Tucta yamwomba Rais Samia kuondoa kodi za likizo, ‘over time’
Muktasari:
Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limeiomba Serikali isaidie kupunguza na kuondoa kabisa kodi maeneo ya marupurupu ikiwemo nauli za likizo, ‘over time’ na maeneo mengine ili kuleta ahueni ya maisha kwa wafanyakazi nchini, huku wakiomba nyongeza zaidi ya mishahara.
Dar es Salaam. Pamoja na maombi mengine, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) limeiomba Serikali isaidie kupunguza na kuondoa kabisa kodi maeneo ya marupurupu ikiwemo nauli za likizo, ‘overtime’ ili kuleta ahueni ya maisha kwa wafanyakazi nchini.
Pia Tucta imeomba Serikali ishughulikie suala la bima za afya ambapo wapo wafanyakazi ambao malipo yao hayapelekwi katika mfuko na hivyo baadhi yao wanashindwa kupokea matibabu.
Hayo yamesemwa leo Jumatatu, Mei Mosi, 2023 na Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta), Henry Mkunda wakati akisoma risala yake mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi kitaifa (Mei Mosi) ambayo kitaifa yanafanyika mjini Morogoro.
“Juhudi zako tumeziona, tunaomba utusaidie kupunguza au kuondoa kabisa kodi maeneo tunayokatwa hasa kwenye marupurupu ya nauli za likizo, ‘ovetime’ na maeneo mengine,” amesema Mkunda.
Kwa mujibu wa tovuti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mtanzania anayepokea mshahara chini ya Sh270,000 hakatwi kodi lakini anayepokea kuanzia Sh270,000 hadi Sh520,000, anakatwa kodi ya asilimia 8 ya kiasi kinachoongezeka baada ya Sh270,000.
Wakati akitoa hotuba hiyo, Mkunda amemuomba Rais kuwasaidia wale waliopata shida ya vyeti, “Ulikubali na kuwapatia asilimia 5 ya michango yao kwenye mifuko si rahisi, lakini wapo wengi ambao bado hawajapata inawezekana waajiri wao walikuwa hawajalipa yale malipo, tunaomba wafanyakazi hao walipwe na mwajiri apeleke kama itapendeza waangalie kwa jicho la upendo.”
Mkunda ameomba Rais aingilie kati suala la bima ya afya, “Tunashkuru tunapata huduma za afya kupitia bima ya afya kwa wote, wafanyakazi walikuwa wanakatwa asilimia 3 ya michango yao lakini mwajiri hajapeleka. Wanapata adhabu ambapo si kosa lao, tunaomba mfanyakazi asiadhibiwe kwa kosa ambalo hajalitenda,” amesema.
Nyongeza mishahara
Mkunda amesema Tucta inatambua kazi nzuri ya kuwaongezea mishahara asilimia 23.3 ambayo hata hivyo amesema iliwagusa wa kima cha chini cha mishahara ya Serikali na wale wa madaraja ya juu waliguswa kwa kiwango kidogo.
“Tunaendelea kubisha hodi kwako na uendelee kutufikiria, tunatambua kazi kubwa uliyofanya kutuongezea posho na marupurupu hiyo yote inazidi kutuongezea kipato sisi wafanyakazi ili kuweza kupata ajira za staha katika sehemu zetu za kazi,” amesema Mkunda.
Pia amemuomba Rais Samia kuwaangalia wafanyakazi ambao waliondolewa kwenye mfumo wa mishahara wa Serikali wakati wa ukaguzi na baadaye wakarudishwa lakini hawajalipwa mishahara yao licha ya kwamba walikuwa wakiendelea na kazi.
“Kuna hili deni lilitengenezwa wakati huo, tuna wafanyakazi wengi kutoka Mwanza, Nyakahanga, Isaka, Biharamulo, Ilula na kwingine ambao wana madeni ya malimbikizo ya mishahara tunaomba hawa waangaliwe ili wafurahie mazingira yao ya kazi,” amesema.