Udsm: Tumieni elimu kuleta mabadiliko

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Jakaya Kikwete akiwatunuku Digrii ya awali ya Jamii na Elimu  wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye mahafali ya 53 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Dar es Salaam leo Oktoba 17, 2023. Picha na Michael Matemanga.

Muktasari:

  • Wahitimu wa vyuo nchini wameaswa kutumia elimu waliyoipata kuleta ushawishi chanya kwa watu wote wanaowazunguka.

Dar es Salaam. Wahitimu wa vyuo nchini wameaswa kutumia elimu waliyoipata kuleta ushawishi chanya kwa watu wote wanaowazunguka.

 Wito huo umetolewa leo Oktoba 17, 2023 jijini Dar es Salaam na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm), Profesa William Anangisye katika duru ya pili ya mahafali ya 53 ya chuo hicho.

Profesa Anangisye amewakumbusha wahitimu hao kuwa elimu waliyoipata ni mali ya umma hivyo ni lazima ilete faida kwa Watanzania.

"Elimu haiwezi kuleta faida na kuwa chachu ya mabadiliko yaliyokusudiwa kama haitatumika katika kutatua matatizo ya jamii," amesema.

Pia amewataka wahitimu hao kuwa wepesi katika kuangalia sehemu zingine ambazo maarifa na ujuzi wao unaweza kutumika kwa ufanisi zaidi kuliko kusubiri ajira kutoka Serikalini au katika sekta binafsi.

"Muwe watu wa kutafuta fursa badala ya kusubiri fursa ziwafuate, jambo ambalo si rahisi kutokea katika dunia ya leo ambayo ni kijiji chenye ushindani mkubwa.

"Mtakapokuwa mnatekeleza wajibu wenu wa kujitafutia maisha mazuri na kuendeleza nchi, muwe na hulka ya kuthubutu mambo ambayo yanaonekana ni magumu."

Vilevile amewasisitiza wahitimu kutovunjika moyo hata pale wanaposhindwa kufikia matarajio yao isipokuwa waendelee na kuwa ari hadi mafanikio yapatikane.

Aidha amewataka wahitimu kuwa wazalendo kwa nchi wakifahamu kwamba Watanzania wengi walioko vijijini na mijini wanatarajia mengi kutoka kwao.

"Matarajio ya Watanzania yanatokana na ukweli kwamba mmepata elimu yenye viwango stahiki, kutoka kwenye chuo kinachoheshimika duniani; na ukweli ni kwamba karibu wahitimu wote ni vijana wenye umri kati ya miaka 21 na 45," amesema.

Pia amewataka kulinda na kudumisha tunu za amani, umoja, mshikamano, uhuru wa nchi, Mapinduzi matukufu ya Zanzibar pamoja na Muungano wetu kama tunu za taifa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa baraza la chuo hicho, Balozi Mwanaidi Maajar amesema, baraza hilo linafahamu na linatambua madhara mbalimbali yanayosababishwa na uzembe wa wanafunzi kwa kutotimiza wajibu wao ipasavyo.

Amesema baraza linaendelea kuwasisitiza wazazi na walezi kusimamia misingi bora ya malezi kwa watoto haswa katika kipindi hiki cha utandawazi kwani bila kufanya hivyo kutakuwa na kizazi tegemezi ambacho hakiwezi kuwajibika ipasavyo.

"Ninaisihi jamii na taasisi mbalimbali zikiwemo za kidini, kurudi kwenye misingi bora ya malezi kwa kuliangalia suala hili kwa jicho la kipekee ili kulinusuru taifa letu la kesho na madhara yatokanayo na kizazi kisichowajibika," amesema Maajar.

Kwa upande wake mwanafunzi aliyehitimu Shahada ya awali ya Sayansi katika Takwimu za Bima, Elizabeth Kway, ameiomba Serikali kuangalia vijana kisheria na kisera, ili kuwawekea mazingira rafiki pindi wamalizapo masomo katika suala la ajira na kujiajiri huku akiainisha changamoto mbalimbali katika chuo hicho.

"Tunaiomba serikali kutusaidia changamoto mbalimbali zinazokabili chuo chetu hasa upungufu wa makazi kwa ajili ya wanafunzi yaani hostel, uchakavu wa miondombinu, upungufu wa vifaa vya kujifunzia kwa vitendo kwenye kozi za sayansi, uhandisi, insia, teknolojia pamoja na changamoto ya ulinzi na usalama wa maeneo yanayozunguka chuo," amesema Kway.

Pia amewataka wanafunzi wanaondelea na masomo katika chuo hicho kujitolea katika kila jambo wakitumia rasilimali za chuo kujifunza na kushirikiana.

Katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete amewatunuku wahitimu wapatao 2,796 kwa shahada za awali ambapo wanawake 1488, sawa na asilimia 55.1 ya wahitimu wote wa ngazi hiyo.

Kwa upande wa stashahada, jumla ya wahitimu walikuwa 78 ambapo wanaume wakiwa 45 na wanawake 33, sawa na asilimia 42.3 ya wahitimu wote wa ngazi hiyo.

Kada zilizohusika katika duru hii ni pamoja na Ndaki ya Sayansi Asilia na Afua, Ndaki ya Insia, Ndaki ya Habari na Teknolojia za Habari, Shule Kuu ya Madini na Jiosayansi, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Shule Kuu ya Biashara, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (Tataki) na Taasisi ya Sayansi ya Bahari-Zanzibar.