Mashirika ya kimataifa yanavyoinyima Afrika uwezo kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi

Moja ya maeneo yaliyoathiriwa na Kimbunga Idai kilichotokea mapema mwaka huu na kusababisha uharibifu wa miundombinu na majanga mengine vikiwamo vifo katika nchi za Zimbabwe, Msumbiji na Malawi.
Dar/Zimbabwe. Tinozivei Mabanga (43) mkazi wa Wilaya ya Chipinge nchini Zimbabwe anaisubiri masika ya mwaka huu kwa hofu. Ingawa ni mkulima, baba huyo wa watoto wanne anayo kila sababu ya kuogopa.
“Bado taswira ya kilichotokea Machi kimbunga Idai kilipopiga eneo hili haijanitoka. Na nikiona masika nyingine inakaribia na sijapata makazi ya uhakika kulaza kichwa changu, nasononeka,’ anasema Mabanga aliyepoteza ndugu watatu kwenye kimbunga hicho.
Taarifa za Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) zinaonyesha zaidi ya watu 270,000 waliathirika na kimbunga hicho na 50,905 kati yao kutoka wilaya 12 nchini Zimbabwe wakilazimika kuyahama makazi yao. Kaya 223 zinaishi ukimbizini mpaka sasa.
Katika Wilaya ya Chipinge iliyopo kusini mwa Zimbabwe ni miongoni mwa maeneo yaliyoharibiwa zaidi na kimbunga Idai na mpaka sasa maisha bado hayajarejea kama zamani.
“Ingawa tunapokea msaada kutoka kwa wafadhili na wasamaria wema, miundombinu mingi bado haijakarabatiwa. Barabara na madaraja yameharibika, nguzo za umeme bado zimeanguka,” anasema Mabanga.
Mwezi uliopita, mkurUgenzi mkazi wa lishe na chakula wa Umoja wa Mataifa, Hilal Elver alitahadharisha uwezekano wa kutokea njaa kubwa nchini humo kutokana na ukame pamoja na kutoboreshwa miundombinu ya kiuchumi.
Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, matukio ya kutokea kwa vimbunga mfano Idai kilichozikumba Malawi, Msumbiji na Zimbabwe kilisababisha zaidi ya vifo vya watu 1,000 yamekuwa yakishamiri.
Benki ya Dunia inakadiria kuwa nchi hizo zinahitaji walau Dola2 bilioni za Marekani kukarabati miundombinu iliyoharibika na kurudisha huduma kama zilivyokuwa mwanzo huku wachambuzi wakisema kuna haja kwa Serikali za Afrika kuhakikisha zinakusanya kodi ya kutosha kutoka kampuni za kimataifa zinazovuna rasilimali kwenye mipaka yao.
Taasisi ya kusimamia rasilimali za asili Afrika (NRGI) inasema ingawa Afrika imebarikiwa rasilimali nyingi, haineemeki sana huku sekta ya madini ikiongoza kutokana na kampuni za uchimbaji kutolipa kodi kwa kipindi kirefu cha operesheni zao.
Mratibu wa Shirika la Mazingira la umoja wa Mataifa (Unep), Dk Richard Munang anasema Afrika inapoteza Dola 50 bilioni za Marekani kila mwaka kutoana na ukwepaji kodi huku ikihitaji Dola 10 bilioni kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
“Afrika inahitaji fedha kukabili changamoto zilizopo. Kudhibiti ukwepaji kodi ni muhimu sana. Jamii ya kimataifa inajitahidi kusaidia fedha kutoka nchi zilizoendelea lakini bado mahitaji ni makubwa. Kutegemea misaada kunaonekana hakutoisadia Afrika, inahitaji kudhibiti ukwepaji kodi hasa kutoka kwa wachimbaji wakubwa wa kimataifa ambao huchangia pa kubwa katika uchafuzi wa mazingira,” anasema Dk Munang.
Tancoal Tanzania
Kampuni ya Tancoal inayochimba makaa ya mawe wilayani Mbinga hapa Tanzania ni miongoni mwa mifano ya kampuni zinazotumia hila kukwepa kulipa kodi ya Serikali huku ikihamisha mabilioni ya shilingi.
Ingawa kimbunga Idai hakikuipiga Tanzania, bado inapata athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile mafuriko na ukame ambayo huongeza umaskini wa wananchi.
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2016/17 inaonyesha ukaguzi maalumu wa ubia wa uendeshaji kati ya Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) linalomiliki asilimia 30 na kampuni ya Intra Energy Tanzania Limited (IETL) inayomiliki asilimia 70 za Tancoal ulibaini miamala kadhaa iliyoenda kinyume na utaratibu.
Mapitio ya taarifa za fedha za Tancoal kuanzia mwaka 2011 hadi 2016 yalionyesha matumizi yasiyostahili ya Sh6.58 bilioni katika utafutaji wa madini kwani utafiti uliisha mwaka 2012. Sh880.7 milioni kati ya fedha hizo zilijumuishwa isivyostahili.
CAG alisema kuingizwa kwa gharama hizo katika taarifa za fedha kumeonyesha Tancoal imepata hasara hivyo Serikali haikulipwa gawio wala kukusanya kodi ya mapato.
Mapitio ya hati za malipo kuanzia mwaka 2014 hadi 2016 yalibaini Tancoal ilitumia Sh940.34 milioni kwenye shughuli zisizohusiana na uchimbaji madini.
Kadhalika, Dola 3.35 bilioni zililipwa kwa Tancoal ya nchini Malawi ambayo ni kampuni ya tanzu ya Intra Energy kama ada ya ushauri, gharama za kukodisha mtambo, masoko na malipo mengine ya kampuni yote hayakuhusiana na shughuli za Tancoal Tanzania.
Matumizi haya yote yalisababisha Tancoal kupata hasara hivyo kutotoa gawio wala kulipa kodi.
Taarifa za fedha za Tancoal pia zinaonyesha kuanzia Juni 2013 hadi Machi 2017 kampuni ililipa jumla ya Sh7.26 billioni kama ada za usimamizi wa menejimenti lakini yakaonyeshwa ni mkopo unaopaswa kulipwa na kampuni hiyo kubwa ya uchimbaji makaa ya mawe nchini.
Ulipaji wa mkopo huo ulianza Mei 21, 2013 ambao ni jumla ya Dola 1.81 milioni za Marekani na mpaka mwaka 2017 kampuni ya IEC ilikuwa imeshalipwa Dola 1.72 milioni. Kati ya fedha hizo, zaidi ya Dola 667.18 milioni za Marekani sawa na Sh1.47 bilioni zililipwa kama ada ya menejimenti kinyume na maelekezo ya bodi ya wakurugenzi ambayo Novemba 2012 iliamua kutokuwa na makubaliano ya huduma ya usimamizi.
“Malipo ya ada za menejimenti kinyume na idhini ya bodi ya wakurugenzi yamepunguza faida ya kampuni hivyo Serikali kutokusanya kodi inayostahili,” amebainisha CAG.
CAG pia, amebainisha udanganyifu katika shughuli za maendeleo ya jamii (CSR). Taarifa za fedha za kampuni hiyo kuanzia mwaka 2012 hadi 2016 zilionyesha ilichangia Sh993 milioni huko Ngaka na Songea lakini ukaguzi ukabaini kiasi kilichotolewa na kuthibitishwa na meneja mwenye jukumu la shughuli hizo ni Sh75.4 milioni tu.
“Menejimenti ya Tancoal haikuwa na nyaraka zozote zinazothibitisha matumizi ya Sh917.62 milioni. Kujumuishwa kwa kiasi hicho katika taarifa za fedha kunapotosha makusudi kwa taarifa za fedha,” alionya CAG na kuiagiza kampuni hiyo kurejesha kiasi ambacho hakina uthibitisho wa nyaraka na kurekebisha vitabu vyao vya hesabu.
Kwenye ripoti iliyofuata, mwaka 2017/18, CAG hakueleza chochote kuhusu mapendekezo aliyoyatoa kwa Tancoal. Juhudi za kuipata menejimenti ya kampuni hiyo kuzungumzia utekelezaji wa mapendekezo hayo kwa zaidi ya wiki mbili hazikuzaa matunda licha kuipigia simu mara kadhaa na kuitumia baruapepe kama ilivyotaka.
Hata hivyo, kwenye taarifa yake ya Oktoba, mwenyekiti wa IEC, Graeme Robertson alisema Tancoal ipo kwenye mazungumzo na Serikali ya Tanzania kutafuta suluhu ya mrabaha na ada za miaka ya nyuma.
“Tunaamini ushirikiano kati yetu utakuwa na matokeo mazuri zaidi kuliko migogoro. Tumechukua hatua kadhaa za makusudi kufanikisha hili ili kuwepo mazingira ya kunufaika kwa kila upande,” anasema Robertson.
Alipouliza CAG mpya, Charles Kichere kuhusu utekelezaji wa mapendekezo yaliyotolewa kwenye ripoti ya mwaka 2016/17 anasema ukaguzi walioufanya ulitokana na maombi waliyoyapokea kutoka Shirika la NDC linaloiwakilisha Serikali ndani ya Tancoal hivyo wao ndio wanaofahamu zaidi.
“Utekelezaji wa ukaguzi uliopita hupitiwa kila mwaka wakati wa ukaguzi wa kawaida au muda wowote ikitokea taasisi husika imeitwa mbele ya kamati ya Bunge. Kwa sasa tunakagua hesabu za mwaka 2018/19, natumaini utekelezaji wa hoja husika utazingatiwa,” anasema Kichere.
Alipotafutwa mkurugenzi mkuu wa NDC, Profesa Damian Gabagambi na kuulizwa kuhusu ukaguzi huo alisema tayari wameyafanyia kazi maelekezo waliyopewa na kurudisha taarifa ofisi ya CAG.
Ukwepaji kodi ni suala lililosababisha kufutwa kwa Kampuni ya Acacia iliyokuwa inamiliki migodi ya Bulyanhulu, North Mara na Buzwagi baada ya kubainika kutolipa stahiki za Serikali kwa zaidi ya miongo miwili ya kuchimba dhahabu nchini.
Baada ya mazungumzo na Serikali, Barrick ambayo ni kampuni mama ya Acacia ilikubali kulipa Dola 300 milioni za Marekani na kuunda kampuni mpya ya Twiga Minerals itakayohakikisha pande hizo mbili zinagawana mapato nusu kwa nusu.
Wadau
Katibu mtendaji wa Jukwaa la Kodi Afrika (ATDF), Logan Wort anasema nchi nyingi barani humu hazikusanyi kodi kama inavyotakiwa kutoka kampuni za kimataifa ambazo hutumia mbinu za hali ya juu kukwepa jukumu hilo.
“Kanuni za mgawanyo wa faida zilizopo hazizipendelei nchi za Kiafrika. Kuongezeka kwa uchumi wa kidijitali nako kunaongeza uwezekano kwa wageni na kampuni za kimataifa kuficha mapato yao kwenye nchi zinazowalinda,” anasema.
Mkurugenzi wa mazingira wa wizara ya mazingira nchini Zimbabwe, Washington Zhakata anasema Serikali yao imejipanga kupitisha sheria na kanuni zitakazozuia uzalishaji wa gesi ya kaboni kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
“Tupo kwenye mchakato wa kuwasilisha muswada bungeni. Upo mpango pia wa kuanzisha mfuko wa mabadiliko ya tabianchi utakaohusika kurekebisha maeneo yaliyoathirika zaidi,” anasema mkurugenzi huyo.
Wakati juhudi za kurekebisha miundombinu zikiendelea kutekelezwa nchini Zimbabwe baada ya uharibifu uliotokana na kimbunga Idai, Wilaya ya Chimanimani ilikumbwa na dhoruba kama hivyo mwezi uliopita na kubomoa shule tatu mjini humo.
“Maisha yetu tumemkabidhi Mola wetu. Hatuna amani tena katika eneo hili na hakuna mwenye uhakika nini kitatokea kesho hasa masika inavyokaribia,” anasema Mabanga.