Uamuzi wa Rais Samia wawagawa wachambuzi

Muktasari:
- Wasomi watoa maoni kuhusu uamuzi wa Rais Samia wapo wanaounga mkono hatua hiyo wakisema wanaamini Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka atatekeleza agizo la kuhakikisha makatibu wakuu na watendaji wakuu wote wa taasisi kupitia taarifa ya CAG na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zinazogusa maeneo yao.
Dar es Salaam. Wakati Rais Samia Suluhu Hassan akivunja bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Reli Tanzania (TRC) na kutengua uteuzi wa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ndege za Serikali, John Nzulule baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa na uchumi wamekuwa na maoni tofauti dhidi ya hatua hiyo.
Wapo wanaona hatua hiyo itasaidia kupunguza ubadhirifu, uzembe na matumizi mabaya ya madaraka yanayoisababishia hasara Serikali huku wengine wakiamini hakutakuwa na mabadiliko yoyote.
Wakizungumza na Mwananchi Digital, leo Jumatatu Aprili 10, 2023, wamesema wanaamini ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere kwa mwaka 2021/2022 iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita kama itafanyiwa kazi kikamilifu itakomesha ubadhirifu, uzembe na matumizi mabaya ya madaraka.
Wanaounga mkono hatua ya Rais Samia wamesema wanaamini Katibu Mkuu Kiongozi Dk Moses Kusiluka atatekeleza agizo la kuhakikisha makatibu wakuu na watendaji wakuu wote wa taasisi kupitia taarifa ya CAG na kuzifanyia kazi kwa haraka hoja zinazogusa maeneo yao na watakaobainika kuhusiska na ubadhirifu wachukuliwe hatua.
Akizungumza na Mwananchi Digital, Dk Aviti Mushi amesema, “Rais ana uwezo wa kuyafahamu haya mambo kabla ya ripoti haijamfikia, kuchukua hatua ni sawa je haya mambo yana mwisho?
Dk Mushi amesema nafasi za bodi na maofisa watendaji wakuu wa taasisi mbalimbali hazitafutwi kwa ushindani bali ni uteuzi unaofanywa na Rais hivyo ni vema zikapatikana kwa kushindanishwa.
“Wangewajibika kabla ya Rais hajawafikia, yaani mtendaji akiangalia ripoti yake mwenyewe anajikuchukulia hatua, lakini anasuburi hadi aondolewe naona ni udhaifu wao wa kutojitambua na kujielewa. Hii inaonekana hawawezi kujisimamia, ndio maana wanashindwa kusimamia maeneo yao.
“Ni hatua nzuri lakini haisaidii kwa nini amevunja moja tu, maana ni hasara ipo katika maeneo mbalimbali. Ilitakiwa kabla ya ripoti kutoka kwa umma, Rais alitakiwa awaambie hawa watu waachie ngazi mapema, kisha ahakikishe upatikanaji wa watendaji uwe wa ushindani,”amesema Dk Mushi.
Mchambuzi mwingine, Dk Faraja Kristomus amesema ni jambo la muhimu kwa Katibu Mkuu Kiongozi kulifanyia kazi jambo hilo, kwa sababu ndiye anayehusika na mapendekezo ya wajumbe wanaohusika katika bodi na watendaji wa mashirika ya umma
“Katibu Kiongozi yeye ndiye anayehusika na ajira zao, kuna tofauti kidogo kati ya ofisi ya Rais (Utumishi) na ofisi ya Rais inayosimamiwa na Katibu Mkuu Kiongozi anayesimamia makatibu wakuu na watendaji wa mashirika ya umma wanawajibika kwake.
Dk Kristomus amesema bodi nyingi za wakurugenzi hazijapewa meno ya kutosha ya kuwajibisha mashirika ya umma na bodi inaweza ikavunjwa lakini mchakato wa upatikanaji bodi mpya bado una changamoto kubwa.
“Baadhi ya mashirika ukifuatilia wajumbe wa bodi hawana sauti au umiliki wa kinachoendelea katika taasisi husika, matokeo yake tutaishia kuvunja bodi wee…Tatizo lipo kwa watendaji wakuu siyo bodi.
“Kinachotakiwa ni kuimarisha mfumo ili kupata watendaji wenye sifa, uadilifu na weledi. Lakini jingine kuangaliwa upya kwa mfumo wa uteuzi wa wajumbe wa bodi, wanatakiwa wawe wajumbe wenye uwezo wa kukosoa na kushauri, sio kuhudhuria vikao na kupitisha vitu,”amesema.
Dk Kristomus amesema changamoto iliyopo mwenyekiti anateuliwa na Rais hivyo hivyo kwa mtendaji au mkurugenzi, wakati wajumbe wa wanateuliwa na mawaziri.
Mchambuzi huyo ambaye ni mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amesema matokeo yake mwenyekiti na mtendaji au mkuregenzi wakiamua kuwa kitu kimoja, wajumbe hukosa cha kufanya.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Charles Matekela amesema Rais Samia, ameonyesha kwa vitendo umuhimu wa uwajibikaji kwa kuanza kutengua uteuzi wa baadhi ya viongozi waliohusika na kuisababishia Serikali hasara.
Amesema hatua ya kuwaagiza makatibu wakuu kufanyia kazi hoja za CAG, ni jambo la msingi lakini changamoto bado iko palepale bila kusimamia na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani hoja za CAG zitaendelea kujirudia mwaka baada ya mwaka.
“Kila taasisi lliyokaguliwa huwa inapewa barua ya kosoro zote zilizoibuliwa na CAG, ombi langu kila ofisa masuhuli achukue hatua stahiki, ikiwemo adhabu kali kwa wale wote waliotajwa.
“Pia bodi za wakurugenzi na kamati za ukaguzi ziwajibishwe kwa kasoro zilizotajwa.Vyombo hivi vina wajibu mkubwa katika utendaji wa taasisi za Serikali na mamlaka ya Serikali za mitaa na mashirika ya umma,”amesema Matekela.
Naye Kiongozi wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe amesema chama hicho kinapendeza kuundwa kwa kamati teule ya Bunge ili watendaji wa TRC wakijieleza ndani ya kamati hiyo kutokana na uzito wa hoja iliyoigusa taasisi hiyo.
“Ukiangalia hoja zote ni kubwa lakini hii ya TRC ni kubwa, ndio maana tumependekeza tusisubiri mchakato wa kawaida wa PAC. Hili suala la ndege za Serikali, Rais amechukua hatua moja kwa moja hatuwezi kuliingilia na halikuwa kwenye hoja za CAG,”amesema Zitto.