Tunzaa yaja na muarobaini matumizi bora ya fedha kwa wanunuaji na wauzaji wa huduma na bidhaa

Mwanzilishi wa Tunzaa Fintech, Ng’winula Kingamkono akiwa anazungumza

Muktasari:

Tunzaa Fintech imezinduzi wa programu ya simu (‘mobile application’) “Tunzaa” kwa ajili ya kukuza tabia chanya za kifedha kwa Vijana wa Kitanzania.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha matumizi bora ya fedha, Tunzaa imezindua jukwaa lake jipya la kukuza tabia chanya za matumizi ya kifedha kwa vijana wa Kitanzania kupitia teknolojia ya simu za rununu yaani ‘smart phones’.

Tunzaa ni kampuni changa (‘start up’) ya ‘fintech’ ya Kitanzania inayotumia teknolojia kubadilisha tabia za matumizi ya kifedha za watumiaji na inawaunganisha wafanyabiashara na wanunuzi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Jumanne Aprili 20, 2021 Jasmine Lupatu amesema kuwa Tunzaa imeundwa kuwezesha malipo ya bidhaa na huduma kwa kiwango kidogo cha pesa kwa kasi ya mtumiaji mwenyewe moja kwa moja kutoka kwenye simu zao na kuifanya iwe rahisi kufikia malengo na mipango yao.

"Fikiria safari ya kwenda Zanzibar na mtu unayemjali, sasa tunakupa kifaa cha kukufikisha kwenye lengo hilo kwa kulipia huduma polepole kwa kasi yako mwenyewe na programu za Tunzaa", amesema Jasmine Lupatu

Amesema kuwa Tunzaa huwapa watumiaji uwezo wa kufuatilia kila pesa wanayoweka kando kwa lengo maalum kwa wakati halisi mfano unataka kununua TV mpya kabisa, au iPhone/Samsung Galaxy ya hivi karibuni au kusafiri kwenda Zanzibar.

Watumiaji wa Tunzaa wanapata bidhaa na huduma kutoka kwa wafanyabiashara kuanzia vifaa vya nyumbani, safari, Runinga, Mashine za kufulia, Friji, Simu za Mkononi, kompyuta na nyinginezo zinazowapa watumiaji njia rahisi ya kulipia huduma na bidhaa na kufuatilia matumizi yao.

Tunzaa inawazawadia watumiaji na pointi ambazo zinaweza kutumika katika maduka makubwa, migahawa au biashara zingine ili kuhimiza tabia chanya za matumizi ya fedha.

Akizungumza na waandishi wa habari, mwanzilishi wa Tunzaa Fintech, Ng’winula Kingamkono amesema ”Safari ya kutengeneza bidhaa hii ni tofauti na nyingine yoyote tuliyowahi kufanya. Tazama, kwenye Tunzaa tunahakikisha tunakidhi mahitaji ya soko sahihi na tumekuwa tukijishughulisha na utengenezaji wa Tunzaa kwa utulivu kwa miezi kadhaa iliyopita tukijaribisha mifano (prototype) zaidi ya mitano bidhaa hiyo hadi sasa." Amesema Kingamkono ambaye ni mwanzilishi wa Tunzaa Fintech na mtaalamu mwenye uzoefu wa zaidi ya miaka 10 katika utengenezaji wa program.

Kwa sasa huduma hii inapatikana kwa mualiko maalum tu ikiwa kwenye majaribio, Tunzaa inakaribisha idadi ndogo ya watumiaji ili kuweza kujifunza zaidi na kuboresha uzoefu wa watumiaji na watu wanaopenda wanaweza kujisajili kupata toleo la beta (majaribio) la Tunzaa kwa kutembelea wavuti yao.