Udsm mwenyeji kongamano la kimataifa, vijana 500 kushiriki

Muktasari:

  • Takribani vijana 500 kutoka nchi 24 duniani, wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, unaotarajiwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuanzia Oktoba 4-7 2023.

Dar es Salaam. Takribani vijana 500 kutoka nchi 24 duniani, wanatarajiwa kushiriki kwenye mkutano wa kimataifa wa mabadiliko ya tabianchi, unaotarajiwa kufanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), kuanzia Oktoba 4-7 2023.

Mkutano huo ambao unalenga kuangalia ushiriki wa vijana katika mapambano dhidi ya mabadiliko hayo, utahusisha ushiriki kwa njia ya mtandao na uhudhuriaji ukumbini.

Hayo yameelezwa leo Oktoba 3, 2023 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uongozi wa Vijana Duniani (GYLC), Ejaj Ahmad na kuongezea kuwa mkutano  huo ni wa pili duniani na kwanza kwa Afrika baada ya ule uliofanyika nchini Bangladesh mwaka jana.

Kwa mujibu wa Ahmad, vijana 200 watahudhuria ukumbini, huku mgeni rasmi akitarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Selemani Jafo; vijana 300 washiriki mkutano huo kwa njia ya mtandao.

Pamoja na Jafo, viongozi wengine wanaotarajiwa kushiriki ni pamoja na Dk Richard Muyungi, ambaye ni Mshauri wa Rais, katika masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki, aliyekuwa Mshauri Mkuu wa Sayansi wa Serikali ya Uingereza, David King, pamoja na mabalozi wa mabadiliko hayo kutoka nchi mbalimbali.

Ahmad anasema lengo kubwa la mkutano huo ni kuwawezesha vijana kupata uzoefu na maarifa ya vitendo katika sayansi ya tabianchi, kuwapa maarifa ya uongozi, utetezi, na uhifadhi wa mazingira, na kuzingatia kukuza biashara ya kijamii kwa mustakabali endelevu.

"Pia kupitia mkutano huo tutajadili namna ya kuwawezesha vijana kutekeleza miradi ya namna ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi walioianzisha," amesema.

Ameongeza kuwa mkutano huo umeandaliwa kwa kushirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Taasisi ya Tathmini ya Maliasili katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (IRA).

Mkurugenzi wa IRA, Profesa Nobert amesema ni jambo la kujivunia kwa chuo hicho kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaokutanisha vijana kutoka maeneo mbalimbali ulimwenguni.

Pia alibainisha baadhi ya sababuzilizofanya chuo hicho kuwa mwenyeji, ni pamoja na kuwa moja kati ya vyuo ambavyo vimejikita katika kufanya tafiti mbalimbali zinazohusu mabadiliko ya tabianchi.

Amesema mkutano huo utajadili mada mbalimbali kuhusu masuala ya mabadiliko ya tabianchi, jinsi ya kukabiliana nayo na kutoa suluhu endelevu.

Mwanaharakati wa mazingira na mwanzilishi wa taasisi ya Doors of Hope Foundation, Shamim Nyanda amesema kuwa anajisikia faraja kama kijana wa Tanzania kuona mkutano huo unafanyika nchini na kwamba vijana wameshirikishwa tangu hatua za awali za maandalizi.

Vilevile ametoa wito kwa vijana nchini kushiriki na kufuatilia mkutano huo ili waweze kujiongezea uelewa walionao katika masuala ya mapambano ya mabadiliko ya tabianchi duniani.

Kwa upande wake Kamishna wa Uhifadhi na Mkurugenzi Mtendaji wa TFS, Profesa Dos Santos amesema pamoja na kushiriki mkutano huo, washiriki watapata fursa ya kutembelea mashamba ya mikoko huko Mbweni pamoja na Msitu wa Pugu Kazimzumbwi.

"Ziara hizi zitatoa ufahamu wa vitendo katika uwanja wa uhifadhi, utalii wa mazingira, na maendeleo endelevu, kuwajengea viongozi vijana uwezo wa kupunguza na kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi," amesema.