Rais Samia, viongozi Afrika wataka mikopo nafuu

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi pamoja na wageni mbalimbali walioshiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika wenye lengo la kuainisha vipaumbele vya nchi hizo ili viweze kuzingatiwa kwenye mzunguko wa 21 wa IDA katika ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Kenyatta (KICC) jijini Nairobi, Kenya leo Aprili 29, 2024. Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Asisitiza upatikanaji wa mikopo yenye masharti ya kulipa baada ya miaka 50.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ili kuziwezesha nchi za Afrika kuwa na maendeleo shindani duniani, ni muhimu taasisi za fedha za kimataifa zizingatie utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu.

Amezitaka taasisi hizo kurahisisha masharti ya mikopo ili nchi za Afrika zijiinue kimaendeleo.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Jumatatu, Aprili 29, 2024 alipohutubia mkutano wa 21 wa wakuu wa nchi wa Shirikisho la Kimataifa la Maendeleo (IDA), jijini Nairobi nchini Kenya.

Katika hotuba yake, Rais Samia amesema nchi za Afrika na dunia kwa ujumla, zipo katika kipindi ambacho, majanga mbalimbali yanazikabili.

Katika kufanikisha ukuaji wa maendeleo shindani, hasa kwa nchi za Afrika, ametoa wito kwa IDA kufanikisha hilo, akisisitiza upatikanaji wa mikopo yenye masharti ya kulipa baada ya miaka 50.

“Kwa kuzingatia changamoto zilizopo, naamini IDA itaendelea na utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu zaidi kama vile ile ya kulipa ndani ya miaka 50. Uwezeshaji huu unatoa nafasi zaidi kwa Afrika kushindania mahitaji ya maendeleo,” amesema.

Amesema Afrika inahitaji uhaulishaji wa teknolojia na namna ya kuzitumia ili ifikie maendeleo yanayotarajiwa na shirikisho hilo, huku akirejea fursa ambazo Tanzania imezipata kupitia IDA.

Ametaja miongoni mwa fursa hizo ni mpango wa utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya Bonde la Msimbazi ambao Benki ya Dunia (WB) imetoa fedha kuufadhili.

Amesema shirikisho hilo limeinufaisha Tanzania kwa kuiwezesha kuboresha huduma za afya ya uzazi, ufikishaji wa huduma ya umeme vijijini na kuongeza upatikanaji wa majisafi na salama.

Ameeleza kuwa mkutano huo unakuja katika kipindi ambacho sera na mipango imeboreshwa kurahisisha utekelezwaji wa shughuli mbalimbali.

Matarajio yake, amesema IDA iziwezeshe baadhi ya nchi kukua kiuchumi na maendeleo.


Uwezeshaji mabadiliko tabianchi

Viongozi wengine wa Afrika wamezisisitiza nchi tajiri kutoa michango kwa Benki ya Dunia ili kuiwezesha kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kusaidia maendeleo na kukabili athari za mabadiliko ya tabianchi.

Nchi hizo tajiri zinatarajiwa kutoa ahadi ya michango yao kwa IDA katika mkutano utakaofanyika Japan, Desemba 2024.

"Tunatoa wito kwa washirika wetu kuhakikisha wanaongeza michango yao ndani ya IDA... angalau ifikie Dola za Marekani 120 bilioni," amesema Rais wa Kenya, William Ruto katika mkutano huo.

Katika hotuba yake  Ruto amesema uchumi wa nchi za Afrika umetikisika kutokana na madeni na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayohitaji hatua za haraka kujiokoa.

Ametoa mfano wa Kenya inayokabiliwa na mafuriko yaliyopitiliza, huku mataifa mengine ya Kusini mwa Afrika, ikiwemo Malawi yakikabiliwa na ukame.

Iwapo wadau hao wataahidi kiwango hicho kilichopendekezwa na viongozi wa Afrika, kitakuwa cha kwanza kwa ukubwa tangu ahadi zilizowahi kutolewa mwaka 2021 zilizoishia Dola za Marekani 93 bilioni.

IDA inatoa mikopo yenye riba nafuu kwa nchi 75 zinazoendelea duniani na zaidi ya nusu zinatoka Afrika.

Fedha hizo kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zinatumika na Serikali za nchi hizo kugharimia upatikanaji wa nishati na huduma za afya, uwekezaji kwenye kilimo na kujenga miundombinu, ikiwemo ya barabara.

Rais wa Benki ya Dunia, Ajay Banga alitumia jukwaa hilo la IDA kuahidi kuondoa vikwazo vyote vinavyotatiza ukopaji ili kuongeza ufanisi na urahisi katika utolewaji wake.

"Tunaamini IDA ikiwa rahisi inaweza kuleta matokeo makubwa na yenye maana zaidi ukilinganisha na kuweka mazingira magumu,” amesema Banga.