UDOM yaanza mchakato kufundisha lugha ya Kirusi
Mwonekano wa Jengo la Utawala la Udom. Picha ya Mtandao
Muktasari:
- Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan alilolitoa Julai 5, 2026 akiwa ziarani nchini Russia ambapo aliitaka taasisi hiyo kuwa kituo cha ufundishaji wa lugha ya Kirusi ili kuzalisha wataalamu wa lugha hiyo.
Dodoma. Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kimeanza mchakato wa maandalizi ya kufundisha lugha ya Kirusi ambapo sasa kinaandaa andiko rasmi litakalowasilishwa kwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa ajili ya kupata ithibati ya kufundisha lugha hiyo.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alilolitoa Julai 5, 2026 akiwa ziarani nchini Russia ambapo aliitaka taasisi hiyo kuwa kituo cha ufundishaji wa lugha ya Kirusi ili kuzalisha wataalamu wa lugha hiyo.
Hayo yameelezwa leo Alhamisi, Julai 2, 2026 na Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano na Masoko wa UDOM, Rose Mdami wakati akizungumza na Mwananchi kuhusu mchakato huo.
Amesema hatua uandaaji wa andiko hilo unafanywa kwa ushirikiano baina ya Chuo kikuu cha Dodoma na Ubalozi wa Russia nchini Tanzania kupitia kituo kinachohusika na utamaduni wa Kirusi.
“Tupo katika hatua za awali za kuandaa andiko letu kwa kushirikiana na Ubalozi wa Russia kupitia kituo cha utamaduni ili kuliwasilisha mamlaka husika kwa ajili ya kupatiwa ithibati ya kufundisha somo hilo katika taasisi yetu ambalo tunatazamia kuanza katika mwaka wa masomo wa 2027/2028,” amesema Mdami.
Amesema andiko hilo litahusisha mapendekezo ya mtaala utakaotumika katika ufundishaji wa lugha hiyo ili kuhakikisha kuwa unakidhi mahitaji ya ufundishaji na viwango vya kitaaluma vinavyotakiwa ili kuwezesha uzalishaji wa wataalamu wanaokidhi vigezo.
Amefafanua kuwa ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu wa kigeni katika somo hilo wanatarajia kufundisha idadi kubwa ya walimu wa chuo hicho ili kuondoa utegemezi kwa walimu wa kigeni na kuondoa hatari za kusitishwa kwa ufundishwaji wa somo hilo kutokana uhaba wa walimu.
“Tuliwahi kufundisha lugha hii lakini tulikwama kutokana na changamoto ya Uviko-19, lakini tutakaporejea tutatoa nafasi kwa walimu wa chuo chetu kujifunza lugha hii ili kuondoa adha ya upungufu wa walimu hawa,” amesema.
Amesema lugha hiyo itafundishwa chuoni hapo katika ndaki ya Insha na Sayansi za Jamii (CHSS) kupitia Idara ya Lugha ambayo mpaka kufikia sasa inasimamia ufundishaji wa lugha za kigeni ikiwemo Kichina, Kiarabu na Kifaransa.
“Tunatarajia kuwa na kozi za muda mrefu kwa ngazi ya shahada na stashahada ambazo mwanafunzi atasoma kwa miaka mitatu na kozi za muda mfupi ambazo taarifa itatolewa baada ya mchakato kukamilika,” amesema Mdami.
Sambamba na hayo, Mdami ameeleza kuwa uanzishwaji wa programu hiyo utaongeza fursa za kimataifa kwa wanafunzi, ikiwemo ushirikiano wa kielimu na taasisi za nje ya nchi zinazotumia lugha ya Kirusi, hatua ambayo itakuwa sehemu ya juhudi za kukuza diplomasia ya elimu na uhusiano wa kimataifa.