Tuna viongozi wasio na sifa ya kuongoza

Wednesday September 29 2021
viongozipic
By Mwandishi Wetu

Dunia ina njaa na kiu ya viongozi bora. Iwe ni katika siasa au serikalini, njaa yetu ya kupata viongozi bora ni kubwa sana.

Ukigeukia katika familia, jamii na katika taasisi za dini, hali ni hiyo hiyo. Viongozi bora si wengi. Viongozi wanaotawaliwa na ubinafsi na umangi meza ni wengi mno.

Kwanza kiongozi bora ni mwadilifu kwa kiasi kikubwa. Anachosema ndicho kilicho moyoni mwake na ndicho anachoamini. Ni mkweli.

Viongozi wengi ni vigeugeu wanaokwambia hili lakini wanatenda vingine. Wanakwambia watafika

Kiongozi mwadilifu akikuambia njoo kesho saa fulani, ukifika utamkuta anakusubiri.

Atakusikiliza kwa moyo wake wote na akili yake yote. Atafunga simu yake na akiwa na dharura ya kutumia simu atakuomba radhi.

Advertisement

Atakuambia wazi wazi kama ataweza kukusaidia au hapana. Ikiwa lazima, atakuelekeza uende wapi na kwa nani kwa msaada zaidi. Akisema ndio, ni ndio na hapana ni hapana. Huyu ni kiongozi bora.

Kiongozi bora ni mtumishi wa wengine. Hapa tuna njaa kubwa sana ya viongozi watumishi. Ni wengi mno wapatapo uongozi wanajiona kwamba wao ni bora kuliko wengine. Wanapenda kuitwa “mkuu” au “boss.”

Wanajisikia vizuri kuitwa hivyo. Kumbe mara nyingi wanaowaita hivyo nao pia wanasaka masilahi binafsi.

Ni bahati mbaya iliyoje kwamba tunawaita “watumishi wa umma” kumbe ukweli ni kwamba wao ni maboss na watumikiwa!

Viongozi hawa wanapenda kusifiwa, kuitwa waheshimiwa na kuogopwa na walio chini yao. Kiongozi huyu hatufai.

Tunatamani kiongozi awe mnyenyekevu, anayejiona kwamba yeye ni mtu binadamu kama wengine.

Kiongozi bora huongozwa na busara. Ana maarifa mengi, lakini busara ndio inampa dira ya maisha. Eleonor Roosevelt, mwanasiasa na mwanaharakati wa Marekani, anasema:

“Unapojitawala mwenyewe, tumia akili yako, unapotawala wengine, tumia moyo wako.”

Kiongozi bora awe tayari kukosolewa na wale anaowaongoza. Afurahie zaidi kukosolewa kuliko kusifiwa. Apende kusikia mawazo mbadala. Kiongozi atambue kwamba wapo wengi anaowangoza ambao ni wasomi kuliko yeye, wenye busara kuliko yeye, wenye maarifa mengi kuliko yeye, tena wapo wengine waliostahili pia kupata hiyo nafasi ya uongozi.

Pia atambue kwamba, kila mtu, hata wale anaodhani hawakusoma sana au ni hohe hahe wa mtaani, wana mawazo mbadala ambayo mara nyingi ni mwanga kwa huyu kiongozi. Akitambua hivyo atakuwa mnyenyekevu na atawasikiliza.

Kiongozi bora ajiongeze daima katika kusoma na kujiendeleza katika fani yake na fani nyingine.

Awe msomi mwendelevu wa maarifa mengi. Dunia inabadilika sana na maarifa mapya yanaibuka kila siku.

Kiongozi asiyetambua kwamba elimu haina mwisho ataachwa nyuma na wakati, atashindwa kuendana na kasi ya zama hizi za sayansi na teknolojia. Viongozi wengi hawajasoma chochote tangu wahitimu elimu ya sekondari au chuo. Wapo wengi mno hata makala za aina hii hawatasoma.

Kiongozi bora atambue kwamba muda wake madarakani ni mfupi sana. Ipo siku madaraka hayo yatakoma kwa kustaafu, kuenguliwa, kuugua au kufa. Muda wetu ni mfupi sana hapa duniani.

Aliye juu mngoje chini, huu ni msemo wa Kiswahili. Mpanda ngazi hushuka. Kiongozi akitambua hivyo, atakuwa mnyenyekevu, mwadilifu, msikivu na mtumishi wa umma.

Mwandishi Jack Welch ameandika kwamba mtu asiye kiongozi bora hushughulikia tu masilahi yake, na hapo atakapotambua maana ya uongozi bora, ataanza kujishughulisha na masilahi ya wengine. Atafanya jitihada zote ili wale awaongozao wafaidike.

Lakini sivyo ilivyo katika hali yetu ya sasa. Wengi hutafuta uongozi kwa masilahi binafsi na masilahi ya familia zao, iwe ni kwa nafasi za kuchaguliwa au kuteuliwa.

Matokeo yake tunaona wananchi bado wanaendelea kukosa elimu bora, kukosa huduma za msingi za afya. Ubinafsi unadhoofisha jamii na taifa.

Tutawapataje viongozi bora? Tuanzie katika familia. Wazazi ni viongozi wa familia zao. Tuwatayarishe wanandoa watarajiwa kwa kuwapa elimu kuhusu majukumu ya ndoa kabla hawajafunga ndoa. Naamini kwamba hii ni hatua ya mwanzo na ya lazima sana.

Pia tufundishe maadili kama somo katika ngazi zote za elimu, na hili la uongozi bora lifundishwe kuanzia shule za msingi hadi chuo kikuu.

Uongozi bora pia uwe ni somo katika taasisi za dini. Tunatamani viongozi wa dini na viongozi wengine wote wawe mfano bora kwa jamii.

Kiongozi bora asiwe na maneno mengi, bali awe mwingi wa vitendo na mifano bora kwa anaowaongoza. Hivi ndivyo viongozi wetu wanavyotaliwa kuwa.


Imeandikwa na Profesa Raymond S. Mosha (255) 769 417 886; (255) 783 417 886. [email protected] www.rsgmosha.com

Advertisement