Tumeshaandaa ramani hali ya udongo nchi nzima – Tari

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kilimo Tanzania (TARI), Dk Godfrey Lukamilo (wa pili kulia) akizungumza wakati wa kongamano la Shamba Darasa lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kupitia Farm Clinic, jijini Mbeya
Muktasari:
Ili kuifikia ajenda ya 10/30, Taasisi ya Kilimo Tanzania (TARI) imeshaandaa ramani ya hali ya udongo nchi nzima ili kumsaidia mkulima kutambua afya ya udongo kabla hajalima.
Mbeya. Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kilimo Tanzania (TARI), Dk Godfrey Lukamilo amesema wameshaandaa ramani inayoonyesha hali ya udongo nchi nzima ili wakulima wanapolima mazao yao, wajue afya ya udongo.
Amesema afya ya udongo ni muhimu katika kufikia ajenda ya kilimo kukua kwa asilimia kumi ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza jana Alhamisi Agosti 4, 2022 katika Kongamano la Shamba Darasa lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) kupitia Farm Clinic, Jijini Mbeya, Dkt Lukamilo amesema ramani hiyo tayari wameisambaza kwenye halmashauri zote ili iwafikie wakulima.
“Ramani inaonyesha eneo hili kuna udongo wenye rutuba ya chini na ili uzalishe unatakiwa ufanye hivi, tayari tumeshasambaza ramani kwenye halmashauri mbalimbali ili wawasaidie wakulima kutoa elimu kwa wakulima,” alisema kiongozi huyo wa Tari.
Dk Lukamilo alisema ili kufikia ajenda hiyo Tawi wamewekeza kwenye utafiti kwa kuhakikisha wanaendelea kuzalisha mbegu za kisasa na kuwafikishia wakulima.
“Jukumu letu kubwa ni kufanya tafiti za kilimo na jambo la kwanza ni kupata matokeo ya tafiti tunazofanya nia ni kupata teknolojia, ubunifu na mbinu za kilimo bora ili kuongeza tija na uzalishaji katika kilimo,” alisema
Alisema kufanya tafiti na kupata teknolojia ni jambo moja lakini kuifikisha teknolojia hiyo kwa wakulima ni jambo la pili.
“Suala la kufikisha teknolojia linahitaji wadau wengi, sisi kama Tari zipo mbinu mbalimbali za kuwafikishia wadau teknolojia,” alisema.
Alisema njia moja wapo wanayotumia katika kufikisha taarifa hizo ni vyombo vya habari na kwamba, wanathamini mchango wa wanahabari katika kuifikisha teknolojia kwa wakulima.
“Njia nyingine, tumeweka vituo kwa ajili ya kutolea mafunzo kwa wakulima na kila kituo kuna wadau wapo hapo,” alisisitiza.
Alisema ili kurahisisha utendaji wa kazi wa Tari na kuongeza ufanisi wanafanya kazi kwa mtandao wa vituo 17 nchini.