Tume huru itakuwa huru?

Muktasari:

  • Wakati Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya 2024 ikianza kutumika, wadau wameikosoa wakisema imejaa utata.

Dar es Salaam. Wakati Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya 2024 ikianza kutumika, wadau wameikosoa wakisema imejaa utata.

Miongoni mwa walioikosoa sheria hiyo ni Tundu Lissu, mwanasheria na makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye ametaja maeneo matano aliyosema yanaonyesha tume hiyo haiko huru, bali ni ya Rais.

Hata hivyo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi ameitetea sheria hiyo, akisema itaifanya tume kuwa huru kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 74(7).

Mambo matano

Akizungumza leo Ijumaa Apeili 12, 2024 na Radio Clouds FM, Lissu amesema taarifa za watazamaji wa uchaguzi wa kitaifa na kimataifa tangu mwaka 1995 zimekuwa zikionyesha kuwa tume hiyo haiko huru, kwa kuwa wajumbe wote ni wateule wa Rais.

“Kwa maana kwamba wajumbe wake wote ni wateule wa Rais, mtendaji mkuu ni mteule wa Rais, watumishi wake wote ni wa Serikali na kwa Katiba yetu, watumishi ni wateule wa Rais au wanafanya kazi kwa niaba ya Rais na yeye ndiye mamlaka yao ya nidhamu,” amesema.

Amesema suala hilo lilibainishwa pia katika ripoti ya Tume ya Jaji Joseph Warioba.

“Kuna juzuu nzima ya Tume ya Warioba kuhusu suala la uchaguzi kwenye nchi yetu na iliangalia hilo suala kwa kina sana. Ilisema hii tume si huru kwa sababu ni ya Rais kwa kuwa viongozi wote ni watu wa Rais,” amesema.

Kuhusu ulinzi wa utumishi wa tume, mwanasiasa huyo alisema tume hiyo haina ulinzi kwa kuwa inaweza kuvunjwa wakati wowote na Rais.

“Kwa Katiba ya nchi ya sasa, wote wanaweza kuondolewa na Rais, maana ndiye anayewapa na ndiye anayewanyang’anya na ni uamuzi wake mwenyewe. Kwa hiyo tume haiko huru, haina security of tenure (uhakika kazini).”

Alisema pamoja na majukumu mengine, Tume hiyo inawajibika kutenga majimbo ya uchaguzi, lakini lazima ipate ridhaa ya Rais, maana yake mkuu wa nchi asipotoa ridhaa, hawatengenezi majimbo.

“Chaguzi huwa zinaanza kushinda au ushindwa kwenye utengenezaji wa majimbo. Kuna uchafu mwingi ya uchaguzi katika nchi yetu na haya ni maneno ya watazamaji wa uchaguzi wetu tangu mwaka 1995,” amesema.

Lissu pia amesema wajumbe na watumishi wa Tume, mamlaka yao ya nidhamu yako kwa Rais, hivyo “kwa ufupi wajumbe wa tume wote na watumishi wake wote kuanzia msimamizi wa kituo mpaka mwenyekiti wa tume, mamlaka ya nidhamu ni rais na wanaotangaza matokeo kwenye majimbo wanateuliwa na Rais.

“Kwa hiyo kwenye uwajibikaji hii si tume huru, ni ya Rais,” amesema.

Hata kwenye masuala ya fedha, Lissu alisema Tume haitakuwa huku kwa kuwa haina bajeti yake, inatakiwa kuwa na bajeti yake ambayo ikipitisha inakuwa na mamlaka kamili na ya kipekee ya kupokea fedha.

“Tume haiendi kupanga foleni kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu au Tamisemi kupata mgawo wa kuendesha uchaguzi au kuandikisha wapiga kura. Inatakiwa kupata bajeti zake bila kuingiliwa katika kutumia fedha zake,” amesema.

Ili tume hiyo iwe huru, Lissu alishauri mamlaka yake ya uteuzi isiwe na masilahi na matokeo ya huo uteuzi.

Alitoa mfano wa Kenya, akisema watu wanaoingia kwenye kamati ya usaili, majaji, wajumbe wa tume au taasisi huru, hao watu Rais hawezi kuwaondoa kazini.

“Hiyo inayoitwa kamati ya usaili, inatakiwa iwe huru na inakuwa hivyo kwa kutowajibika kwa huyo inayemshauri.

“Hiyo kamati ya usaili inapitisha usaili, inafanya maombi, inapendekeza majina, hayo majina yanapelekwa bungeni, yanajadiliwa na Bunge, yakipitishwa anapelekewa Rais kutia baraka tu, hawezi kukataa,” amesema.

Lissu, akizungumza kwa simu na Mwananchi juzi, alisema hata jina la tume hiyo linakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 74(1).

“Hili jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi lilianza kutumika mwaka 1992, tangu mwaka 1961 ilikuwa ikiitwa Tume ya Uchaguzi kwa mujibu wa Katiba, sasa jina la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ni mbwembwe tu,” amesema.


Ni tume huru

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi amesema malalamiko ya vyama vya upinzani kuhusu uhuru wa tume yalianza tangu kwenye mikutano ya kukusanya maoni na walianza kulalamikia jina la tume.

“Ibara ya 74(1) imetaja kuwepo kwa Tume ya Uchaguzi na ndiyo ilikuwa hoja ya upinzani, kwamba hapana tunahitaji tume huru ya uchaguzi. Ukisoma ibara hiyohiyo ya 74(7) inasema tume ya uchaguzi itakuwa huru, inayojitegemea. Hawakupenda, wakawa wanasisitiza kwamba hii Tume jina lake liwe huru.

“Kwa sababu Katiba inasema kutakuwa na tume ya uchaguzi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini kama majukumu yake yametajwa na ibara ya 74(7) kwamba itakuwa huru, hamwoni kwamba hiyo ibara ina cure every anomalous (inaondoa kisicho cha kawaida)?” amehoji.

Kuhusu jina la tume, ametoa mifano ya Tume ya Utumishi wa Mahakama (ibara za 112) na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora (Ibara ya 126), akisema Katiba imekwenda mbali na kutaja jina la taasisi hizo.

Kwa maana nyingine, hiyo ingeweza kwenda kwa kiasi cha kusema na katika Katiba hii tume hii itaitwa… Kwa kuwa haijataja jina, Serikali ikaamua. “That wasn’t a great deal at all (hicho sio kitu kikubwa). Kama mtu atafungua shauri mahakamani leo, hawezi akafaulu, sheria mpya inachokifanya ni kuongeza jina.

“Hiyo ndiyo ilikuwa mijadala yao, sasa sheria imepita, wanarudi tena kuigeuza,” amesema.

Alipoulizwa kuhusu muundo wa tume na haja ya kuwa na mabadiliko madogo ya Katiba ili kuifanya tume kuwa huru, Dk Feleshi alisema suala hilo lilishajadiliwa kwenye mikutano ya Kituo cha Demokrasia (TCD) na ikaonekana kwamba Katiba itabidi isubiri.

“Hata Mheshimiwa Rais (Samia Suluhu Hassan) akawaambia mchakato wa kubadili Katiba siowa vyama, ikiwemo CCM, Chadema wala CUF, ni mchakato wa Watanzania.

“Walikuja tena na hoja kwamba kunatakiwa kuja na mabadiliko madogo ya Katiba, hivi utakuwa na akili kweli uchukue kitu kidogo kwenye Katiba wakati una mchakato mkubwa umeshaweka roadmap (mpango kazi)?

“Serikali imeshaweka mchakato wa kutoa elimu ili tuwe na mchakato wa mabadiliko uliokwishaanza tangu awamu ya nne.

“Ndiyo maana ya Serikali kuamua kwamba, kwa sababu ibara ya 74 inasema kwa mujibu wa Katiba hii, yaweza kutungwa sheria mahsusi. Kwa mfano namna ya kuwapata wale wajumbe wa tume na mambo mengine, hilo lilikuwa ni ombwe ambalo haliwezi kusubiri marekebisho ya Katiba,” amesema.

Alisema ili kubadilisha Katiba ya Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya tume, kuna hoja nyingi tu, sio ya jina.

“Kuna mambo ya kubadilisha madaraka ya Rais, utayajadili bila kurudi kwa wananchi? Kuna kuanzisha mahakama ya upeo, utajichukulia mamlaka kupitia marekebisho madogo?” amehoji.

Alipoulizwa kuhusu mamlaka ya Rais kuteua watendaji wa INEC, Dk Feleshi alisema: “Hizo ni assumptions (dhana), halafu ukisoma sheria yetu ibara ya 30, sheria ikishatungwa kama ina dosari, kwa nini mtu asiipinge mahakamani ifutwe?”


Ni mkanganyiko

Kwa upande mwingine, Mratibu Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa aliyezungumza pia katika kipindi hicho, amesema sheria hiyo inaanza kutumika ikiwa na utata.

“Sheria hii imeanza kutumia leo (jana)  lakini wananchi wamepata mkanganyiko mkubwa. Je, tunakwendaje kwenye uchaguzi ilhali tume na uongozi wake, kila kitu kimetokana na sheria ambayo imefutwa?” amehoji.

“Mimi ningependekeza tuanze kuvunja tume, kila kitu kianze upya. Pamoja na kwamba sheria ina changamoto zake lakini tuanze kutumia sheria hiyo, tupate timu ya usaili, uendeshaji wa uchaguzi,” amesema.

“Ili tume hiyo iwe huru ni lazima kuwe kuna mambo ya kuangalia, kwa mfano upatikanaji wa wajumbe, huwezi ukasema tume huru wakati wajumbe walipatikana kwa njia ambazo si za uhuru na uwazi,” amesema.


Matumaini ya Zitto

Akizungumza katika kipindi hicho, Kiongozi mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alishauri wadau kwanza washikilie mambo machache yaliyopatikana kwenye sheria ya sasa.

“Ni dhahiri kwamba hatuwezi kupata Katiba kabla ya uchaguzi mkuu, kwa hiyo ni lazima ujenge mazingira ambayo yatawafanya watu wakichaguliwa waingie bungeni,” amesema.

Alisema japo sheria hiyo inalalamikiwa, ina mambo mazuri ambayo ni pamoja na kuzuia wagombea kupita bila kupingwa.

Sheria imekataza wagombea kupita bila kupingwa. Zamani Rais alikuwa anaamka asubuhi anatangaza Tume, lakini sasa inabidi waombe, watu wachujwe ndipo Rais anaweza kutangaza.

“Zamani Rais alikuwa anaamka asubuhi anamwondoa kamishna na kumpangia kazi nyingine, sasa hivi ni lazima aunde kamati, ichunguze impelekee ushauri ndipo aamue,” amesema.