Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kufanya mahafali ya 53 kihistoria

Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais mstaafu wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William A. L. Anangisye (wa pili kushoto) wakikabidhi bendera ya chuo kwa mhitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1983, Juan Jacomino Castellanos (kulia) kutoka Cuba katika mahafali ya 53 duru ya kwanza yaliyofanyika katika ukumbi wa Mlimani City, Mei 19, 2023.

Muktasari:

  •  Mahafali kufanyika katika duru nne ndani ya mwaka
  •  Idadi ya wahitimu wa kike yazidi kupaa.

Dar es Salaam. Kuna mahafali za vyuo vikuu vingine, halafu kuna mahafali ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Kuanzia mwaka huu, UDSM inakwenda kuandika historia mpya ya ufanyaji mahafali kwa namna bora zaidi, huku idadi ya wanafunzi watakaohitimu katika ngazi zote ikiwa kubwa zaidi.

Ongezeko la wanafunzi wanaodahiliwa na wanaohitimu inatajwa kama moja ya sababu za msingi za mabadiliko hayo, chuo hicho, hivi sasa kinakadiriwa kuwa na zaidi ya wanafunzi 44,000. Mbali ya ongezeko hilo, wingi wa vyuo vishiriki na kampasi za chuo hicho; ikiwamo Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere, Chuo Kikuu Kishiriki cha Mkwawa (MUCE), Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (DUCE), Ndaki ya Afya na Sayansi Tumizi (MCHAS), Ndaki ya Tehama (CoICT), Taasisi ya Sayansi za Bahari- Zanzibar na Kampasi ya Uvuvi iliyopo Kunduchi, ni sababu nyingine inayoipa mamlaka UDSM kubadili utamaduni wake wa kufanya mahafali, anaeleza Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Prof. Bonaventure Rutinwa.

“Chuo pia kimepokea fedha za Benki ya Dunia chini ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaolenga  kuleta maboresho katika taasisi za elimu ya juu nchini ambapo, kwa UDSM, pamoja na maboresho mbalimbali Chuoni, fedha hizo zitatumika pia katika upanuzi wa chuo kwa Kampasi ya Lindi na Kampasi ya Kagera,” anaeleza Prof. Rutinwa.

Anasema kuwa mwaka huu peke yake, kutakuwa na duru nne za mahafali ya chuo hicho huku duru ya kwanza ya mahafali ya 53 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ikiwa tayari imeshafanyika tangu Mei 19, 2023 ambayo ilihusisha utunuku wa vyeti kwa wahitimu 595 wa shahada za juu; ikiwamo shahada ya uzamili, astashahada ya juu na shahada ya uzamivu.

Anafafanua kuwa Oktoba 17, 2023, itakuwa ni duru la pili. Katika duru hiyo, wahitimu wapatao 2,796 wanatarajiwa kutunukiwa tuzo mbalimbali. Kwa shahada za awali wahitimu 2,700 watatunukiwa tuzo zao, wanaume wakiwa 1,212 na wanawake 1488, sawa na asilimia 55.1 ya wahitimu wote wa ngazi hiyo. Kwa upande wa stashahada, jumla ya wahitimu 78 wanatarajiwa kutunukiwa tuzo hiyo, wanaume wakiwa 45 na wanawake 33, sawa na asilimia 42.3 ya wahitimu wote wa ngazi hiyo.

Kwa ngazi ya astashahada, wahitimu wapatao 18 watatunukiwa tuzo, wanaume wakiwa 10 na wanawake 8, sawa na asilimia 44.4 ya wahitimu wote wa ngazi hiyo.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ally Mwinyi akimkabidhi Dk Kulwa Mtaki (kulia-) cheti cha Shahada ya Uzamivu katika Sayansi za Bahari baada ya kutunukiwa shahada hiyo na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais mstaafu wa Tanzania, Dk Jakaya Kikwete katika mahafali ya kwanza ya Taasisi ya Sayansi za Bahari yaliyofanyika Kampasi ya Buyu, Zanzibar Novemba 14, 2022.

Kada zitakazohusika katika duru hii ni pamoja na Ndaki ya Sayansi Asilia na Afua, Ndaki ya Insia, Ndaki ya Habari na Teknolojia za Habari, Shule Kuu ya Madini na Jiosayansi, Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma, Shule Kuu ya Biashara, Taasisi ya Taaluma za Kiswahili (TATAKI) na Taasisi ya Sayansi ya Bahari—Zanzibar, anaeleza Prof. Rutinwa.

Duru ya tatu inatarajiwa kufanyika Oktoba 19, 2023, huku wahitimu wapatao 2,609 wakitunukiwa tuzo mbalimbali. Duru hii itahusisha wahitimu wa ngazi za shahada za awali na astashahada pekee, ambapo kwa shahada za awali, jumla ya wahitimu 2,592 watatunikiwa tuzo hiyo, wanaume wakiwa 1,105 na wanawake 1,487, sawa na asilimia 57.4 ya wahitimu wote.

Kwa upande wa astashahada, jumla ya wahitimu 17 watatunikiwa tuzo hiyo huku wanaume wakiwa 12 na wanawake 5, sawa na asilimia 29.4 ya wahitimu wote, anaeleza. Kada zitakazohusika katika duru hii ni pamoja na Ndaki ya Kilimo na Sayansi ya Chakula, Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia, Ndaki ya Sayansi ya Jamii, Shule Kuu ya Uchumi, Shule ya Akwa na Teknolojia ya Uvuvi, Shule Kuu ya Sheria, Shule Kuu ya Ualimu na Taasisi ya Taaluma za Maendeleo.

Katika duru ya nne na ya mwisho itakayofanyika Novemba 30, 2023, Prof. Rutinwa anasema kuwa itahusisha wahitimu wote shahada za juu, wahitimu kutoka Ndaki ya Afya na Sayansi Tumizi – Mbeya na wahitimu wa shahada za awali waliokuwa na sifa ya kuhitimu pengine hawakuweza kuhitimu katika duru ya kwanza kwa sababu mbalimbali.

Katika mahafali ya 53 ya chuo hicho, wahitimu wa kike wamefikia asilimia 57 huku wanaume wakiwa asilimia 43 ya wahitimu wote kutoka asilimia 55 na wanaume wakiwa asilimia 45 katika mahafali ya 52 yaliyofanyika mwaka jana, ongezeko la asilimia 2 kwa jinsi zote.

Naibu Makamu Mkuu wa Chuo-Taaluma, Prof. Bonaventure Rutinwa.

Ongezeko hilo linaakisi kuongezeka kwa ufaulu wa wanafunzi, ikiwemo wa wanafunzi wa kike katika ngazi ya elimu ya sekondari na pia uwepo wa sera na mazingira bora ya masomo ambayo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimewekwa zinazowavutia wanafunzi wengi, hususan wa kike kujiunga na kusoma masomo mbalimbali hapa.

Jambo lingine la aina yake katika mahafali haya ni kuwa mahafali hayo yatashuhudia programu mpya zinazokwenda kutoa wahitimu kwa mara ya kwanza; ikiwamo Shahada ya Awali ya Sayansi katika Maikrobailojia Tumizi na Kemia, Shahada ya Awali ya Sayansi katika Kemia na Fizikia, Shahada ya Awali ya Elimu Jamii katika Historia, Usimamizi wa Turathi za Kitamaduni na Utalii na Shahada ya Awali ya Sayansi katika Uhandisi na Teknolojia.

Mahafali hayo yatafanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City huku yakitarajiwa kuhudhuriwa na Mkuu wa Chuo na Rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ujumbe wa viongozi waandamizi wa chuo, viongozi wa Serikali, wahitimu, wanafunzi na waandishi wa habari.