Ubungo kujenga bustani maeneo yote ya umma
Muktasari:
- Manispaa ya Ubungo inatarajia kuja na mkakati wa kuboresha maeneo yote ya umma kwa kutengeneza bustani za maua ikiwemo stendi ya Magufuli, madaraja na vivuko na kuyafanya mazingira kuwa safi muda wote.
Dar es Salaam. Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imejiwekea mkakati wa kufanya usafi kwa kuboresha mazingira katika maeneo ya umma ikiwemo stendi ya Magufuli, madaraja, vivuko na makutano ya barabarani.
Hayo yamesemwa leo Agosti 21 na Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Hashimu Komba alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu ufunguzi wa kampeni ya mazingira wilayani humo unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu itakayokuwa na Kaulimbiu; ‘Kataa uchafu, safisha, pendezesha Ubungo’.
Amesema uboreshaji huo unahusu upandaji wa bustani kwa ajili ya mapumziko ya watu na huduma ya intaneti bure.
"Kampeni yetu itakayozinduliwa Jumamosi Agosti 26, 2023 katika Mtaa wa Manzese ni mwendelezo wa kampeni iliyofunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam hapo awali," amesema
Komba amesema lengo la kampeni hiyo ni kudhibiti taka ngumu kwenye Kata zote 14 mitaa 90, ili jamii ijenge utamaduni wa kutunza mazingira na kuifanya Ubungo kuwa kivutio.
"Wilaya ya Ubungo tumeshirikiana na wenzetu wa mazingira kuhakikisha kwamba kwenye maeneo yote ya umma tuliyonayo ambayo yanahitaji kupendezeshwa kwa kuwekewa bustani yanapendezeshwa.
"Kipaumbele chetu ni maeneo yafuatayo maeneo ya Ubungo Kijazi Interchange... eneo la pili ni stendi ya mabasi yaendayo mikoani ya Magufuli na eneo la tatu ni kwenye makutano ya barabara zote."
Ametaja maeneo mengine ya kipaumbele kuwa maeneo ya kuingilia katika jiji na hasa katika mpaka wake na Kibaha ambapo upendezeshwaji huo utafanyika kwa kuweka mazingira safi na mabango.
Komba ametumia fursa hiyo kuzishukuru taasisi mbalimbali waliokwisha kuonyesha nia ya kuchukua maeneo kadhaa kwa lengo la kuyaendeleza na kuwaalika wadau wengine kufanya hivyo.
Mkuu huyo wa Wilaya amesema wamepanga kuweka mashindano ya mitaa yote lengo likiwa ni kutoa hamasa kwa wananchi kufanya usafi.
"Kampeni hii itakuwa inatoa zawadi ya pikipiki, katika mitaa 90 mtaa ambao utaonekana umefanya vizuri kuliko mitaa yote utakabidhiwa pikipiki mbili.
"Pikipiki ya kwanza itakuwa ni ya Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa na pikipiki ya pili itakuwa ni mali ya mtaa ambayo itakuwa imesajiliwa kwa namba za halmashauri."
Komba amesema zawadi ya pikipiki itakayotolewa mara moja kwa mwaka, zawadi nyingine zitatolewa kila baada ya miezi mitatu kwa washindi watatu.
"Mtaa wa kwanza ambao utafanya vizuri tutawakabidhi shilingi laki sita, mtaa wa pili utakabidhiwa shilingi laki tatu na mtaa wa tatu shilingi laki mbili," amesema Komba.
Kwa mujibu wa Komba, mtaa utakaofanya vibaya nao hutoachwa nyuma kwani utapewa bendera yenye maneno "Balozi wa Uchafu," mpaka pale utakapojirekebisha.