Wadau wang'aka mabadiliko jina la Tume ya Uchaguzi

Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi

Muktasari:

 Baada ya kukamilika kwa mabadiliko ya sheria ya tume ya taifa ya uchaguzi, hatimaye jina la tume inayosimamia uchaguzi linatarajiwa kubadilishwa Aprili 12, mwaka huu


Dar es Salaam. Wakati Serikali ikitangaza mabadiliko ya jina la tume ya uchaguzi kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, wadau, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa wametaka mabadiliko hayo yaendane na mabadiliko ya muundo kwa mujibu wa Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na.2 ya 2024.

Sheria hiyo ni miongoni mwa sheria tatu zilizotiwa saini na Rais Samia Suluhu Hassan, zikiwamo Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2024.

Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Matinyi ilisema kuwa, mabadiliko hayo yanafuatia tangazo la Serikali Na.225 la Machi 29, 2024, ambapo sheria hiyo itaanza kutumika Aprili 12, 2024.

Hata hivyo, tangazo hilo limewaibua wadau, wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa wakitaka mabadiliko hayo yaendane na utekelezwaji wa sheria yote ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Akizungumza na Mwananchi jana, Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Dorothy Semu alisema kutangazwa kwa jina jipya ni hatua moja, ila wanaitaka Serikali iendelee kutekeleza yaliyomo kwenye sheria, ikiwemo kuwapata wajumbe wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi

“Pia Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imepewa wajibu wa kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa na imeelekeza waziri husika kuleta sheria kuhusu uchaguzi huo utakavyokuwa.

“Hivyo, tunategemea sheria ya usimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa italetwa haraka iwezekanavyo na mengine ambayo tume imepewa mawanda ya usimamizi wa sheria, ikiwemo kupata makamishna wapya wa tume kwa njia ya kutangazwa na kusailiwa,” alisema.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika akizungumzia mabadiliko ya jina hilo, alisema yalipaswa kuanzia kwenye mabadiliko ya Katiba.

Akionyesha dosari ya tume hiyo, Mnyika alisema kwa mujibu wa Katiba, uamuzi wowote unaofanywa na tume hiyo hauwezi kuhojiwa na kama mtu anataka kuyapinga apinge uchaguzi, jambo alilosema linaifanya tume hiyo isiwe huru.

Akigusia mfumo wenyewe, Mnyika alisema tume ni ya Serikali, kwani wadau hawana uwakilishi ndani yake na hata uundaji wake kwa muswada uliopo ni danganya toto.

“Muswada wa sasa ni sheria ambayo ni danganya toto, wamesema kutakuwa na kamati ya uteuzi kabla tume haijateuliwa, lakini hiyo kamati ni ya kina nani? Ni Jaji Mkuu wa Muungano, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Utawala Bora na makamu wake kwa upande wa Zanzibar? Kwa hiyo kwa msingi hii ni Tume ya Rais,” alisema Mnyika.

Alisema kwa Katiba iliyopo matokeo ya urais hayawezi kuhojiwa mahakamani, hivyo hata tume ikiwa bora kiasi gani itafanya vurugu zote, lakini matokeo ya urais hakuna pa kukimbilia.

Aliendelea kusema katiba ya sasa inaelekeza watumishi wa umma na haijaweka utaratibu wa tume kuajiri watumishi wake, hivyo itakuwa ikiamua aina ya watumishi wa umma kusimamia uchaguzi.

Mnyika amerejea kifungu cha 27 cha sheria hiyo, akisema kinatoa mwanya kwa tume kutumia wakurugenzi wa halmashauri na watendaji kusimamia uchaguzi.

Naye kiongozi mstaafu wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameandika katika ukurasa wake wa X, akisema, “Kwa kuwa Sheria mpya ya Tume Huru ya Uchaguzi imeanza kutumika na kwa kuwa makamishna wa tume wanaohudumu walipatikana kabla ya sheria hii na kwa mazoea tu (hapakuwa na Sheria ya Tume ya Uchaguzi kabla ya sasa), tunawasihi wajumbe wa Tume ya Uchaguzi waliopo wajiuzulu.”

“#NEC ijiuzulu ili Watanzania wapate makamishna wanaotokana na sheria mpya kwa njia ya ushindani.” lilisomeka andiko hilo.