Ufanisi Bandari Dar wapaa, wabunge walilia uwekezaji

Dar/Dodoma. Wakati ripoti ya Benki ya Dunia (WB) ikionyesha kuwa ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam umeongezeka na kuipiku ile ya Mombasa nchini Kenya katika orodha ya bandari zenye ufanisi zaidi duniani, wabunge wameshauri bandari hiyo ibinafsishwe.

Hata hivyo, baadhi ya wachumi wametofautiana, kuna wanaounga mkono ubinafsishaji na wameshauri njia nzuri za kuongeza ufanisi, ikiwemo kutoa mkataba wa muda mrefu kwa kampuni itakayopewa tenda ya kupakua mizigo bandarini ili ifanye uwekezaji.

Kwa mujibu wa ripoti ya The Container Port Performance Index 2022 iliyotolewa siku chache zilizopita, bandari ya Dar es Salaam imepanda kwa nafasi 49 na kufikia nafasi ya 312 kutoka 361 mwaka 2021, huku bandari ya Mombasa ikishuka hadi kufika nafasi ya 326 mwaka 2022 kutoka 293 mwaka 2021.

Kupanda kwa nafasi hiyo kunaenda sambamba na ongezeko la mizigo inayohudumiwa kutoka tani milioni 15.742 mwaka wa fedha 2018/2019 hadi tani milioni 17.851 mwaka wa fedha 2021/2022 kwa mujibu wa Benki kuu ya Tanzania (BoT).

Akizungumzia ufanisi wa bandari, Plasduce Mbossa, Mkurugenzi Mkuu wa TPA alisema kupanda kwa nafasi ya bandari ya Dar es Salaam katika kuhudumia shehena ya makasha ni matokeo ya uwekezaji uliofanywa na Serikali.

Alisema Sh1 trilioni zilizowekezwa kupitia mradi wa maboresho wa Bandari ya Dar es Salaam zilihusisha uboreshaji wa Gati namba 1 hadi 7 kwa kuongeza kina chake hadi kufikia mita 14.5 kutoka mita 7 za hapo awali.

“Kuongezeka kwa kina katika gati hizo kunaruhusu meli za kizazi cha tatu kuegeshwa ambazo zina uwezo kwa kubeba makasha hadi kufikia 6,500 kwa pamoja ikilinganishwa na meli zilizokuwa zinaegeshwa hapo awali,” alisema.

Mbossa alisema kupitia maboresho hayo, idadi ya meli za makasha zimeongezeka mara mbili ya idadi iliyokuwa inahudumiwa awali kabla mradi huo haujatekelezwa.

Wakati Mbossa akitoa ufafanuzi huo, bungeni Jijini Dodoma jana, wabunge walitaka bandari hiyo ibinafsishwe wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mbunge wa Mvumi (CCM), Livingstone Lusinde alisema ubinafsishaji katika bandari siyo dhambi, lakini akashangazwa kwa nini kunakuwa na hofu ya kufanya hivyo.

“Hakuna dhambi kwa faida ya nchi, lengo ni kurahisisha uchukuaji wa bidhaa katika soko la ushindani, hivyo Serikali isijifungie,” alisema Lusinde.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema kumekuwa na mipango mingi ya kuzunguka inayosababisha kuwepo kwa ongezeko la gharama, hususani ucheleweshaji wa mizigo inayotolewa bandarini hapo.

Mbunge wa Singida Magharibi (CCM), Eribariki Kingu alisema kama itabinafsishwa itasaidia kufanya mambo mengi kuwa rahisi.

Alisema kuna ukiritimba mkubwa katika utoaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam aliodai husababisha ongezeko la gharama kwa wahusika.

Kauli ya wabunge hao iliungwa mkono na Profesa Samwel Wangwe, ambaye alitoa angalizo kuwa kabla ya kubinafsisha lazima kuwepo makubaliano.

“Lazima kuwepo na ushirikiano, huwezi kuwapa moja kwa moja kwa sababu ni uwekezaji muhimu kwa Taifa, endapo hili likifanyika litapunguza mzigo kwa Serikali kwa sababu itakuwa na uwekezaji wake na sekta binafsi na uwekezaji wake,” alisema Profesa Wangwe.

Hata hivyo, mtaalamu wa uchumi, Oscar Mkude alisema miongoni mwa yanayoweza kufanyika ili kuongeza ufanisi ni vyema kampuni itakayopewa tenda ya kupakua mizigo katika meli ipewe mkataba wa miaka mingi ili ifanye uwekezaji wa kutosha.

“Ukimpa miaka mitatu au minne ni ngumu kwake kutumia fedha nyingi katika uwekezaji kwa sababu biashara hairudishi fedha haraka, unaweza kufanya uwekezaji ukaanza kupata faida ndani ya miaka mitatu na mkataba wako unaisha na huna uhakika wa kuongezewa, ni ngumu kuweka fedha nyingi,” alisema Mkude.

Alisema jambo hilo linafanya kukosekana kwa vifaa vya kisasa na miundombinu ambayo ingechangamsha biashara.

Itakumbukwa kuwa Januari mosi, 2023 TPA kupitia taarifa kwa umma iliyotolewa na mkurugenzi wake mkuu, ilisema mkataba wao na Kampuni binafsi ya kuhudumia makontena (TICTS), ulifikia mwisho Desemba 31,2022, huku TPA ikibeba shughuli zote za bandari katika gati namba 8 na 11 za bandari ya Dar es Salaam.

Kutokana na hilo, Mkude alisema ni vyema kampuni zinazopewa kazi hizo pia ziwe na uwezo wa kufanya usafirishaji majini ili kuongeza ufanisi.

“Pia tuangalie muda ambao meli inatumia bandarini kushusha mzigo, ukiwa mchache zaidi tutafanya vizuri zaidi, chombo (meli) ikisimama muda mrefu na mizigo ni hasara kwetu na kwao,” alisema na kuongeza kuwa suala la uaminifu ni jambo ambalo linalopaswa kutupiwa jicho kwa kuwa kama utaondoka unaweza kuchafua hadhi ya bandari.

Naye Profesa Abel Kinyondo kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema ni vyema sekta nyingine zikaelekezwa kuwa saidizi kwa bandari ili kuongeza ufanisi.

Akitolea mfano uunganishaji wa kipande cha reli ya kisasa na bandari ya Dar es Salaam, alisema utasaidia kupunguza gharama za usafirishaji na kubeba mzigo mwingi kwa wakati mmoja, jambo litakalomsaidia mfanyabiashara.


Majibu ya Serikali

Kuhusu suala la ubinafsishaji, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alisema Serikali imepokea maoni na itakwenda kufanyia kazi suala hilo.

Akizungumzia utendaji kazi wa TPA, alisema mwaka 2015/2016 ilihudumia mizigo tani milioni 15.67 na mwaka 2022 ilihudumia tani 20.73 milioni sawa na ongezeko la asilimia 30.5 ambapo ni sawa na ongezeko la asilimia 4.3

“Ongezeko hili linaonekana ni kubwa lakini ni kidogo ikilinganishwa na mpango mkakati wa TPA ambao ulisema ongezeko wa mizigo lazima liwe kati ya asilimia 10 hadi 12.9 kwa mwaka” alisema

Alisema miongoni mwa changamato zilizochangia ukuaji huo mdogo ni uendesheji na ucheleweshaji wa mizigo nangani, uwekezaji mdogo katika uwekezaji wa mitambo ya kisasa, usimikaji wa mifumo ya tehema imesababisha ucheleweshaji utoaji mizigo na ujenzi wa magati.