Teknolojia kudhibiti uvujaji wa mafuta baharini

Muktasari:
- Imeelezwa kuwa, inapotokea mafuta yamwemwagika, mimea na viumbe hai vinakufa au kuondoka katika mazingira hayo
Dar es Salaam. Kampuni ya utengenezaji wa vifaa vya kukabiliana na uvujaji mafuta baharini ya Desmi Africa imekuja na teknolojia mpya kukabiliana na changamoto hiyo ya viumbe hai wa majini kufa au kuondoka.
Imeelezwa kuwa, inapotokea mafuta yamwemwagika, mimea na viumbe hai vitakufa au kuondoka katika mazingira hayo, hivyo kuathiri pia uoto wa asili wa eneo husika na kutopatikana tena.
Kutokana na hali hiyo, kampuni tanzu ya Desmi Africa ya Desmi Ro-Clean, yenye makao yake makuu mjini Odense, Denmark, imejitosa kukabiliana na tatizo hilo.
"Tunaamini maendeleo endelevu hayawezi kutenganishwa na uhamishaji wa maarifa na mbinu za mafunzo," amesema Leslie Peter Andrews, Mkurugenzi Mtendaji wa Desmi Africa alipozungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Julai 7, 2025.
"Uwekezaji wetu Tanzania si miundombinu pekee, ni kuhusu watu. Tumejikita katika kuwezesha timu za ndani kutoa huduma bora za kiwango cha kimataifa na kuchangia kwa namna chanya katika maendeleo ya ukanda huu," amesema.
Amesema wamefanya utafiti wa kina kabla ya kuamua kuja kuwekeza hapa nchini, akisema kuna bandari nzuri yenye miundombinu bora.
"Kuna mfumo mzuri wa elimu unaotuwezesha kufanikisha ujuzi wa kiufundi tunaohitaji, kuna usalama wote tunaohitaji, miundombinu tunayohitaji, eneo zuri, nchi inafaa kuwekeza kwa kipindi kirefu kwa kuwa, kuna utulivu wa kisiasa na ndio maana tupo kwa miaka kumi sasa," amebainisha.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari, Meneja Uendeshaji wa Desmi Africa, Philbertus Mujuni amesema:“Inapotokea mafuta yamemwagika baharini, kwenye mito au maziwa, athari zake ni kubwa.
“Kuna wanyama na mimea vinavyoishi baharini na nchi kavu, inapotokea mafuta yamwemwagika, mimea na viumbe hai vitakufa au kuondoka katika mazingira hayo, hivyo kuathiri pia uoto wa asili wa eneo husika na kutopatikana tena.
“Ili kuzuia hayo yasitokee ni lazima kuwe na vifaa, ndio maana sisi kama Desmi tumekuja na teknolojia inayoweza kusaidia kuzuia hili tatizo la kumwagika mafuta, kusambaa na kuathiri mazingira lisiweze kutokea," amesema Mujuni.
Amesema Desmi imekuwa ikifanya kazi nchini kwa zaidi ya miaka 10 na ofisi ya Tanzania imejikita kama kitovu muhimu cha shughuli za Desmi, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikihudumia sekta mbalimbali zikiwamo za mafuta na gesi, waendeshaji wa mabomba na bandari.
Mujuni amesema uwepo wa kampuni hiyo moja kwa moja nchini kutawezesha ushirikiano na Serikali za mitaa, mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi katika miradi inayohusu mazingira na maji, hatua inayoenda sambamba na kaulimbiu ya: “Kampuni ya Suluhisho safi kwa dunia bora."