ambapo tutapata fursa ya kuwaeleza njia nzuri ya kurahisisha kufanya shughuli zao za utalii nchini kote bila usumbufu kwa pamoja na wageni wanaofika nchini," amesema.
Nao baadhi ya wadau wa sekta ya utalii walisema mahali wanapoomba wafanyiwe marekebisho ni pamoja na mfumo wa ulipaji kodi pamoja na baadhi ya sera ambazo zimekuwa changamoto katika shughuli zao za utalii hiyo kupitia kikao hicho wataweza kuwaonyesha taswira kamili.