Tucta yasubiri nyongeza ya mshahara Mei Mosi

Raisi wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Tumaini Nyamhokya akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Dunia (Mei Mosi) yatakayofanyika kitaifa jijini Arusha. Picha na bartha Ismail

Muktasari:

Matarajio ya Tucta yanakuja, baada ya Rais Samia kukubali kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kitaifa, inayotarajia kufanyika Arusha Mei 1, 2024 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Arusha. Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limeeleza matarajio yake ya kuwepo kwa ongezeko la mishahara kwa wafanyakazi nchini kutokana na kupanda kwa gharama za maisha.

Matarajio hayo yamekuja, baada ya Rais Samia kukubali kuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya wafanyakazi kitaifa, yanayotarajia kufanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Mei 1, 2024.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Aprili 17, 2024, Rais wa Tucta, Tumaini Nyamhokya amesema kutokana na vikao mbalimbali walivyofanya na Serikali, wamepitisha kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu kuwa ‘Nyongeza ya mishahara ni msingi wa mafao bora na kinga dhidi ya hali ngumu ya maisha.’

Nyamhokya amesema maandalizi yote kuelekea sherehe hizo yamekamilika na maboresho makubwa yanaendelea  katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

 “Serikali ndio mwajiri namba moja, ndio maana tuna matarajio makubwa kwa Rais kutoa neno jingine la kuleta ahueni ya maisha kwa wafanyakazi katika maadhimisho ya mwaka huu,” amesema Nyamokya.

Amesema wanayo matarajio makubwa ya kupandishiwa kiwango cha mishahara kwa ajili ya kuboresha maisha ya wafanyakazi nchini kukabiliana na kupanda kwa gharama za maisha na kipato kisichokidhi mahitaji ya kila siku ya mfanyakazi.

 “Lakini pia sisi kama watetezi wa masilahi ya wafanyakazi ni jukumu letu kuikumbusha Serikali na waajiri wetu juu ya mambo haya, kuwa mishahara ikiwa bora itawezesha mafao kuwa bora tukiwa kazini na wakati wa kustaafu,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo, kuwataka wafanyakazi wote walioko Mkoa wa Arusha na mikoa ya jirani kuhudhuria sherehe hizo kwa wingi ili kuonyesha umoja wao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia na Utafiti (RAAWU), Jane Mihanji amesema maadhimisho hayo mbali na kutetea masilahi ya wafanyakazi, pia wanalenga kuwahimiza wanachama wao kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi ili kuleta tija iliyokusudiwa.

 “Tunapodai masilahi mazuri, lazima tuonyeshe kwa nini tunadai na njia ni moja tu, kutekeleza wajibu wetu kwa kuchapa kazi kwa bidii na ufanisi mkubwa, ndio maana lazima tukutane kwa pamoja tukumbushane hayo,” amesema.

Amesema chimbuko la maadhimisho hayo ni kukumbuka madhila ya wafanyakazi waliyoyapata miaka ya zamani wakati wa mapinduzi ya viwanda wakitegemea haki zao, ambapo baadhi yao waliuawa na wengine wakateseka.

“Dunia ya leo mateso ya aina ile yako machache lakini bado kuna baadhi ya wenzetu wanapata shida, hivyo tunapoadhimisha siku hii ni kupinga mambo haya,” amesema Mihanji.