Ubelgiji yatoa Sh10 bilioni kukabili tabianchi

Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Peter Huyghebaert akipanda mti kama ishara ya kuzindua mradi wa uhifadhi wa mazingira dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma. Picha na Happiness Tesha

Muktasari:

Zaidi ya Sh10 bilioni zimetolewa na Serikali ya Ubelgiji kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo mradi wa uhifadhi wa mazingira kupitia Mpango wa Pamoja Kigoma (Kjp) kwenye maeneo yanayozunguka kambi za wakimbizi.

Kigoma. Zaidi ya Sh10 bilioni zimetolewa na Serikali ya Ubelgiji kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ukiwemo wa uhifadhi wa mazingira, kupitia mradi wa Pamoja wa Kigoma (Kjp) kwenye maeneo ya wananchi wanaoishi jirani na kambi za wakimbizi mkoani Kigoma.

 Akizungumza Juni 7, 2023 wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuhifadhi mazingira dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi, Balozi wa Ubelgiji nchini Tanzania, Peter Huyghebaert,  amesema mradi huo utasaidia jamii inayozunguka kambi za wakimbizi zilizopo mkoani humo.

Akiwa ameambatana na baadhi ya mabalozi wa nchi za Umoja wa Ulaya waliotembelea Mkoa wa Kigoma, Balozi Hyghebaert  amesema Serikali ya Ubelgiji imekuwa rafiki wa Tanzania na kusaidia katika miradi mbalimbali ikiwemo kilimo, hivyo kuwepo kwa mradio huo ni mwendelezo wa miradi mingine iliyokuwepo nchini ingawa huo umelenga hasa maeneo yanayozunguka kambi za wakimbizi.

Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), Mahoua Parums amesema mradi huo utasaidia kurudisha uoto wa asili uliopotea baada ya ujio wa wakimbizi katika maeneo ya mkoani humo, hivyo wananchi wanaozunguka maeneo hayo watanufaika ikiwemo kupata hewa nzuri inayotokana na uoto huo.

“Huwezi kuzungumzia wakimbizi ukaacha kuzungumzia jamii inayozunguka kambi za wakimbizi kwasababu ndio watu wanaokaa nao kwa muda mrefu na kutumia baadhi ya vitu vinvyowazunguka kwa pamoja,”amesema

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema mradi huo ni moja ya miradi iliyopo katika mradi wa KJP awamu ya pili ambayo inaelenga kusaidia wananchi wanaozunguka maeneo ya kambi za wakimbizi.

Mratibu wa Mradi wa Kjp awamu ya pili, Kanali  Rankho amesema mradio huo wa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2022/27 una lengo la kuhakikisha vipaumbele vya elimu bora, afya bora, kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, ulinzi, amani, haki na usawa pamoja na jinsia vinapatikana kwa wananchi wanaoishi maeneo jirani na kambi ya wakimbizi kwa ubora.

“Mpango huu unahusisha takribani mashirika 17 ya Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na Serikali ya mkoa wa Kigoma, ambapo yana vipaumbele tisa ikiwemo kutokomeza ukatili dhidi ya kina mama na watoto, afya, elimu , ulinzi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi,”amesema Rankho