Treni SGR bado, wadau washauri PPP

Dar es Salaam. Wakati danadana zikiendelea katika mradi wa reli ya kisasa (SGR), Serikali imeshauriwa kuangalia namna ya kutekeleza mradi huo kwa ubia kati ya Sekta Binafsi na Serikali (PPP).

Ushauri huo umetolewa kipindi ambacho ahadi ya Serikali kupitia kwa Shirika la Reli Tanzania (TRC) kuwa reli hiyo ingeanza mwezi uliopita ikikwama, licha ya ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam hadi Morogoro kukamilika.

Jana, Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa akizungumza na gazeti hili alisema kilichosababisha kuahirishwa kwa safari hizo ni vichwa vya treni ambavyo bado havijafika, huku akieleza kwa mujibu wa mkataba walipaswa walete wakati huo (uliokuwa umeahidiwa).

“Kutokana na changamoto zilizo nje ya uwezo wao, wamechelewa, mabehewa yanaendelea kuingia mengine tutapokea wiki hii au ijayo. Na kichwa cha kwanza tunatengemea kitaingia mwishoni mwa mwezi ujao,” alisema Kadogosa, alipokuwa akizungumza na mwandishi kwa simu.

Alisema mabehewa sita ya ghorofa moja yanatarajiwa kuwasili nchini wiki ijayo na yatakuwa na uwezo wa kuchukua watu 150 waliokaa.

Kadogosa alisema vifaa hivyo vinachelewa kuwasili kwa kuwa utengenezaji wake haufanywi na kiwanda kimoja, baadhi ya vitu vinatoka nchi tofauti, hivyo mnyororo wa usafirishaji kutoka nchi hizo umekuwa na changamoto kwa sababu nyingine zimekumbwa na mitikisiko ya kiuchumi na kijamii.

“Njia yetu mpaka sasa inapitika kutoka Dar es Salaam mpaka Dodoma kwa SGR, treni ya umeme inafika Morogoro bila tatizo, upande wa Morogoro mpaka Dodoma, miundombinu ya umeme ipo asilimia 99,” alisema Kadogosa.

Alisema mara baada ya kuwasili kwa vifaa vinavyosubiriwa itakuwa ni mwanzo wa safari hizo, kwani madaraja yanayoendelea kujengwa, ikiwemo la Vigunguti, daraja la Nyerere na daraja la Banana yako zaidi ya asilimia 95 na hivi karibuni yanakamilika,” alisema.

Februari 14, mwaka huu akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari, Kadogosa alisema ujenzi katika kipande hicho umefikia asilimia 97.91, kazi iliyokuwa imebaki ni ujenzi wa madaraja yanayokatiza kwenye reli yameongezeka tofauti na makadirio ya awali.

Alisema awali hawakuwa wameweka mpango wa njia za kupita wanyama katika maeneo ambayo reli imekatiza kwenye hifadhi, lakini sasa imeonekana umuhimu wa kujenga njia hizo.

Sababu nyingine ya kusogezwa mbele kwa safari hizo ni kuchelewa kuwasili vichwa vya treni, jambo ambalo liko nje ya uwezo wa shirika hilo.

Akizungumza namna danadana hizo zinavyoweza kumalizwa, mmoja wa vigogo ndani ya Serikali aliyeomba hifadhi ya jina lake alisema, Serikali kama inahitaji kuufanya mradi wa SGR kuwa wa kisasa zaidi ni muhimu itumie PPP, kwa maana yenyewe iishie kujenga tu, jukumu la uendeshaji lipelekwe kwa mwekezaji.

Alisema manufaa ya hilo ni ufanisi wa huduma, kampuni italipa kodi kuliko TRC, itapunguza mzigo kwenye bajeti ya Serikali kununua vichwa na mabehewa na gharama za uendeshaji.

“Hii itasaidia kuifanya huduma kuwa bora, Serikali itajiondoa kwenye gharama za uendeshaji kama kununua mabehewa, vichwa pamoja na kuwagharimia wafanyakazi, yote haya yatafanywa na mwekezaji.

“Italeta ubunifu zaidi, ikiwemo kuongeza mzigo kwa kuhakikisha wafanyabiashara zaidi wanaitumia," alisema.

Kigogo huyo anayefanya kazi Wizara ya Fedha na Mipango alisema: “Hata sijui mikataba mibovu ya ununuzi wa mabehewa haitakuwepo, tutapata huduma nzuri sana na Serikali itabaki kuchukua kodi kulingana na mkataba wake na mwekezaji.

“Yaani ninachokisema ni kama mradi wa mabasi ya mwendokasi, Serikali imejenga miundombinu, halafu uendeshaji amepewa mwekezaji, ndicho kinapaswa kufanyika kwenye SGR na hiki kitaondoa kuahirisha mara kwa mara kuanza kutoa huduma. Katika dunia ya sasa PPP haiepukiki”.


Wachumi na PPP

Hoja ya PPP ilielezwa pia na Profesa wa uchumi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Jehovaness Aikaeli ambaye alibainisha njia sahihi ya kuendesha mradi wa SGR ni kuhusisha sekta binafsi kwa kuingia ubia au kuingia makubaliano kwa kuweka kiasi cha mapato yanayopaswa kuingia serikalini.

Alisema Serikali haina sababu ya kutumia fedha katika kununua mabehewa na vichwa vya treni kwa kuwa jukumu hilo lingefanywa na wafanyabiashara ambao pia wangewajibika kuvitunza.

“Unapokuwa na kitu cha kibiashara ni vizuri kikaendeshwa na wafanyabiashara na hapa tunazungumzia sekta binafsi, Serikali ifanye vile vitu ambavyo haviwezi kufanywa na sekta binafsi, mfano ujenzi wa miundombinu ya reli unagharimu fedha nyingi, mfanyabiashara hawezi kujenga.

Hata hivyo, mchumi huyo alitahadharisha ubia huo unapaswa kuingiwa kwa umakini mkubwa na makubaliano yaainishe Serikali itakavyopata mapato.

“Ni lazima kuwe na usimamizi mzuri wa mapato, kila fedha inayoingia ionekane na ijulikane wazi Serikali inapata kiasi gani.

Njia nyingine inaweza kuwa makubaliano ya kukodisha kwa kipindi fulani kama ilivyo nyumba au fremu ya biashara kwamba kila mwezi unatakiwa kulipa kiasi gani ili hata kama hawa wafanyabiashara wakiingia ijulikane wazi kila mwezi Serikali inachukua mapato yake yanayoendana na thamani ya uwekezaji uliofanyika,” alisema Profesa Aikaeli

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), Dk Donald Mmari alisema endapo PPP itatumika kuendesha mradi huo ni vyema mkataba wake uwe madhubuti kuonyesha jukumu la kila upande.

“Kufanya kwa PPP ni jambo linalowezekana na ndilo haswa linalotakiwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa kama hii ya kibiashara. Kinachotakiwa hapa ni mkataba madhubuti utakaoonyesha majukumu ya kila upande. Udhibiti wa mapato ni kitu kinachopaswa kupewa kipaumbele.”

Naye Oscar Mkude alisema ni muhimu kwa sheria ya PPP kuwekwa katika mtazamo unaoonyesha ubia huo utakuwa na manufaa kwa pande zote mbili.